SIRI YA KUDUMU HARAKATI YA IMAM HUSSEIN (A.S).
Ashura ni tukio ambalo imepita miaka 1373 tokea kujiri kwake lakini si tu kuwa tukio hili la kihistoria linawavutia Waislamu bali pia wapenda uhuru kote duniani wamevutiwa na yaliyojiri katika jangwa la Karbala.
Katika kipindi chote cha historia, kumejiri matukio mengi ambayo akthari yamesahaulika. Lakini tukio la Karbala ni la aina yake kwani tokea kujiri kwake hadi sasa limekuwa likivutia hisia za wengi na kuleta nuru katika nyoyo zilizokuwa kizani.
Siku ya 10 ya mwezi Muharram mwaka 61 Hijria Qamariya, kilio cha Imam Hussein AS na wafuasi wake cha kutaka haki kimebakia na kudumu katika kurasa historia. Leo kilio cha Imam Hussein AS kimewafikia watu wenye kiu cha kusikia kilio cha haki. Tuko katika siku za kukumbuka kuuawa shahidi Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS na wafuasi wake katika jangwa la Karbala.
Uislamu, umejengeka katika fitra na hii fitra inawatazama wanaadamu wote kuwa ni kitu kimoja. Ni kwa sababu hii ndio mwanaadmau katika maumbile yake ya dhati anamtafuta Mwenyezi Mungu, uadilifu, umaridadi , uhuru na maisha ya milele. Lakini baadhi ya wakati kutokana na kughafilika, madhambi au matukio ya kijamii, kiuchumi na kisiasa mwanadamu huondoka katika mkondo wa ujumbe wa fitra. Kwa hivyo jukumu kubwa zaidi la Mitume na viongozi wa kidini ni kuwatakasa wanadamu na kuwakumbusha kuhusu neema walizozisahau za Mwenyezi Mungu.
Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa jukumu kuu la Imam Hussein AS lilikuwa ni kuwaongoza wanaadamu katika njia sahihi na maadili bora zaidi ambayo yanaenda sambamba na fitra.
Imam Hussein AS alitaka kuondoa vizingiti vilivyokuwepo katika kufikia malengo haya ya juu. Kizingiti kikubwa katika njia hii kilikuwa ni utawala wa kiimla wa Bani Umayya ambao haukuwa ukiwapa watu fursa ili waweze kuitikia wito wa fitra. Kwa hivyo katika zama za utawala wa Bani Umayya, watu walikuwa mbali na masuala ya kutafuta haki, kupigania uhuru pamoja na kueneza maadili mema na uadilifu. Kilichojiri wakati huo ni kuenea ufisadi na ukatili na watu kupoteza ubinaadamu wao pamoja na thamani za kidini.
Katika zama hizo, Imam Hussein AS alianzisha harakati na mapambano ya kuwarejesha watu katika mafundisho ya kidini na thamani za juu za kibinaadamu. Nukta hii inaashiria muelekeo wa kimataifa wa mapambano ya Imam Hussein AS kwani harakati yake iliwahusu wanadamu wote.
Yamkini ni kwa sababu hii ndio Mahatma Gandhi kiongozi wa ukombozi India alisema kuwa harakati ya Ashura ilikuwa ilhamu ya harakati na mapambano yake dhidi ya mkoloni Muingereza.
Waandishi wengi wanaotetea haki duniani kama Kurt Frischler wa Ujerumani wamezungumzia adhama ya moyo na shakhsia ya juu ya Imam Hussein AS. Na hii ni kwa sababu mapamabno ya Imam Hussein AS yalikuwa mwamko wa kurejea katika thamani asili za mwanadamu na hivyo wito huu umekuwa wa kudumu kwa wote.
Imam Hussein AS alianzisha mapambano yake ili kutenganisha baina ya haki na batili. Alifahamu kuwa nguvu za utawala wa Yazid ulikuwa umejengeka katika misingi ya batili na iwapo ungeendelea hivyo, basi kungeshuhudiwa kuangamia kazi zote za mitume za kueneza uadilifu na ukweli. Kwa hivyo katika vikao vyake tafauti mtukufu huyo alifafanua na kuweka wazi haki na batili.
Kwa mtazamo wa Imam Hussein AS, batili huwa na nguvu ya kidhahiri na kupuuza mipaka ya mwenyezi Mungu na kupelekea kujitokeza kwa muundo wa utawala wa kiimla kisha kuwachukua watu mateka hadi kiasi ya wao kushindwa kutetea haki zao.
Tokea kuumbwa Adam kulikuwepo mapambano baina ya haki na batili na vita vingi katika historia ya mwanaadamu vilijiri kwa ajili ya hayo mawili. Katika kipindi muhimu zaidi, Imam Hussein AS alijitokeza kama mbeba bendera ya haki alipokabiliana na Yazid ambaye alikuwa mbeba bendera ya batili. Ili kulinda haki na kuweka wazi njia yake hadi siku ya qiyama, Imam Hussein AS, familia yake pamoja na wafuasi wake watiifu; wote kwa pamoja walitoa maisha yao muhanga. Ashura ni kielelezo cha vita vya daima baina ya haki na batili na thamani bora dhidi ya upotofu.
Ni kwa msingi huu ndio maana kama ambavyo tukio la Ashura limebakia hai na kudumu katika historia na jamii mbalimbali na hivyo kuwalinda wanaomuabudu Mwenyezi Mungu, wapiganiao uhuru na wanapoinga dhulma pia watabakia hai na kudumu siku zote.
Moja ya sababu nyingine za kudumu harakati adhimu ya Karbala ni uwazi wa mwamko huo. Imam Hussein AS wakati akianzisha mapambano yake makubwa, awali kabisa alibainisha utambulisho wa mapinduzi yake kwa njia ya wazi kabisa. Aliwafahamisha watu kuwa mapamabano yake yalilenga kupinga dhulma na kuhuisha Uislamu sambamba na kuwaokoa watu kutoka katika shari ya utawala wa Yazid. Alibainisha hata mbinu za mapambano ambazo zilipaswa zitumike.
Kwa hivyo, katika mapamabano ya Karbala kila kitu kilikuwa wazi ili katika mustakabali asijitokeze mtu kumkosoa Imam au apotee katika kufuata njia yake.
Imam Hussein AS katika wosia wake kwa Muhammad Hanafiyya aliweka wazi utambulisho wa mapambano yake na kusema yamejengeka katika msingi wa Kiislamu. Alisema mapambano yake yalikuwa na lengo la kutekeleza sheria za Kiislamu na kuangamiza utawala fisadi wa Bani Umayya na kuanzisha utawala adilifu wa Kialawi.
Mtukufu huyo vilevile katika kubainisha mbinu alizotumia kufikia malengo ya mapambano yake, alisisitiza kuhusu kuamurisha mema na kukataza mabaya ili kurekebisha jamii na kuwaokoa watu kutoka katika dhulma na utawala wa kiimla ambao haukuwa ukizingatia uadilifu. Imam aidha aliwataka watu watekeleze sira ya Mtume SAW na Imam Ali AS.
Imam Hussein AS akizungumza Makka alisema: "Ewe Allah! Unajua kile ambacho tunakifanya katika jamii si kwa sababu ya kupata mamlaka na utawala na wala si kwa ajili ya kupata utajiri. Sisi tunataka kuonyesha njia ya dini yako, tufanye marekebisho katika miji yako, waja wako waliodhulumiwa waishi katika utulivu na usalama na waweze kukutii Wewe pasina bughudha. Sisi tumeazimia kutekeleza yaliyofaradhishwa katika Uislamu, Suna ya Mtume SAW na sheria za Allah."
Mtukufu huyo katika hotuba yake aliashiria mahitajio ya kimsingi kabisa ya wanadamu. Je, inawezekana mapinduzi yajiri kwa sababu ya kufikia malengo ya kimsingi zaidi ya jamii za wanadamu na yasidumu milele?
Nukta nyingine iliyopelekea mapambano ya Ashura yawe ya kipekee ni kuwa, mwamko huu ulikuwa mwamko wa kiakhlaqi.
Katika historia kumejiri mapinduzi mengi ambayo yalitoa mhanga akhalqi katika mkondo wa mapambano. Lakini katika mapambano ya Karbala, suala la akhlaqi na maadili bora lilikuwa mhimili mkuu. Kuhusu hili tunaweza kuashiria hapa muamala wa Imam Hussein AS na maadui. Katika mapambano ya Karbala, mtukufu huyo hakuchukua hatua yoyote inayopingana na maadili ya Kiislamu.
Wakati Imam Hussein AS alipowasili Nainawa, Hurr ibn Yazid Ar-Riyahi kamanda wa jeshi la adui alipomlazimisha mtukufu huyu kukaa Karbala, Zuhair bin al Qain kati ya masahaba zake ambaye alikuwa kamanda maarufu wa kijeshi alimpa pendekezo Imam Hussein AS kuwa kutokana na kuwa idadi ya maadui walikuwa wachache katika kipindi hicho na wengine bado hawajafika, basi waanzishe vita. Lakini Imam alisema: "Mimi nazingatia msingi wa kiakhlaqi ambao ni kuwa sitakuwa mwanzishaji vita. Sisi hatutaanzisha vita na hawa." Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kuwa katika siku ya Ashura Hurr ibn Yazid Ar-Riyahi alitubu na Imam Hussein alikubali tauba yake.
Tukio la Ashura limejaa nukta nyingi ambazo zinaonyesha kuwa mapambano ya Karbala yalikuwa ya kiakhlaqi kabisa na yalifuata misingi ya kibinadamu na Kiislamu.
Ni kwa sababu hii ndio kila mtu awe Mwislamu au asiyekuwa Mwislamu anapoangalia mapambano ya Imam Hussein AS anayatazama mapambano hayo kwa mtazamo tafauti na kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na thamani za kiakhlaqi za harakati ya Imam Hussein AS.
Hakuna shaka kuwa mapambano na harakati ya Imam Hussein AS ni ya kipekee katika historia ya Kiislamu na dunia na kama alivyosema Shahid Mutahhari shakhsia ya Imam Hussein ni ya kipekee kabisa.
Mwamko wa Imam Hussein ni kielelezo cha hali ya juu cha thamani za kiakhlaqi na kibinadamu. Hii ni kwa sababu katika medani ya vita wakati huo, mapambano yalikuwa baina ya imani na umaanawi kwa upande moja na upande mkabala ukafiri na ufisadi. Waliopigana upande wa haki hawakuwa na budi ila kuibua hamasa na ushujaa. Kwa hivyo mapambano yaliyojawa hekima na kwa wakati wake ya Imam Hussein yamebakia kama johari yenye thamani katika historia na ujumbe wake unaendelea kufikia kizazi hadi kizazi kingine.
1 - MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA HAMASA YA 'ASHURA
Bismillahir Rahmanir Rahim. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika sehemu ya kwanza ya makala hii inayozungumzia mchango wa wanawake katika hamasa wa 'Ashura. Mwezi wa Muharram mwaka 61 Hijria ulipambika kwa mapambano ya kishujaa ya Imam Husain AS na wafuasi wake. Mapambano hayo ya yaliyopelekea kumwagika damu nyingi, yalikuwa na lengo la kuwaamsha watu na kuleta marekebisho katika jamii ya Kiislamu ambayo ilikuwa chini ya utawala kandamizi wa mtawala dikteta ambaye hakujali matukufu ya Kiislamu. Imam Sadiq AS anasema hivi katika Ziara ya Arubaini ya Husain kwamba: "Damu yake (Imam Husain AS) aliimwaga katika njia Yako (Ewe Mwenyezi Mungu) ili awatoe waja Wako katika ujinga, kuchanganyikiwa na kupotea."
Wakati wanawake wa Bani Hashim waliposikia kuwa Imam Husain AS ameazimia safari, waliitisha kikao cha pamoja ili kutaamali nini cha kufanya. Walikuwa na yakini kwamba Imam Husain AS hatorejea salama katika safari yake hiyo. Akinamama hao waliamua kutumia vilio na hisia za kuungulika mtimani ili kuonyesha majonzi yao ya nyoyoni. Imam Husain akajongea karibu nao na kuwasemeza akiwaambia: "Nakunasihini kwa Dhati ya Mwenyezi Mungu, Allah Allah msije mkaitangaza habari hii, ikaja ikawa ni kukhalifu amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake."
Akinamama wa Banii Hashim wakanena: Vipi tutahimili kujizuia kulia wakati siku hii ya leo kwetu ni sawa na siku alipofariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, ni sawa na siku alipouawa shahidi Ali na Faatima na ni mithili ya siku walipofariki dunia Ruqayyah, Zaynab na Ummukulthum, mabinti wa Bwana Mtume SAW? Husain wetu mpendwa! Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba tuachie tutoe fidia roho zetu kwa ajili yako ili wewe ubakie salama, tunakuomba kwa kusisitiza ewe mpendwa wa waja wema unayetutoka...
Nasaha za Imam Husain AS hazikusadia kitu na hazikuwanyamazisha akinamama wa Bani Hashim. Akinamama hao wakaelekea kwa Ummu Hani, shangazi wa Imam Husain AS na kumwambia: Ummu Hani! Vipi umekaa kimya wakati Husain na aila yake ndio hao tena wanakwenda?!
Ummu Hani akatoka kwa haraka sana kuelekea kwa Imam Husain. Baada ya kumuona tu, Imam alimwambia: Shangazi yangu mpendwa, kwa nini uso wako umesawijika kiasi chote hiki?
Ummu Hani akasema: Vipi nisisawijike wakati naona mlezi wa mayatima na watu wasio na pa kwenda, ananitoka?
Huku akishindwa kujizuia kububujikwa na machozi, Ummu Hani akaanza kutoa sifa za Husain AS akinena: Husain ni shakhsia tukufu ambaye watu wanaomba kupata baraka za mvua kwa utukufu wake. Husain ni chemchemu ya furaha za mayatima na ni mlezi wa watu wasio na pa kukimbilia. Husain ni katika kizazi cha Hashim ambaye anajitolea muhanga kwa ajili ya wengine. Wakati wanyonge walineemeka kwa fadhila na ukarimu yake, Husain pia, ni kipenzi cha Mtume wa Allah SAW. Husain hakosei na huu msiba mkubwa (wa kuuawa kwake shahidi), unabainisha wazi utukufu wa sira yake."
Imam Husain AS akamwambia: "Shangazi yangu mpenzi! Usiwe na wasiwasi halilatotokea ila lililopangwa na Mwenyezi Mungu. Watu hao hawawezi kumshinda mwana wa mshindi wa vita vyote (yaani mwana wa Imam Ali AS). Masuala haya yanakwenda kwa qudra na elimu ya ghaibu ya Mwenyezi Mungu."
Akinamama wa Bani Hashim ambao walimaizi kuwa Uislamu ulikuwa umefikishwa mahala ambapo usingeliweza kuokoka ila kwa kujitoa muhanga Imam Husani AS, walijitolea kwa roho na nyoyo zao kuandamana naye kuelekea kwenye medani ya mapambano.
***
Tarikh ya Uislamu ya tangu kudhihiri kwake, muda wote imeshuhudia mchango mkubwa wa akinamama katika medani za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi. Nafasi muhimu ya wanawake katika kila lahdha na sekunde ya historia ya Uislamu ni kitu kisichoweza kukanushika kabisa. Mapambano ya Karbala ni katika matukio muhimu na ya aina yake kabisa katika tarikh ya Uislamu. Mapambano hayo ni matunda ya pamoja ya ushujaa na kujitolea muhanga wanawake kwa wanaume katika njia ya Haki. Kwa maneno mengine ni kuwa, kama Uislamu ulihuishwa kwa mapambano ya Imam Husain AS huko Karbala, basi mchango mkubwa wa mapambano hayo ulitolewa na wanawake ambao hawajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia. Wanaume wote walioonyesha hamasa ya kupigiwa mfano huko Karbala walipata malezi kutoka kwa akinamama mashujaa waliopambika vizuri kiimani na weledi wa mambo, ambao walipata taufiki ya kuitunuku jamii ya Kiislamu watu mashujaa kama hao. Hivyo kuweko wanaume kama hao kwenye vita hivyo visivyo na mlingano sawa vya Karbala ni matunda ya kujitoa muhanga na kuwa na muono wa mbali akinamama. Subira na istikama ya wanawake waliokuwemo kwenye msafara wa Imam Husain AS nayo ilitoa mchango mkubwa sana kwa wafuasi wa Imam Husain AS waliopambana kiume hadi tone la mwisho la damu zao. Mchango huo wa akinamama ulianza hata kabla ya kuuawa shahidi Imam Husain AS kwa njia isiyo ya moja kwa moja na ulianza kwa kuwahamasisha waume na watoto wao kushiriki kwenye mapambano hayo matakatifu licha ya kujua kwamba wangeliuawa shahidi na mchango wao ulionekana zaidi baada ya tukio la 'Ashura ambapo akinamama hao walifanya kazi kubwa ya kutangaza malengo matukufu ya mapambano ya Karbala.
Wanawake wa Karbala walithibitisha kivitendo kuwa majukumu ya kijamii hayawahusu tu wanaume. Kila linapojitokeza suala la kuilinda dini na kusimamisha haki; wanadamu wote – iwe wanawake au wanaume – kila mmoja ana jukumu la kutoa mchango wake. Tab'an katika Uislamu si wajibu kwa wanawake kushiriki katika medani za mapambano na jihadi. Hata katika medani ya Karbala pia Imam Husain hakuwaingiza wanawake katika medani ya vita na ndio maana wanawake hawakushiriki kijeshi katika 'Ashura. Ni wanawake wawili tu ndio waliokwenda kwenye medani ya vita, lakini Imam Husain AS aliwashukuru na kuwaondoa kwenye medani hiyo. Mchango mkubwa wa akinamama katika kadhia ya Karbala ulikuwa ni kufikisha ujumbe wa mapambano hayo kwa walimwengu.
***
Kiujumla tunaweza kuugawa mchango wa wanawake kwenye hamasa ya Karbala katika mafungu matatu. Kabla ya 'Ashura, siku ya 'Ashura na baada ya 'Ashura.
Dulham, alikuwa mke wa Zuhayr ibn Qayn. Dulham alikuwa miongoni mwa wanawake ambao waliwahamisisha waume zao wajiunge na msafara wa Imam Husain AS katikati ya njia. Nafasi ya Dulham ilikuwa muhiumu kiasi kwamba kisa chake na mumewe Zuhayr ni vizuri nikikusimulieni hapa.
Wakati Zuhayr ibn Qayn alipokuwa anarejea kwao Iraq pamoja na kundi la watu wengine kutoka Makka walikotekeleza ibada ya Hija, alipata taarifa kuwa Imam Husain AS alikuwa amekataa kutoa bay'a na kutangaza utiifu wake kwa mtawala dhalimu wa wakati huo, Yazid bin Muawiya. Alipata taarifa pia kuwa Imam Husain alikuwa anaelekea Iraq na wafuasi wake na alikuwa na yakini kwamba uamuzi uliochukuliwa na Imam Husain AS ulikuwa wa haki, lakini hakutaka kuchanganya utamu wa ibada yake ya Hija na uzito wa vita na mapambano. Hivyo akajitahidi kadiri alivyoweza, ukwepa kukutana na msafara wa Imam Husain AS. Ikawa kila msafara wa Imam Husaini ulipokuwa ukipumzika, msafara wa Zuhayr uliendelea na safari na kila msafara wa Imam Husaini ulipoendelea na safari, msafara wa Zuhayr ulipumzika. Wakati msafara wa Zuhayr ulipokuwa amepiga kambi eneo la mbali na sehemu ya mahema yalipokuwepo Imam Husain kwa ajili ya kupumzika na kula chakula, ghafla Zuhayr alimuona mjumbe wa Imam Husain AS amefika kwake akimtaka Zuhayr aende kwa Imam. Watu wote waliokuwemo kwenye msafara huo wakapigwa na bumbuwazi na kila mmoja akawa anamuangalia mwenzake machoni. Zuhayr akajifanya hakusikia. Hapo hapo mke wa Zuhayr, yaani Dulham, binti wa Amru aliwashangaza wote aliposimama na kusema: Subhanallah! Mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW amekutumia mjumbe uende kwake wewe hutaki kwenda?! Unaogopa kitu gani, nenda ukamsikilize anachokuitia, hiyo ndiyo busara. Maneno hayo yalimlainisha Zuhayr na kumfanya aitikie mwito wa Imam. Aliporejea, uso wake ulionekana umejaa nuru, akamtaka mke wake amkusanyie vitu vyake ili aende akajiunge na msafara wa Imam Husain AS. Hata hivyo akamwambia mkewe kwamba, hataki afikwe na chochote kibaya mikononi mwake, hivyo anampa talaka ili arejee kwa wazee wake. Lakini Dulham alikuwa na mapenzi makubwa kwa mumewe, walikuwa wameishi pamoja kwa miaka mingi, maneno ya mumewe ya kumpa talaka yalimchoma na kumuumiza sana. Hata hivyo mapenzi yake kwa mumewe hayakuwa chochote mbele ya matakwa ya mwana wa Mtume. Alichosema Dulham kumwambia mumewe ilikuwa: "Natawakali kwa Mwenyezi Mungu. Namuomba anisaidie na akusaidie na wewe. Nakuomba siku ya Kiama unishike mkono na kunipeleka kwa Aba Abdillahil Husain AS ili aniombee shufaa."
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
2 - MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA HAMASA YA 'ASHURA
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji kusikiliza sehemu ya pili ya kipindi hiki maalumu kinachoelezea mchango wa wanawake katika Tukio 'Ashura, ni matarajio yetu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki, karibuni.
Mwezi wa Muharramu mwaka 61 Hijria ulipambika kwa mapambano ya kishujaa ya Imam Hussein AS na wafuasi wake. Mapambano hayo ya umwagaji damu yalikuwa na lengo la kuwaamsha watu na kuleta marekebisho katika jamii ya Kiislamu ambayo ilikuwa chini ya utawala kandamizi wa mtawala dikteta ambaye hakujali matukufu ya Kiislamu. Karbala ijapokuwa ni eneo la jangwani na lisilokuwa na ukubwa wa kiasi hicho wakati huo, amma ardhi hiyo ilikuwa uwanja wa hamasa kubwa iliyokuwa imejaa vigezo vyote vikuu vya dini kutokea masuala ya kiakhlaki, imani, kuchukua uongozi hadi sala, kuamrisha mema na kukataza maovu, subira, urafiki, upendo na kujitolea. Ijapokuwa wahamasishaji wa tukio la Ashura walikuwa wachache, amma walikuwepo watoto wachanga waliokua wakinyonya hadi vijana wadogo, mabarobaro kwa watu wazima na waume kwa wanawake katika kulinawirisha tukio hilo. Kwa mtazamo mpana wa tukio la 'Ashura, Mwenyezi Mungu aliweza kumpa mwanamke mazingatio maalumu katika kuonyesha uwezo wake wote wa kutekeleza majukumu yake makubwa na hatimaye kutoa funzo na somo la kutetea haki kwa watu wengine. Katika ardhi ya Karbala, pamoja na kuuawa shahidi wapenzi na wapendwa wao, wanawake walitekeleza kwa njia bora zaidi nafasi mbalimbali za kibaba, kimama na kidada ili vizazi vijavyo viwe na umaanawi na kusimama kidete katika kukabiliana na udhalilishaji unaotokana na utamaduni kandamizi wa kimaada, na hatimaye kuweka mitazamo mipya ya kidini ulimwenguni. Wanawake wa Kiislamu katika uwanja wa Karbala wameweza kuwathibitishia walimwengu kwamba walikuwa na uelewa mkubwa wa mambo kinyume na wanavyoeleza wale wanaodai kutetea haki za binadamu eti walikuwa mbali na masuala ya kijamii na kisiasa. Wanawake katika tukio la 'Ashura hawakuhitaji uangalizi, uungaji mkono wala usaidizi, bali wao wenyewe walikuwa walinzi na wasaidizi watiifu wa wapiganaji wa Imam Hussein AS. Kwa minajili hiyo, inaonyesha ni kwa jinsi gani wanawake walivyokuwa na imani, uelewa, busura na kukubali majukumu katika tukio hilo adhimu.
*********
Katika uwanja wa Naynawa, kulikuwa na mapambano kati ya haki na batili, vijana waliingia kwenye medani wakiwa na shauku kubwa ya kuwalinda watoto wa Mtume Mtukufu SAW, huku wanawake wakiwa wameshikamana barabara na hamasa zao. Akina mama kadhaa waliokuwepo kwenye ardhi ya Karbala, waliwashuhudia watoto wakivaa mavazi ya kivita huku wakiwa na matarajio ya kuwaona watoto wao wakipata daraja la ushahidi. Maadui wa Uislamu baada ya kuwauwa shahidi watoto hao waliwakata vichwa, na kwa manyanyaso na udhalilishaji mkubwa, walivitupa vichwa hivyo mbele ya mama zao! Amma akina mama walitoa radiamali ya kivitendo na kusisitiza kwamba, kile walichokitoa kwenye njia ya Mwenyezi Mungu kamwe hawakirejeshi, matamshi yaliyowashangaza mno maadui hao wa Uislamu. Miongoni mwa wanawake hao, walikuwepo wanawake watatu ambao ni wake za masahaba wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW.
Amru bin Junadah alikuwa kijana mwenye nguvu. Hayakupita masaa mengi tokea alipotengana na baba yake aliyeuawa shahidi. Kijana huyo alimwendea mama yake kwa shabaha ya kumpa pole na kuomboleza naye msiba wa baba yake. Amma mama yake alimuambia kijana wake: 'Mwanangu ondoka pambizoni mwangu, nenda kwenye uwanja wa mapambano na upambane dhidi ya maadui wanaopigana na mtoto wa Mtume Mtukufu SAW'. Amru alitaka kuelekea kwenye uwanja wa vita, lakini Imam Hussein AS alisema: 'Baba wa mtoto huyu ameuawa, bila shaka kuuawa kwa mtoto huyu kutakuwa msiba mwingine mkubwa kwa mama yake'. Kijana Amru akajibu: 'Baba na mama yangu wawe fidia kwako! Mama yangu ameniamuru niingie kwenye medani ya vita na nipigane katika njia yako'. Kijana huyo akaanza kusoma shairi la kujisifu kwa kusema: 'Kiongozi wangu Hussein, kiongozi bora zaidi; Hussein ni furaha ya moyo wa Mtume, Hussein ni mtoto wa Ali na Fatima, Je, mnamfahamu kiongozi mithili yake? Sura yake mithili ya jua angavu, uso wake unavyong'aa ni mithili ya mwezi wa usiku wa mwezi kumi na nne. '
Kijana Amru bila ya khofu wala woga alipigana kwa ushujaa mkubwa na kuwauwa wapiganaji kadhaa wa upande wa adui. Hatimaye, kundi la wapiganaji wa adui lilimzingira kijana huyo na kumuuwa shahidi. Kisha kichwa cha Amru kilitenganishwa na kiwiliwili chake na kikatupwa upande lilipokuwa jeshi la Imam Hussein AS. Mama yake Amru alikikimbilia kichwa cha mwanawe na kukiokota kichwa hicho na kukikumbatia kifuani mwake na kisha akasema: 'Hongera, hongera mwanangu, ewe furaha ya moyo wangu na nuru ya macho yangu! Kisha akakitupa kichwa cha mwanawe upande wa maadui na kusema: 'Kile tulichokitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, hatukichukui. Kisha mama yake Amru akiwa na hasira na ukamavu mkubwa alichomoa nguzo ya hema na kuwapiga nayo kichwani na kuwauwa maadui wawili! Lakini Imam Hussein AS alielekea haraka kwa mama Amru na kumtaka arejee hemani, na mama huyo kutii takwa la mjukuu wa Mtume Muhammad SAW.
********
Wasikilizaji wapenzi, maadui walikua maelfu kwa maelfu na kila wakati walikuwa wakikabiliana na wafuasi 72 tu wa Imam Hussein AS na kuwauwa shahidi mmoja baada ya mwingine. Ikawadia zamu ya Abdullah bin U'mair, ambapo katika sanadi nyingine anajulikana kwa jina la Wahab bin Abdullah. Shakhsia huyo alijitolea na kujisabilia kwa Imam Hussein AS na kuingia kwenye medani ya vita. Wahab alikuwa na nguvu mno, alishambulia kundi la maadui na kuwauwa baadhi yao. Kisha alimuelekea mama yake Ummu Wahab na kumuuliza: 'Ewe mama yangu, uko radhi nami?' Mama yake akamwambia: 'Siwezi kuwa radhi nawe, mpaka pale utakapokuwa bega kwa bega na Imam Hussein AS na kumsaidia katika kuwauwa maadui! Wahab kwa mara nyingine tena alirejea kwenye medani ya vita. Allamah Majlisi ameandika: 'Maadui walimkamata mateka Wahab baada ya kuwauwa kwa ushujaa mkubwa wanajeshi 24 wa Umar Sa'ad na kuwajeruhi wapanda farasi 12'. Walimpeleka Wahab mbele ya kamanda wa jeshi la adui, na Umar Sa'ad alistaajabishwa na ushujaa wa kijana huyo na kusema: 'Una ushujaa na nguvu za ajabu?' Kisha walimuua shahidi kwa ukatili mkubwa. Mama wa Abdullah kwa haraka alimuelekea mtoto wake na kuupangusa mwili wake uliokuwa umetapakaa vumbi na kusema; 'Mwanagu, umesibu kupata pepo.' Baadaye Shimr bin Jawshan mmoja kati ya viongozi wa jeshi la adui, alimuamuru mpiganaji wake mmoja kumpiga kichwani mama huyo, kipigo ambacho baadaye kilimpatia daraja la ushahidi na kuhesabiwa kuwa mwanamke wa kwanza kuuawa shahidi katika ardhi ya Karbala.
Kabla ya kuuawa shahidi mama huyo, wanajeshi wa jeshi la Yazid walikikata kichwa cha Abdullah bin U'mair na kisha kumtupia mama yake. Mama kwa ujasiri mkubwa alikiokota kichwa hicho cha mwanawe, akakibusu na kisha akakitupa upande wa maadui na kutaka kuwashambulia maadui. Katika hali hiyo nyeti, Imam Hussein AS aliingilia kati na kusema: 'Rejea, mwanamke hapaswi kupigana jihadi, wewe na mtoto wako muna nafasi yenu peponi pamoja na babu yangu Muhammad SAW. Namuomba Mwenyezi Mungu asikate matarajio yako.'
Moyo wa muqawama na ustahamilivu wa wanawake katika tukio la Karbala ni miongoni mwa darsa na mafunzo muhimu ya 'Ashura. Kwani wanawake hao walitambua kwamba Hussein AS ni dhihirisho la haki na uadilifu na Yazid ni nembo ya wazi kabisa ya batili. Batili huenda ikapata nguvu na kuishinda haki kidhahiri, amma malengo ya kupigania haki kamwe hayawezi kutoweka, bali daima hubaki hai na kuendelea kubainishwa kwa uwazi kabisa katika historia. Kwa mtazamo huo, wanawake wa Karbala licha ya kuwa na huzuni kubwa kwenye nyoyo zao, amma hawakulia sana wakati wa kuagana na kutengana na wapendwa wao waliokuwa wakipigania haki dhidi ya batili. Wanawake hao walipokuwa wakiiona miili ya waume au watoto zao ikiwa imetapakaa damu na kukatwa vipande vipande, hawakulia hata kidogo mbele ya Imam Hussein AS, kwani kufanya hivyo kungemtia huzuni na uchungu mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW. Hata kile kipindi alipouawa shahidi Ali Asghar mtoto mchanga anayenyonya wa Imam Hussein anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi sita, Rubab mama wa mtoto huyo hakusogea mbele kwa kuhofia kwamba Imam Hussein AS angelishuhudia hali ile na kuhuzunishwa na hatua yake ya kumlilia mwanawe. Wanawake hao walijifakharisha kuwa bega kwa bega na wasaidizi wa mjukuu wa Mtume SAW, na walikuwa wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa taufiki hiyo.
Naam wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi hiki maalumu kilichoelezea mchango wa wanawake katika tukio la A'shura umefikia tamati.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
3 - MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA HAMASA YA 'ASHURA
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu ya tatu ya mfululizo huu maalumu unaozungumzia nafasi ya wanawake katika tukio la kihistoria la Ashura lilitokea mwaka 61 Hijria katika ardhi ya Karbala huko Iraq.
****
Ashura ni chemchemi ambayo daima ni yenye kutoa msukumo wa harakati baina ya vizazi vya mwanadamu. Katika harakati adhimu ya Imam Hussein bin Ali AS mjukuu wa Mtukufu Bwana Mtume SAW, wanawake walikuwa na nafasi muhimu mno kutokana na kutambua wakati, masuuliya na majukumu na mambo hayo yanatajwa kuwa yalikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa katika kubakia na kuendelea kwa harakati iliyoanzishwa na Imam Hussein AS ya kusimama na kupambana na dhulma, madhalimu pamoja na upotoshaji dini. Kuwa na mtazamo mpana na welewa wa dini ulioambatana na mapenzi aali kwa rudhia na Ahlul Bayt wa Mtume SAW ni miongoni mwa zilizokuwa sifa maalumu za wanawake waliokuwako katika harakati ya 'Ashura. Kwa hakika wao walifasiri na kutoa maana na fasili ya maneno kama huba, mapenzi, kujitolea, kusubiri, muqawama, na kusimama kidete katika kumlinda Imam Hussein. Wanawake hao waliotengeneza historia, licha ya kuwa kama walivyo wanawake wengine uwepo wao ulikuwa umejaa, huba, huruma na mapenzi kwa ajili ya watoto na waume zao, lakini hawakuruhusu hisia zao ziwatale wakati wa kutetea dini na matukufu yake yaliyojidhihirisha na kujipamba katika harakati na mapambano ya Imam Hussein AS. Kwa mtazamo wao ni kuwa, jukumu la Waislamu ni kuwa na welewa na muono wa mbali kuhusiana na dini sanjari na kuwa na ufahamu kuhusiana na maarifa ya Ahlul Bayt wa Mtume SAW na kuwa na urafiki nao, urafiki ambao unaambatana na huba na mapenzi kwao; kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Sura ya Ash Shura aya ya 23:
Sema, Siwaombi ujira isipokuwa mapenzi katika ndugu (yaani kwa kizazi changu).
Katika masiku ya mwisho ya maisha yake, Imam Hussein AS akiwa amezingirwa na maadui, alitumia fursa hiyo kuwatimizia hoja masahaba zake na kuwaambia kwamba, wanaweza kukhitari na kuchagua baina ya kuondoka katika medani ya vita na madhalimu na hivyo kusalimisha roho zao au kubakia na kuuawa. Imam alisema kuwahutu masahaba zake, "kila mtu ambaye amekuja hapa na ahli na famia yake, usiku huu huu anaweza kuichukua familia yake na kuipeleka sehemu yenye amani na usalama, kwani kesho watu watauawa na familia yangu itachukuliwa mateka."
Lakini wanawake waliokuwa katika medani hiyo, walisimama kidete tena bila kutetereka na kuwataka waume zao wawe bega kwa bega na Imam Hussein na Ahlul Bayt wa Mtume SAW.
*****
Tukio la Ashura ni tukio muhimu ambapo wanawake na wanaume kila mmoja yaani mwanamke na mwanaume alikuwa na nafasi na mchango wake. Uislamu unajifakharisha kwamba, kwa karne kadhaa hata kabla ya kujitokeza mapote mapya haya yanayodai kutetea haki za binadamu, dini hii tukufu ilikuwa imempatia mwanamke haki zake kwa mujibu wa fitra na maumbile yake. Tukirejea katika historia ya Uislamu tunapata kwamba, Mtume SAW alifanya hima na idili kubwa kwa ajili ya kunyanyua kiwango cha ufahamu cha wanawake pamoja na utamaduni wao. Mtume SAW alikuwa akimleta mwalimu kwa ajili ya watu wa nyumbani kwake. Wakati mwingine baadhi ya wanawake walikuwa wakiambatana na binti yake vitani kwa ajili ya kuwatibu majeruhi wa vita. Aidha warithi wake yaani maimamu watoharifu, nao walifanya jitihada kubwa katika suala la malezi na mafunzo kwa wanawake na kwa hima na idili yao, jamii ikaondokea kupata wanawake wenye kujitolea, wa kupigiwa mfano na wasio na kifani. Matunda ya juhudi hizo tunaweza kuyashuhudia wazi na wadhiha baina ya wanawake waliokuwako katika msafara na kafila ya Imam Hussein AS katika ardhi ya Karbala. Baadhi ya wanawake waliokuwako katika ardhi ya Karbala na katika tukio la Karbala ni watoto wa Imam Ali kama vile Zaynab, Ummu Kulthum, Fatima na Safia. Aidha walikuweko pia mabinti wa Imam Hussein As yaani Fatima, Sukaina, na Ruqaiyyah pamoja na mkewe Imam Hussein aliyejulikana kwa jina la Ummu Rubab na A'tikah mke wa Imam Hassan AS.
Bibi Zaynab AS binti mkubwa Imam Ali AS na dada yake Imam Hussein AS ni miongoni mwa majina ya wanawake yanayong'ara katika tukio la Ashura. Bi Zaynab ambaye amezikwa huko nchini Syria, alikuweko tangu mwanzoni mwa mwa harakati ya Imam Hussein pamoja na watoto wake wawili wa kiume. Katika usiku wa kuamkia Ashura, baada ya hali ya vita na kuuawa shahidi kueleweka kwa kila mtu na baada ya Bi Zaynab kushuhudia kwamba, masahaba wa Imam Hussein AS wanakwenda kumuona Imam hali ya kuwa wana shauku na hamasa kubwa iliyoambatana na furaha ya kusimama na kumtetea mjukuu wa Bwana Mtume SAW alifurahi mno. Aliondoka na kwenda kumuona kaka yake huyo hali ya kuwa ni mwenye tabasamu na bashasha kubwa. Imam Hussein baada ya kumuona dada yake akiwa katika hali hiyo alisema, Dada yangu mpenzi, tangu tuondokea Madina, katu sijawahi kukuona ukiwa unatasamu namna hii, umepata khabari gani ambayo imekufurahisha kiasi hiki na kukufanya uonekane ni mwenye furaha namna hii? Bi Zaynab alimjibu Imam Hussein kwa kuashiria utiifu na himaya ya masahaba wa kaka yake. Imam Hussein baada ya kusikia maneno ya Bi Zaynab akasema, dada yangu mpenzi, tambua kwamba, masahaba ambao wako bega kwa bega na mimi ni marafiki na masahaba wangu. Babu yangu Mtume SAW aliniahidi kuhusiana na utiifu na urafiki wao kwangu."
*****
Historia inaonesha kuwa, baada ya tukio la kuhuzunisha na kutia simanzi la Karbala, Bi Zaynab AS alisimama kidete na kukabiliana barabara na dhulma za watawala madhalimu na majahili wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein AS. Kwa hakika maneno na muamala wa wanawake waliokuwa katika harakati ya Imam Hussein huko katika ardhi ya Karbala ni mambo ambayo mtu akiyatazama anaona ni kwa kiasi gani wanawake hawa walikuwa watiifu, waliokuwa na moyo wa subira na walijitolea na kuonyesha ushujaa wa hali ya juu wa kuvumilia taabu na masaibu. Wanawake hao licha ya kukabiliwa na masaibu na kushuhudia kwa macho yao mauaji ya kinyama kabisa yaliyofanywa na jeshi la batili la Yazid bin Muawiya, walisimama kidete na kutotetereka katika kumtetea mjukuu wa Mtume SAW Imam Hussein bin Ali AS. Bibi Zaynab AS binti wa Imam Ali bin Abi Talib alionesha adhama kubwa katika harakati ya Karbala. Adhama ya bibi mwema huyo na yale yaliyonukuliwa kumhusu kuhusiana na msimamo wake thabiti katika mapambano ya Karbala ni jambo linaloonesha adhama na kusimama kidete bibi huyu katika njia ya haki. Kwa hakika subira ya Bibi Zaynab AS katika tukio la Karbala haina mithili. Ikiwa imepita nusu siku tu tangu kaka yake, mtoto wa kaka yake na watoto wake wawili wauawe shahidi mbele ya macho yake katika uwanja wa Karbala, alisimama kando ya kiwiwili cha kaka yake yaani Imam Hussein na akiwa na moyo thabiti na irada kamili alimtaka Mwenyezi Mungu apokee udh'hiya huo wa dhuria ya Bwana Mtume SAW.
السلام علی الحسین
و علی علی بن الحسین
و علی اولاد الحسین
و علی اصحاب الحسین
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabaraakatuh.
IMAM HUSSEIN (A.S) ALIHUISHA UISLAMU.
Katika historia ya jamii ya mwanaadamu maisha yamekuwa yakiendelea na kuandamana na matukio mbali mbali. Ni wazi kuwa baadhi ya matukio ya zama tofauti si tu kuwa hayawezi kufutika bali pia hubakia na kung'ara katika kursa za historia na kuteka fikra na mitazamo ya wengi.
Mnamo mwaka 61 Hijria Qamaria, historia ilishuhudia tukio muhimu ambalo licha ya kupita karne nyingi lakini bado ni ilhamu kwa matukio mengi ya kijamii na kisiasa.
Hapa tunakusudia Hamasa ya Imam Hussein AS katika ardhi ya Karbala. Hii ni hamasa ambayo imebakia katika zama na maeneo yote. Ni hamasa ambayo imevuka mipaka ya kijiografia na kihistoria na kuwa ilhamu na mfano wa kuigwa katika zama zote za jamii ya mwanadamu.
Tuko katika siku za awali za mwezi wa Muharram, kumbukumbu ya hamasa adhimu ya Karbala. Tunatoa salamu zetu kwa Hussein bin Ali AS. Salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Imamu huyo mkubwa ambaye alinawiri katika kilele cha karama na heshima ili aweze kumpa mwanadamau somo la maisha ambalo litabakia na kudumu milele. Salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Imam Hussein AS na wafuasi wake watiifu, ambao walitoa maisha yao muhanga kwa ajili ya kuinua Uislamu.
Imam Hussein AS alianzisha harakati yake takatifu wakati ambao utamaduni na mafundisho asili ya Kiislamu yalikuwa katika hatari ya kupotoshwa.
Imam Hussein AS alikuwa akishuhudia namna malengo na mafundisho ya Mtume Muhammad SAW yalivyokuwa yakisahauliwa hatua kwa hatua huku Bani Ummaya wakiwatawala watu kwa mabavu na hadaa.
Kutokana na kuwa moja ya majukumu muhimu ya uongozi katika Uislamu ni kuuongoza umma katika njia ya haki, Imam Hussein AS aliamua kuwa ni jukumu lake kusimama na kupambana dhidi ya upotofu uliokuwepo katika zama zake. Ni kwa sababu hii ndio mtukufu huyo alisema: "Mfahamu kuwa hawa (Bani Ummaya) wako pamoja na shetani, wameacha kutii amri za Allah na wanaeneza ufisadi wazi wazi. Wamekiuka mipaka ya Allah na kupora mali ya umma na kuifanya kuwa yao. Wameyafanya yaliyoharamishwa na Allah kuwa halali na kuhalalisha yaliyoharamishwa na Allah."
Kwa kuzingatia hotuba hii tunaweza kufahamu kuwa msingi mkuu wa harakati ya Imam Hussein AS ulikuwa ni kuhuisha na kuimarisha thamani za kidini katika jamii. Mtukufu huyo alisema hivi kuhusu sababu ya mapambano yake dhidi ya hali mbaya iliyokuwepo:
"Ewe Allah! Wewe unajua kuwa kile ambacho tunakisema si kwa ajili ya kuwania utawala na wala si kwa ajili ya kuipenda dunia bali ni kwa ajili ya kuiona dini yako ikiwa imesimama na kuleta marekebisho katika ardhi zako na kuwasaidia waja wako waliodhulumiwa ili majukumu na hukumu za kidini ziweze kutekelezwa."
Maneno haya ya Imam Hussein AS yanaashiria kuporomoka umaanawi katika jamii ya Kiislamu ya zama hizo. Katika upande mwingine, kitendo cha watawala kupora mali na kueneza bidaa na khurafat sambamba na kusahauliwa Masahaba wa Mtume SAW na kutengwa Ahlul Bait wa mtukufu huyo, yote hayo yalikuwa yameandaa mazingira ya kurejea jamii katika zama za ujahiliya. Katika wakati wa utawala wa Bani Ummaya, ukabila na kujifakharisha kwa msingi wa rangi au kaumu, mambo ambayo yalipingwa vikali na Mtume, yalianza kuibuka tena katika jamii.
Tafsiri potofu kuhusu dini, kuibuliwa hadithi bandia na kuenezwa habari za uongo ni mambo ambayo yalipelekea watu kuwa na shaka kuhusu thamani halisi za kidini na hivyo kuwachanganya kuhusu muongozo sahihi.
Bani Ummaya kwa kueneza hadithi bandia kutoka kwa Mtume SAW na Masahaba zake walijiarifisha kuwa warithi wa Mtume.
Katika upande mwingine, tabia ya Bani Umayya ya kuhodhi kila kitu na kujitakia makuu ni mambo ambayo yalipelekea kuwepo ukosefu mkubwa wa usawa katika muundo wa kiuchumi katika jamii. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba pote la wachache waliokuwa wakitawala na wapambe wao walitumia fedha za umma au baitul mal kujitajirisha na kuishi maisha ya raha mstarehe huku wananchi waliowengi wakiishi katika mbano mkubwa wa kiuchumi. Hali hii mbya pamoja na upotofu wa kiitikadi na kijamii ulifika kileleni wakati wa utawala wa Yazid bin Muawiyya.
Mashinikizo na hitilafu za kisiasa katika zama za ukhalifa wa Bani Ummaya zilipelekea kuibuka hofu na wasiwasi katika umma kiasi kwamba watu hawakuthubutu kutetea haki zao.
Aghalabu ya watu mashuhuri katika jamii na wasomi wakubwa wa kidini walinyamaza kimya kwa kuhofia ukandamizaji na udhalimu wa Bani Umayya na hata walitoa wito kwa Imam Hussein AS asalimu amri kwa hali hiyo. Kidhahiri watu wote walikuwa wakiswali, kufunga na kuenda hija lakini swali linaloiibuka ni hili kuwa je, amali na ibada zao zilikuwa na athari na natija iliyokusudiwa maishani?
Ni kwa nini Waislamu wa zama hizo walionyesha kutojali kuhusu matukio ya kijamii na kisiasa katika mazingira hayo?
Kwa sentensi moja tunaweza kusema kuwa kulikuwa na ufa baina yao na uhakika wa dini. Ujahili na kutofahamu masuala ya kisiasa na kijamii kulizusha matatizo katika upambanuzi baina ya haki na batili, na wala hawakujua waelekee wapi.
Kufuata dunia na kusahau umaanawi ni jambo ambalo liliwashughulisha zaidi watu kuliko suala jingine lolote. Kuhusu hili, Imam Hussein AS alisema: "Mnaona namna ahadi ya Mwenyezi Mungu inavyovunjwa, lakini hamsemi chochote na wala haiwaingii hofu. Katika hali ambayo mnapiga mayowe pale baadhi ya ahadi za baba zenu zinapovunjwa, lakini hamlipi umuhimu suala la kupuuzwa ahadi za Rasulullah SAW." Tuhaf Al Uqul Uk. 237
Katika hali hii ya kusikitisha ni kipi kingeweza kufanyika ili kuinusuru dini kutoka kwenye makucha ya madhalimu?
Imam Hussein AS aliposhuhudia hali hii, alichukua hatua za kuzuia kuporomoka umma kifikra na aliamini kuwa si tu katika masuala ya kiitikadi na kimaanawi, bali pia katika masuala ya kijamii na kisiasa kulihitajika marekebisho na mabadiliko ya kina na kimsingi katika jamii. Labda kama Imam angechukua hatua ya harakati ya kiakhlaqi na kiutamaduni tu, hangefanikiwa kuufahamisha umma kile kilichokuwa kikiusibu.
Kwa hivyo ili kuiondoa dini katika tatizo hili kubwa, hatua ya awali ilikuwa ni kutoutambua rasmi utawala wa Yazid na pili kujitoa muhanga kwa ajili ya mapambano haya yenye kuainisha hatima.
Imam Hussein AS aliwasilisha mpango sahihi wa mfumo wa Mwenyezi Mungu uliojengeka juu ya msingi wa kumtii imamu muadilifu na kulaani tabia za mtawala dhalimu. Imam alibainisha nadharia ya kimantiki ya dini ya Kiislamu kwa kutegemea kauli ya Rasulullah SAW kwa kusema: "Kila ambaye anamuona mtawala dhalimu anaharamisha aliyohalalisha Allah na kunyamaza kimya na kutoonyesha radiamali yoyote, basi Mwenyezi Mungu atamhukumu." Tuhaf Al Uqul Uk. 505
Maneno haya ya Imam ni nembo ya hati ya kiitikadi na kifikra ya umma. Lakini ubabe wa kisiasa na kiutamaduni wa Bani Ummaya ni jambo ambalo lilipelekea ujumbe huu usienee miongoni mwa Waislamu na kizuizi hiki kilikuwa chanzo cha ujahili na kutotambua mambo watu na hivyo kuandalia Bani Umayya mazingira ya kuukandamiza zaidi Umma wa Kiislamu.
Imam Hussein AS alifahamu ukweli kuwa madhalimu waliweza kuwatawala Waislamu kwa kudai kuwa wanafuata dini. Madhalimu hao walijitahidi kutumia mbinu mpya kuhuisha Ujahiliya uliokuwepo kabla ya Uislamu. Walihalalisha yaliyokuwa yameharamishwa na Allah na kuharamisha aliyoyahalalisha. Ni kwa sababu hii ndio wakati Imam Hussein AS alipobainisha lengo la mwamko wake wa kukabiliana na Yazid alisema hivi:
'Mimi nimejitokeza kwa ajili ya kuurekebisha umma wa babu yangu. Ninataka kuamurisha mema na kukataza mabaya na kuenda kwa mujibu wa Seerah na Sunna ya babu yangu, Rasulullah SAW.'
Imam katika falsafa ya harakati yake alibainisha suala la kurekebisha umma na kuhuisha Seerah ya Rasullah SAW. Kimsingi aliwataka watu watambue kuwa mushkili katika Umma wa Kiislamu ulitokana na wao kujiweka mbali na Sunna ya Mtume SAW. Imam Hussein AS alifahamu kuwa upotofu uliokuwepo ulikuwa unahatarisha fikra za Kiislamu na iwapo hali hiyo ingeruhusiwa kuendelea basi sehemu kubwa ya mafundisho halisi ya kidini yangetengwa na kile ambacho kingebakia katika Uislamu ni dhahiri tu pasina kuwepo na chochote cha maana. Baada ya kubainika ufisadi na upinzani wa wazi wa Yazid dhidi ya mafundisho ya kidini, haikujuzu tena kunyamaza kimya. Hii ni kwa sababu yamkini kimya kingepelekea kupotoea yale yote yaliyoletwa na Mtume SAW. Kimsingi harakati ya Imam Hussein AS ilikuwa onyo kwa umma wa Kiislamu. Onyo kwa zama zote za historia na kwa hivyo tokea wakati huo, harakati ya mtukufu huyo imekuwa ni ilhamu kwa wanaharakati wote wa Kiislamu. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa chanzo kikuu cha harakati ya Imam Hussein AS ilikuwa ni kujaribu kuonyesha Uislamu wa kweli katika jamii iliyokuwa imepotea wakati huo. Ni kwa sababu hii ndio katika kutathmini mapambano ya Imam Hussein AS, tukasema kuwa mtukufu huyo alihuisha tena Uislamu.Bottom of Form.
RIWAYA YA ASHURA KATIKA VYOMBO VYA MAWASILIANO VYA KIJADI NA VYA KISASA.
Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami katika makala hii maalumu inayokujieni badala ya kipindi cha Iran Juma Hili kwa mnasaba wa maombolezo ya mauaji ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya Karbala. Makala yetu ya leo itatupia jicho riwaya ya tukio la tarehe 10 Mfunguo Mosi Muharram katika vyombo vya bahari vya kijadi. Karibuni.
Tukio la Ashura, yaani tarehe 10 Mfunguo Mosi Muharram, lilikuwa tukio kubwa na adhimu lililojiri mwaka 61 Hijria (680 Miladia) katika jangwa la Karbala, nchini Iraq. Tukio hilo liliandamana na hamasa na ushujaa wa aina yake katika historia ya mwanadamu na vilevile mambo ya kutisha yaliyolifanya tukio hilo libakia hai daima katika kumbukumbu za historia. Tukio hilo la Ashura limeacha taathira kubwa katika masuala ya mtu binafsi na jamii na lilikuwa chachu ya matukio na harakati mbalimbali katika historia ya Kiislamu. Hapana shaka kwamba mchango wa matukio ya Ashura katika maisha ya Waislamu ni matokeo ya misimamo imara ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na masahaba wake waaminifu na mapambano yao dhidi ya dhulma na uovu wa serikali ya Bani Umayyah.
Hadi sasa mamia ya vitabu, makala, filamu, mashairi na kazi nyingine nyingi za kisanii zimefanyika katika kumsifu Imam Hussein na mapambano yake. Hata hivyo mvuto wa tukio na mapambano hayo bado unawateka wanadamu wengi katika pembe zote za dunia. ni mvuto huo ndio ambao bado unawakusanya pamoja mamilioni ya watu katika maeneo mbalimbali dunia katika siku hizi za Muharram ili kukumbuka tukio hilo na kuadhimisha ushujaa usiokuwa na mithili wa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).
Shughuli ya maombolezo inayofanyika kila mwaka katika mwezi huu wa Mfunguo Mosi Muharram si jambo la kawaida, la sivyo lisingekuwa na taathira kubwa kama ilivyo sasa katika maisha ya mtu binafsi na jamii za Kiislamu. Mbali na kutoa funzo la kusimama kidete mbele ya dhulma, kutetea matukufu ya dini, moyo wa hamasa na uungwana na moyo wa kujitolea kufa shahidi kwa ajili ya kutetea thamani za kidini na kibinadamu, tukio la Ashura limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii.
Nukta muhimu zaidi katika tukio hilo ni kubakia kwake hai siku zote na kuwa na taathira katika maisha ya Waislamu. Hapa linajitokeza swali kwamba, ni nini sababu ya kubakia hai tukio la Ashura la kuuawa shahidi Imam Hussein (as) na masahaba zake waaminifu? Ni kwa nini watawala madhalimu na watu waliosababisha mauaji hayo ya kutisha hawakufanikiwa kupotosha ukweli na malengo ya harakati ya Ashura au kuibadilisha kwa maslahi yao licha ya jitihada kubwa zilizofanyika katika uwanja huo? Je, vyombo vya habari na mawasiliano ya umma vya wakati huo havikuwa na taathira, au mbinu iliyotumiwa katika kufanikisha ujumbe wa Ashura na harakati ya Imam Hussein (as) ambaye Mtume amemwita kuwa ni Bwana wa Mashahidi wa Peponi, ilitofautiana na za matukio mengine?
Ili kuweza kuchambua nafasi ya vyombo vya habari katika kunukuu matukio ya siku ya Ashura na tukio la kuuawa shahidi Imam Hussein (as) tunalazimika kwanza kuchunguza mbinu za mawasiliano katika jamii ya kijadi (Traditional community).
Utamaduni wa kunukuu matukio kwa maneno na mawasilino ya uso kwa uso ni baadhi ya sifa za upashaji habari na mawasiliano ya zama za zamani ambapo utaratibu wa kuandika matukio mbalimbali haukuwa umefikia kiwango cha sasa. Mbinu za mawasiliano zilizokuwa zikipewa thamani na umuhimu mkubwa ni zile ambazo zilikuwa na uwezo wa kuwasiliana kwa njia ya moja kwa moja na wananchi. Kwa msingi huo mahudhurio ya watu katika nyumba za wageni, medani za umma, masoko na maeneo kama mikahawa havikuwa mahala pa kupitishia kipindi cha mapumziko na starehe tu, bali pia sehemu za upashaji habari, kujifunza na kubadilishana uzoefu na tajiriba. Japokuwa aina hii ya mawasiliano iliendelea kwa kipindi cha karne kadhaa, lakini imebadilika kwa kiwango kikubwa katika utendaji wa vyombo vya sasa vya mawasiliano.
Katika dunia ya Kiislamu mawasiliano ya vyombo vya habari yalikuwa na muundo makhsusi na wa aina yake ambao ulitofautiana na ule wa dini nyingine. Kwa mfano miskiti, shule za kidini na marasimu kama Swala za jamaa na Ijumaa zilikuwa na zina umuhimu mkubwa kati ya Waislamu na zilitambulia kama vyombo na nyenzo muhimu za upashaji habari na mawasiliano.
Msikiti ni moja ya matunda ya thamani kubwa ya dini ya Uislamu. Tukio la hijra na kuhama Mtume (saw) kutoka Makka na kwenda Madina lilikuwa na maana ya kuasisi kituo na makao makuu ya serikali kwa ajili ya Uislamu ili Waislamu waweze kukusanyika sehemu moja kandokando ya kiongozi wao mkuu na kujenga msingi wa awali wa jamii ya Kiislamu. Baada ya kuwasili Madina, hatua ya kwanza ya Mtume ilikuwa ni kuasisi Msikiti wa Quba na baadaye Msikiti wa Mtume ili kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu na kujenga maeneo ya ibada na masuala muhimu ya Waislamu. Ratiba na kazi za Mtukufu Mtume zilikuwa zikitangazwa katika misikiti hiyo ambako watu walikuwa wakikusanyika kwa ajili ya ibada na mambo mengine. Misikiti ilitumika kwa ajili ya mashauriano yanayohusu masuala ya jamii. Hayo yote yaliifanya misikiti kuwa nyenzo na chombo cha habari na mawasiliano. Historia inasimulia kwamba watawala na shakhsia wakubwa wa Kiislamu walikuwa wakitumia misikiti kwa ajili ya kutoa hotuba muhimu na daima walikuwa wakiwaita watu misikiti kwa ajili ya kutangaza jambo muhimu au kuwazindua kuhusu tukio fulani.
Kuhusu tukio la Ashura tunapaswa kusema kuwa misikiti imekuwa na nafasi kubwa na muhimu katika kulinda na kuhamisha ujumbe wa tukio hilo. Hotuba za viongozi wa dini katika mimbari za misikiti ambazo ziliweka wazi sura halisi ya harakati ya Imam Hussein (as) ziliifanya misikiti kuwa vituo vya kupasha habari kwa wananchi. Kwani japokuwa serikali ya kidhalimu ya Bani Umayyah ilikuwa ikikataza kuandikwa matukio halisi yaliyojiri katika ardhi ya Karbala, lakini mbinu hii ya kusimulia matukio ya Ashura kwa njia ya hotuba katika misikiti na maeneo mengine imelinda na kufikisha kwa wananchi ujumbe wa tukio hilo adhimu. XXXXX
Mtafiti wa Kiirani Dakta Nasir Bahonar anasema: Mbali na hotuba za kuzindua wananchi zilizokuwa zikitolewa na maulamaa katika misikiti, majlisi za maombolezo na vikao vya kusoma msiba kwa mbinu ya kutaja masaibu na sifa za Imam Hussein na masahaba zake kwa nathari au mashairi yaani "Rathaa" kwa lugha ya Kiarabu, ni chombo na wenzo mwingine uliolinda na kuhifadhi harakati ya Ashura kwa karne kadhaa. Japokuwa vikao vya maombolezo vina historia ndefu katika historia ya Uislamu lakini rithaa au mbinu ya kuomboleza kwa kutaja sifa na masaibu ya mtu husika kwa njia inayoshuhudiwa sasa ina umri wa karne kadhaa. Wasomaji na wasimulizi wa matukio hayo ya Ashura na harakati ya mapambano ya Imam Hussein (as) kwa nathari au mashairi huwazindua watu na kuzusha mazingira ya huzuni na simanzi katika nafsi za wasikilizaji wake. Vikao vya simulizi kama hizi vimekuwa vikifanyika kwa karne kadhaa katika misikiti, huseiniya na hata katika nyumba za watu na vimetumika kama chombo cha habari na mawasiliano ya umma cha kidini baina ya wananchi katika miji na vijiji vya baadhi ya nchi za Kiislamu kama Iran, Iraq, Saudi Arabia, Bahrain Kuwait, Lebanon na kadhalika. Vikao hivi vya simulizi za Ashura kwa njia ya mashairi au nathari huathiriwa na ada na desturi za watu wa kila eneo.
Katika ulimwengu wa Kiislamu kila taifa limekuwa likitumia mbinu na nyenzo mbalimbali kwa ajili ya kubakisha hai na kulinda matukio ya Karbala kwa ajili ya vizazi vijavyo kwa kutumia sifa makhsusi za kiutamaduni na kisanaa za kaumu na taifa husika. Kwa mfano tangu karne nyingi zilizopita Wairani wamekuwa wakitumia sanaa ya tamthilia inayojulikana kwa jina la "Taaziye" ambayo imetumiwa katika masuala ya kidini hususan katika kudhihirisha masaibu ya Imam Hussein na masahaba zake huko Karbala. Sanaa hii ya taaziye hufanyika kwa kudhihirisha baadhi ya vipengee vya mapambano ya Imam Hussein na masahaba zake katika tamthilia na kuhudhuriwa na watu wengi. Kutajwa kwa hamasa za kidini katika taaziye kumevuta idadi kubwa ya watu wa jinsia, umri na matabaka mbalimbali katika maonyesho hayo na kukifanya chombo vya mawasiliano na habari kinachowasilisha na kulinda ujumbe wa Ashura kwa ajili ya vizazi mbalimbali.
Jambo linaloonekana katika vyombo hivi vya mawasiliano vya kijadi katika jamii za Kiislamu kuhusu tukio la Karbala ni kuwa mawasiliano hayo yamekuwa na sifa makhsusi za utamaduni wa kila nchi na taifa husika. Sifa nyingine ya nyenzo na vyombo hivyo vya mawasiliano ni kwamba maulamaa wa kidini wamekuwa na mchango mkubwa zaidi ndani yake na wamekuwa na nafasi adhimu katika kulinda na kubakisha hai harakati ya mapinduzi ya Imam Hussein na masahaba zake kupitia hotuba na vikao vya maombolezo ya kidini. Vilevile inashuhudiwa kuwa wanaolengwa na vyombo hivyo ni watu wote wa jamii wanaoshiriki kwa wingi katika vikao vya maombolezo hayo kutokana na mapenzi yao makubwa kwa Mtume (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Wassalam alaykum warahmatullah Wabarakatuh.
NAFASI YA WANAWAKE KATIKA MAPAMBANO YA IMAM HUSSEIN (A.S).
Bismillahir Rahmanir Rahim
Makala hii itatupia jicho nafasi muhimu ya wanawake katika hamasa na mapambano ya Imam Hussein AS huko Karbala Iraq, katika vita baina ya haki na batili vilivyotokea mwaka 61 Hijria.
Akthari ya watu wakubwa na shakhsia ambao walikuwa na nafasi muhimu katika historia, mafaniki yao yalitokana na kujitolea kusiko na mithili kwa makundi mawili ya wanawake. Kundi la kwanza ni la akina mama wenye imani thabiti ambao walifanikiwa kuwalea watoto wao kwa huba na mapenzi makubwa na kuipatia jamii watoto kama hawa. Kundi la pili ni wake wenye kujitolea ambao walikuwa bega kwa bega na hatua kwa hatua na waume zao na kuwaliwaza na kuwapa moyo wakati waume zao walipokuwa katika mazingira magumu. Kwa muktadha huo, haiwezekani kufumbia macho nafasi ya wanawake iliyoko nyuma ya pazia ya matukio au uwepo wao wa moja kwa moja katika matukio mbalimbali. Miongoni mwa matukio ya aina yake katika historia ya Uislamu ni mapambano na harakati ya Imam Hussein AS. Moja ya makundi yaliyokuwa na nafasi muhimu katika harakati hii tukufu ni wanawake. Katika tukio hilo wanawake walionyesha kwamba, pale linapojitokeza suala la kutetea dini na kutaka kupigania haki na uadilifu, wao wanaweza kuwa bega kwa bega na wanaume na kuwa na nafasi muhimu na yenye taathira chanya na hivyo kuchangia kutengeneza historia. Mahudhurio na uwepo wa wanawake katika mapambano na harakati ya Imam Hussein kwa namna fulani kulikuwa ni kamilisho la harakati ya mtukufu huyo na wanawake hao walikuwa na nafasi ya kipekee katika vita baina ya haki na batili huko Karbala. Katika harakati na mapambano ya Imam Hussein katika siku ya Ashura, maelfu ya wapiganaji wa jeshi la batili walisimama kupambana na jeshi dogo la wafuasi wa haki. Ni jambo lililo wazi kwamba, katika mazingira kama haya watu pekee wanaoweza kusimama kidete ni wale ambao wamejipamba na daraja aali ya imani pamoja na ushujaa.
Miongoni mwa masahaba wa Imam Hussein AS kuna ambao hawakuwa na hata chembe ya shaka ya kwamba, njia ya Imam Hussein ni ya haki na hakuna kitu ambacho kingewazuia waja hao wasisimame na kutetea haki. Lakini kulikuweko na kundi jingine la watu na masahaba wa Imam Hussein ambao wao tangu awali na mwanzoni mwa njia hiyo walikuwa na shaka. Mmoja wa watu wa namna hiyo alikuweko Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Zuhair bin Qayn. Awali Zuhair hakuwa akimuunga mkono Imam Hussein AS. Lakini baadaye baada ya kutahadharishwa na kushajiishwa na mkewe yaani Deilam bint Amru, hatimaye Zuhair alijiunga na Imam Hussein. Mmoja wa marafiki wa Zuhair anasema: mwaka 60 Hijria sisi tulikwenda Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija. Kutokana na kusikia habari za safari ya Imam Hussein iliyokuwa imejaa hatari, tulikuwa tukifanya hima kujitenga na kuwa mbali na kafila na msafara wa Imam Hussein ili tusije tukakutana naye. Tulikwenda na kusimama katika nyumba moja. Imam Hussein na masahaba zake nao waliwasili hapo. Wakati tulipokuwa tumejishughulisha na kula chakula cha mchana, ghafla mjumbe wa Imam Hussein bin Ali AS alitufuata na kumwambia Zuhair, Imam anakuita. Baada ya Zuhair kusikia maneno hayo, uso wake ulitawaliwa na hali ya wasi wasi na mshangao mkubwa kiasi kwamba, alidondosha kila kilichokuwa mikononi mwake. Katika hali kama hiyo, mara sauti ya mkewe Zuhair ikasikika akisema kwamba, "Subhanallah ! mjukuu wa Bwana Mtume wa Mwenyezi Mungu anakuitaka na kisha wewe unakataa kuitikia wito wake?! Itakuwa nini kama unakwenda na kumsikiliza anachotaka kukuambia? Kwa hakika manenio ya mke wa Zuhair yalikuwa yamejaa ikhlasi na ya kutua moyoni yalileleta msukumo mkubwa katika moyo wa Zuhair kiasi kwamba, sentesi hiyo hiyo moja ya mkewe ilimfanya akakutane na Imam Hussein na kisha kuandamana naye."
Pengine Zuhair asingekuwa na mke kama huyu, asingeweza kupata fakhari zote zile za kufuatana na Imam Hussein na kisha kupata shahada ya kuuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mkewe Zuhair wakati anamuaga mumewe, alimtaka amuombee uponyo kwa Imam Hussein siku ya kiyama. Mwanamke mwingine shujaa wa Karbala ni Ummu Wahab. Akiwa pamoja na mwanawe yaani Wahab pamoja na mkwewe alikutana na kafila ya Imam Hussein katika kitongoji kimoja na kuungana nayo. Kutokana na Ummu Wahab kuvutiwa na shakhsia ya Imam Hussein alikuwa tayari kujitolea. Katika siku ya mapambano Ummu Wahab alimshajiisha mwanawe ambaye alikwenda katika uwanja wa mapambano na kupigana kishujaa mpaka akauawa shahidi. Ummu Wahab alikuwa mwanamke wa kwanza kuuawa shahidi katika vita vya Karbala na kujulikana kuwa mwanammke wa kwanza shahidi wa Karbala.
Mama wa Amr bin Junada ni mwanamkwe mwingine shujaa aliyejitolea katika vita vya Karbala hususan siku ya Ashura ambayo Imam Hussein akiwa pamoja na masahaba zake aliuawa kidhulma. Moyo wa ushujaa wa mama huyu katika siku ya Ashura hautosahaulika. Baada ya mwanawe kupigana kishujaa na kuuawa shahidi, maadui walikata kichwa chake na kumpelekea mama huyo. Mama yake Amr baada ya kukiona kichwa cha mwanawe alikichukua na kukirusha katika uwanja wa mapambano na kusema: "mimi siko tayari kuchukua kile ambacho tayari nimekitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu."
Kwa hakika maneno na muamala wa wanawake waliokuwa katika harakati ya Imam Hussein huko katika ardhi ya Karbala ni mambo ambayo mtu akiyatazama anaona ni kwa kiasi gani wanawake hawa walikuwa watiifu, waliokuwa na moyo wa subira na walijitolea na kuonyesha ushujaa wa hali ya juu wa kuvumilia taabu na masaibu. Wanawake hao licha ya kukabiliwa na masaibu na kushuhudia kwa macho yao mauaji ya kinyama kabisa yaliyofanywa na jeshi la batili la Yazid bin Muawiya, walisimama kidete na kutotetereka katika kumtetea mjukuu wa Mtume SAW Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS.
Ni nani asiyefahamu adhama na subira kubwa ya Bibi Zaynab AS binti wa Imam Ali bin Abi Talib na dada wa Imam Hussein aliyoionyesha katika harakati ya Karbala. Adhama ya bibi mwema huyo na yale yaliyonukuliwa kumhusu kuhusiana na msimamo wake thabiti katika mapambano ya Karbala ni jambo linaloonyesha adhama na kusimama kidete bibi huyu katika njia ya haki. Kwa hakika subira ya Bibi Zaynab AS katika tukio la Karbala haina mithili. Ikiwa imepita nusu siku tu tangu kaka yake, mtoto wa kaka yake na watoto wake wawili wauawe shahidi mbele ya macho yake katika uwanja wa Karbala, alisimama kando ya kiwiwili cha kaka yake yaani Imam Hussein na akiwa na moyo thabiti na irada kamili alimtaka Mwenyezi Mungu apokee udh'hiya huo wa dhuria ya Bwana Mtume SAW. Kwa hakika hii inaonyesha kwamba, Zaynab alikuwa akifikiria malengo na masuuliya makubwa zaidi. Imam Hussein AS alikuwa amewataka wanawake waliokuwa katika uwanja wa Karbala wasije wakashindwa kudhibiti hisia zao na hivyo kufanya mambo ambayo ni kinyume na haiba yao. Usiku wa kuamkia Ashura aliwaambia wanawake hao kwamba: Ewe Zaynab, Ewe Ummu Kuluthum, Ewe Fatima na Ewe Rubab, tafakarini, wakati mimi nitakapouawa, msije mkajiparura parura nyuso zenu na msije mkasema maneno ambayo hayastahiki." Wakati anawaaga pia aliwaambia: Jiandaeni kwa ajili ya balaa na tambueni kwamba, Mwenyezi Mungu muungaji mkono na mlinzi wenu, Yeye atakuokoeni na shari ya maadui. Badala ya balaa na magumu haya, atakupeni anuwai kwa anuwai ya neema kama ndio ujira wenu. Hivyo msilalamike na msitamke kitu ambacho kitapunguza thamani na daraja yenu. Kwa hakika nafasi ya wanawake ilikuwa na umuhimu wa aina yake pia baada ya Ashura katika kafila na misafara ya mateka. Kwa hakika wanawake hao wakiongozwa na Bibi Zaynab waliweza kufikisha vizuri risala ya Imam Hussein kupitia kubainisha masaibu ya Karbala. Wakiwa mjini Kufa, Zaynab bint Ali AS, Fatima na Ummu Kuluthum mabinti wa Imam Hussein kila mmoja wao alihutubia watu na kupelekea kutokea mlipuko wa sauti za vilio na majonzi. Imekuja katika historia kwamba, baada ya wanawake wa Kufa kusikia maneno hayo, walijimwangia udongo, wakajipa nyuso zao na kuomba mauti yawafike. Hivyto basi msikilizaji, tukitupia jicho tukio la Karbala tunashuhudia ni jinsi gani wanawake walivyokuwa na nafasi muhimu katika harakati hiyo. Ingawa kuna mengi ya kusema kuhusiana na nafasi ya wanawake katika tukio hilo lakini muda uliotengewa kipindi hiki hauturuhusu kufanya hivyo. Ni matarajio yangu kuwa, mmenufaika na yale niliyokuandalieni. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atufanye kuwa miongozi wa wafuasi wakweli wa Ahlul Bayt na dhuria wa Bwana Mtume SAW.