Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Jumatano alikutana na
washiriki wa Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran na kusema,
'Qur'ani Tukufu ni mhimili wa Umoja wa Umma wa Kiislamu.
Aliongeza kuwa, katika wakati huu ambao sera za madola ya kibeberu ni kuibua hitilafu na malumbano baina ya Waislamu, Umma wa Kiislamu unapaswa kuungana katika duara la neema kubwa ya Mwenyezi Mungu, yaani Qur'ani Tukufu, na kwa msingi huo kuchukua mkondo wa umoja na mashikamano.
Kitabu cha mbinguni cha Qur'ani Tukufu kimepuuzwa katika dunia ya leo. Qur'ani Tukufu si kitabu tu, bali ni muongozo wa maisha ya Waislamu. Qur'ani ni muujiza wa kudumu. Katika Qur'ani Tukufu na miongozo kuhusu majukumu ya kila Mwislamu kama vile ibada za kila siku, majukumu ya kijamii n.k.
Mtume Muhammad SAW, ni kigezo cha mwanadamu kamili kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu.
Kwa hakika Qur'ani Tukufu na Sira ya Mtume SAW ni mihimili miwili ya wafuasi wa madhehebu yote ya Kiislamu.
Lakini katika dunia ya leo, baadhi wana ufahamu potofu kuhusu mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Sunna ya Mtume SAW. Wenye ufahamu huo usio sahihi wanaibua mifarakano na kupelekea Waislamu wapigane na kuuana. Watu kama hawa wanadai kuwa wao tu ndio wanaotekelelza mafundisho ya Qur'ani na kwamba Waislamu wengine wote wasio na mitazamo sawa na yao ni makafiri wanaopaswa kuuawa.
Baadhi ya nchi zinaunga mkono makundi haya ya wakufurishaji hasa katika nchi za Syria, Iraq, Yemen, na katika baadhi ya nchi za Afrika ambapo Waislamu wanauana sambamba na kushambulia wafuasi wa dini nyinginezo katika maeneo hayo.
Maadui wa Uisamu wakiongozwa na Marekani wanatumia makundi haya ya kigaidi na wakufurishaji kuendesha vita vya niaba katika eneo.
Ayatullah Khamenei amebainisha masikitiko yake kuwa baadhi ya nchi za Kiislamu katika eneo zimefungamana na taghuti badala ya kushikamana na Mwenyezi Mungu SWT. Amesisitiza kuwa, nchi ambazo zinatekeleza sera za Marekani, kwa hakika zinaufanyia hiana Umma wa Kiislamu sambamba na kuandalia Marekani njia ya kueneza ushawishi wake muovu. Katika hotuba yake hiyo siku ya Jumatano, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema, leo jukumu muhimu zaidi la Umma wa Kiislamu hasa Ulamaa, wanafikra na wasomi katika nchi za Kiislamu, ni kuanzisha mapambano ya kuweka wazi Uislamu sahihi na kutekeleza jihadi ya kuelimisha kuhusu Uislamu sahihi.
Hii leo tunaona namna ambavyo maadui wanatumia fikra potovu za wakufurishaji na magaidi kuhusu Uislamu na kudai kuwa eti kwa msingi huo Uislamu unaunga mkono vita na misimamo mikali. Kwa kueneza fikra hizo za chuki dhidi ya Uislamu kupitia makundi ya kigaidi, madola ya kibeberu yanatumia kisingizio hicho kuzihujumu nchi za Kiislamu.
Hii ni katika hali ambayo, Uislamu sahihi unatafuatiana kikamilifu na misimamo ya magaidi wakufurishaji.
Serikali za nchi za Magharibi zinafahamu kuwa, iwapo fikra za Uislamu sahihi zitaenea katika nchi za Waislamu, basi madola hayo ya kibeberu hayataweza kueneza satwa yao katika nchi hizo.
Ujumbe wa Uislamu ni kupambana na taghuti na madola ya kibebebru. Moja ya sababu za kuhasimiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni mapambano yake endelevu dhidi ya sera za kibeberu za Marekani na waitifaki wake.
Ayatullah Khamenei amesema, imani na kuendelea kusimama kidete taifa la Iran mbele ya ubeberu wa Marekani ndicho chanzo cha nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Nguvu hizi zimejengeka katika msingi wa Uislamu na adui anauogopa 'Uislamu wenye nguvu' na 'Uislamu wa kishujaa'.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, misimamo imara na utendaji kazi wenye ikhlasi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nukta kuu zilizopelekea Iran iwe na ushawishi miongoni mwa Waislamu na hicho ni chanzo muhimu cha nguvu za mfumo wa Kiislamu. Aidha amebainisha kuwa, hadi sasa, madola ya kibeberu hayajaweza kuhadaa taifa la Iran wala vitisho vyao haviogopeshi taifa hili.