Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, ushindi wa muqawama na mapambano ya Kiislamu katika Mashariki ya Kati unaendelea.
Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo katika hotuba yake ya kuwapongeza watu wanaousaidia muqawama na kuupatia himaya na kusema kwamba, mapambano yanaendelea kuzihami nchi na mataifa na ushindi katika uwanja huu utaendelea kupatikana.
Sayyid Nasrullah amepongeza misimamo ya hivi karibuni ya Ayatulkah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kuyaunga mkono mapambano na muqawama na kubainisha kwamba, mapambano ya wananchi yakitumia nguvu zake yamekuwa yakisambaratisha mipango ya maadui.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, njama za kutoa pigo kwa muqawama zitaendelea madhali kungali kunashuhudiwa mipango katika Mashariki ya Kati ya kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Nasrullah ameashiria lengo la kushambuliwa Syria na kutoa pigo kwa mhimili wa muqawama na kuushinda na kusema bayana kwamba, Marekani na vibaraka wake katika Mashariki ya Kati wakiongozwa na Saudi Arabia wamo katika harakati za kutoa pigo kwa kambi zinazounga mkono muqawama na mapambano ya wananchi.
Kiongozi huyo wa Hizbullah amelaani uamuzi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC wa kuitaja Hizbullah kwamba, ni kundi la kigaidi na kuongeza kuwa, Saudia imekuwa mtekelezaji wa mipango dhidi ya muqawama katika Mashariki ya Kati.