Khatibu wa sala ya Ijumaa iliyoswaliwa jana mjini Tehran, Hujjatul Islam Wal Muslimin Kadhim Siddiqi, amesema kuwa, kamwe Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitoelewana na Marekani.
Ayatullah Kadhim Siddiqi ameyasema hayo katika hotuba ya sala ya Ijumaa na kuongeza kuwa, hii leo suala la kukabiliana na Marekani ni moja ya nyadhifa za kukabiliana na hila, ukiukaji, utumiaji mabavu na ugaidi. Sanjari na kulaani hatua ya Marekani ya kuzuia dola bilioni mbili mali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uvunjaji ahadi na mikataba unaofanywa na serikali ya Washington juu ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji unaoitwa kwa ufupisho wa JCPOA, Ayatullah Siddiqi amesema, Iran kwa kutumia uwezo ilionao, itafanikiwa kurejesha fedha hizo kutoka Marekani. Kadhalika Hujjatul Islam Wal Muslimin Kadhim Siddiqi sanjari na kuienzi siku ya Mwalimu, Wafanyakazi na Hilali Nyekundu amesema kuwa, kuwapa heshima walimu na wafanya kazi, ni lazima kwende sawa na hadhi yao ya kimaisha. Akisema wafanyakazi nchini Iran wameweza kufaulu mtihani mgumu, ameongeza kuwa wafanyakazi nchini hapa wamepitia vitisho na vikwazo katika kila sekta suala ambalo liliwalazimu baadhi yao kukosa hata ajira na kwamba pamoja na hali hiyo walisalia na imani, subira na moyo wa kimapinduzi. Pia amezungumzia siku ya Mab'ath ambayo ni siku aliyopewa Utume Nabii Muhammad (saw) na kuitaja siku hiyo kuwa harakati ya uokovu wa mwanadamu na kukabiliana na ujahili na kusema, kubaathiwa Mtume wa Uislamu kulikuwa ni kuhuishwa matukufu yote ya mwanandamu na kumaliza dhulma, ukatili na ukandamizaji duniani.