UN YAGUNDUA MAKABURI 50 YA UMATI NCHINI IRAQ.



Umoja wa Mataifa umesema makaburi ya umati zaidi ya 50 yamegunduliwa katika maeneo mbali mbali ya Iraq, baada ya vikosi vya serikali kuchukua udhibiti wa maeneo yaliyokuwa chini ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Jan Kubis, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq jana Ijumaa aliliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba, kuna ushahidi wa kutosha wa kuonyesha namna kundi hilo la kigaidi lilivyotekeleza jinai za kutisha katika maeneo ambayo yalikua chini ya udhibiti wao na makaburi hayo ya umati ni mojawapo ya ushahidi huo. Akitoa mfano mbele ya baraza hilo, Kubis amesema makaburi matatu ya umati yenye miili zaidi ya 80 yaligunduliwa katika uwanja wa mpira wa miguu katika mji wa Ramadi mkoani Anbar Aprili 19. Kundi la Daesh lilichukua udhibiti wa mji huo mwezi Mei mwaka jana lakini ulikombolewa mwezi Disemba.
Aidha mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama kuwa thuluthi moja ya wananchi wa Iraq, sawa na zaidi ya Wairaqi milioni 10 wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu
Katika ripoti yake ya kila mwezi Jumapili iliyopita, UN ilisema zaidi ya watu 700 wameuawa mwezi uliopita wa Aprili pekee. Takwimu hizo za Umoja wa Mataifa zimeonyesha kuwa waliouawa katika kipindi hicho ni raia 410 na maafisa usalama 331. Aidha ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa watu 1,374 wamejeruhiwa katika machafuko hayo mwezi Aprili. Maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Iraq yamekuwa yakishuhudia wimbi la mashambulizi ya kigaidi kutoka kundi la Daesh, tangu lilipoanzisha hujuma zake za kinyama mwezi Juni mwaka 2014.