MATOKEO YA JINAI ZA UTAWALA HARAMU WA ISRAEL DHIDI YA WANANCHI WA PALESTINA.


Kushadidi jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina kumeibua wasiwasi mkubwa kimataifa.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA jana Ijumaa sambamba na kutoa taarifa na kukosoa kuongezeka jinai za Israel dhidi ya Wapalestina ilisisitiza kwamba, juma lililopita wanajeshi wa Israel waliwauwa shahidi Wapalestina kadhaa katika maeneo mbalimbali ya Palestina na kuwajeruhi wengine 85.
Ripoti zinaonesha kwamba, katika kipindi cha juma moja lililopita wanajeshi wa Israel wameharibu na kubomoa makumi ya milango ya nyumba za Wapalestina. Ripoti ya Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA inatolewa katika hali ambayo, jeshi la utawala ghasibu wa Israel likitumia kisingizio cha kutafuta njia za chini kwa chini za Hamas katika Ukanda wa Gaza limefanya mashambulio makubwa katika siku nne zilizopita katika eneo hilo, ambapo shambulio lake la mzinga hapo juzi mashariki mwa Khan Yunis lilipelekea kuuawa shahidi Wapalestina kadhaa.
Matukio ya wiki iliyopita ya Palestina yanaonesha kushadidi ukandamizaji na siasa za kupenda kujitanua za utawala katili wa Israel. Hatua hizo za Israel zinabainisha kwamba, utawala huo wa Kizayuni daima umo katika kutafuta fursa ya kusukuma mbele gurudumu za siasa zake za kupenda kujitanua ukiwemo ushadidishaji wa hatua za kijeshi kwa lengo la kufuatilia malengo yake.
Kuendelea hatua za ukandamizaji na utumiaji mabavu za utawala wa kimabavu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina ni ukiukaji wa wazi wa mikataba ya kimataifa ukiwemo ule wa Geneva Uswisi. Hatua hizo za utawala wa Tel Aviv zimewafanya walimwengu kuyazingatia matukio ya Palestina na hata kuweko radiamali ya kimataifa dhidi ya utawala huo bandia.
Hii ni katika hali ambayo, ripoti za Umoja wa Mataifa katika uwanja huo hazifuatiliwi na kupewa uzito kutokana na ukwamishaji mambo wa Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi pamoja na kigugumizi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; na kwa muktadha huo hakuna wakati ripoti hizo zimefuatiliwa na kupelekea kuchukuliwa hatua za maana.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba, hatua hizi za kusitasita na kigugumizi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kuichukulia hatua Israel ni jambo lililoupa kiburi utawala ghasibu cha kuendelea mbele na jinai zake dhidi ya Wapalestina bila ya kuwa na woga wala hofu. Licha ya kuwa kushtadi jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel kumepelekea hali ya Wapalestina kuwa mbaya mno, lakini jambo hilo halijawafanya Wapalestina hao wasalimu amri mbele ya siasa za kupenda kujitanua za maghasibu Wazayuni. Wananchi wa Palestina wakitegemea muqawama na mapambano dhidi ya Uzayuni sanjari na kusimama kidete mbele ya Israel, wameukwamisha utawala huo katika kufikia malengo yake na huu ni ukweli ambao hata viongozi wa Tel Aviv wenyewe wameukiri dhahir shahir.
Si tu kwamba, hujuma na mashambulio hayo ya Israel hayajaweza kuifanya ifikie malengo yake bali jambo hilo limeongeza nukta nyingine katika faharasa ya kushindwa utawala huo ghasibu.
Matatizo ya Israel ya kushindwa kukabiliana na Wapalestina hayaishii hapo tu kwani kushindwa huko kumeufanya utawala huo uchanganyikiwe na hivyo kupelekea kuongezeka matatizo ya ndani ya utawala huo ghasibu.
Hapana shaka kuwa, duru mpya ya mashambulio na hujuma za Israel lengo lake ni kujaribu kufunika kushindwa kwake na wakati huo huo kuzipotosha fikra za waliowengi kuhusiana na wimbi la mivutano ndani ya utawala huo.
Hata hivyo matukio ya Palestina yanaweka wazi nukta hii kwamba, chokochoko mpya za Isreal hjazijawa na natija nyingine bighairi ya kuutumbukiza zaidi utawala huo katika kinamasi ilichokwama ndani yake.