Rais
Hassan Rouhani wa Iran amelaani hatua ya Saudia kuwazuia Wairani kutekeleza
ibada ya Hija mwaka huu na kusema hatua hiyo ni kwa maslahi ya utawala wa
Kizayuni wa Israel.
Ameongeza kuwa wale wanaodai kuwa eti ni wahudumu wa Misikiti Miwili Mitakatifu wanatekeleza hatua ya kitoto ya kuzuia Njia ya Mwenyezi Mungu na Hijja huku wakieneza machafuko katika eneo, na yote hayo ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Siku ya Jumapili Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran alisema njama na vizingiti vya Saudia ni jambo ambalo limewazuia Wairani kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.
Naye Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara za Kidini la Iran Saeed Ohadi amebainisha sababu ambazo zimepelekea Mahujaji Wairani washindwe kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu. Amebaini kuwa Wasaudi wamepiga marufuku kuwekwa bendera ya Iran katika majengo ya Mahujaji Wairani. Aidha wameweka vizingiti kuhusu idadi ya zahanati za Iran katika msimu wa Hija sambamba na kuzuia madawa yanayotumiwa na Mahujaji Wairani. Aidha amesema Wasaudi wamekataa ushanga wa mkononi wa kielektroniki ambao Iran ilikuwa imetengeneza kwa ajili ya kuwatambulisha Mahujaji wake huku wakisema watatengeneza ushanga ambao watawalazimisha Wairani kuuvaa. Ohadi amesema Wasaudi pia wamepiga marufuku baadhi ya hafla za Mahujaji Wairani jambo ambalo Iran haikulikubali. Afisa huyo wa Hija wa Iran pia amesema Saudi Arabia inawadhalilisha Wairani kisiasa na hata wakati wa mazungumzo kuhusu Hija Wasaudi walionyesha muamala mbovu sana. Mkuu wa Shirika la Hija la Iran pia amesema maafisa wa Saudia kwa kawaida huvunjia heshima nakala za Qur’ani zilizochapishwa nchini Iran na kuwapokonya Mahujaji Wairani nakala hizo za Qur’ani huku wakizirusha huku na kule kwa madharau.