KAMISHNA MKUU WA HAKI ZA BINADAMU KATIKA UMOJA WA MATAIFA AMESEMA SAUDIA NA WAITIFAKI WAKE WANADONDOSHA MABOMU KATIKA SHULE, MAHOSPITALI NA VITUO VYA AFYA NCHINI YEMEN.

Zeid Raad al-Hussein, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa katika ripoti yake siku ya Ijumaa ameongeza kuwa: "Katika hujuma za muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen tokea Machi 2015, katika hujuma kwa maeneo yasiyo ya kijeshi raia wapatao 3,218 wameuawa. Aidha amesema watu wengine 5,778 wamejeruhiwa katika hujuma hizo. Maafisa wa Yemen wanasema watu 8,500 wameuawa katika hujuma za mwaka moja wa Saudia dhidi ya nchi hiyo.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameaalni vikali hatua ya hivi karibuni ya jeshi la Saudia kuhujumu soko moja katika mkoa wa Hajja nchini Yemen ambapo watu 106 waliuawa wakiwemo watoto 24.
Jana makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen waliandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a kulaani siasa za kichokozi na kivamizi za utawala wa Aal Saud.
Katika maandamano hayo wananchi wa Yemen mbali na kulaani utawala wa Aal Saud na Marekani wamelaani mashambulio ya anga yaliyofanywa dhidi ya soko mkoani Hajja.
Tangu mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa Saudi Arabia imeiwekea mzingiro wa angani na baharini Yemen na kuzuia misaada ya kibinadamu isiwafikie wananchi wa nchi hiyo, lengo likiwa ni kuindoa madarakani harakati ya wananchi ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake Abd Rabbuh Mansour Hadi.
Mashambulio ya Saudia dhidi ya Yemen yameangamiza na kusababisha hasara kubwa pia kwa miundombinu ya Yemen, mbali na kulenga na kubomoa hospitali, shule, nyumba za raia na misikiti nchini humo.