Umoja wa Ulaya umejiunga na Umoja wa Mataifa katika kulaani hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kupora ardhi zaidi za Wapalestina.
Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa, hatua ya Israel ya kupora mamia ya hektari za ardhi zaidi za Palestina katika Ukingo wa Magharibi imechukuliwa kwa lengo la kuzuia kuundwa kwa nchi ya Palestina katika siku zijazo. Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya, Bi Federica Mogherini, ametangaza kuwa uamuzi wa Israel wa kujenga na kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Ukingo wa Magharibi ni kinyume na sheria za kimataifa. Taarifa ya Mogherini imeongeza kuwa, utendaji wa serikali ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ni kizuizi katika kutafuta njia ya utatuzi wa amani wa mgogoro wa Palestina. Amesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unapinga vikali siasa za Israel za kujenga vitongoni vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya ujenzi na upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina umeshadidi zaidi baada ya redio ya jeshi la Israel kutangaza Jumanne iliyopita kwamba, serikali ya Benjamin Netanyahu imetwaa sehemu kubwa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi karibu na Bahari Maiti (Dead Sea) na mji wa Jericho (Ariha) kwa ajili ya ujenzi wa vitongiji vipya vya Wayahudi.
Harakati ya mrengo wa kushoto huko Israel ya Peace Now inayopinga sera za serikali ya Netanyahu za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina imetangaza kuwa, hiyo ni operesheni kubwa zaidi ya kutwaliwa ardhi za Palestina katika kipindi cha miaka kiwili iliyopita.
Mazungumzo ya Wapalestina na Israel yalisimama baada ya utawala huo wa Kizayuni kukataa kusitisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina, mpango wa kuasisiwa nchi mbili kwa mujibu wa mipaka ya mwaka 1967 na kuachiwa huru maelfu ya Wapalestina wanaoshikiliwa katika korokoro za kutisha za Israel. Mazungumzo hayo yalianza mwaka 1991 chini ya upatanishi wa Marekani kwa lengo la kuhitimisha mgogoro wa siku nyingi kati ya Waarabu na Israel katika eneo la Mashariki ya Kati na kutatua kadhia ya Palestina. Hata hivyo yalififia katika muongo wake wa kwanza na kusimama kikamilifu mwaka 2009 baada ya serikali yenye misimamo mikali ya Benjamini Netanyahu kushika hatamu za uongozi huko Israel. Wakati huo Marekani iliwashawishi Wapalestina kuketi kwenye meza ya mazungumzo na Israel ili eti kufikia mapatano ya kuundwa dola huru la Palestina kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Makundi ya mrengo wa kulia ya Israel daima yamekuwa yakipinga suala la kuundwa nchi huru ya Palestina na kwa msingi huo yanapinga mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati. Wakati huo huo makundi ya mrengo wa kushoto yanakubali kimsingi suala la kuundwa nchi huru ya Palestina lakini ndani ya shirikisho la Jordan na Palestina au kupewa mamlaka ya utawala wa ndani chini ya usimamizi wa Israel.
Ni wazi kuwa, ili kuweza kuunda nchi huru ya Palestina ni lazima kwanza liwekwe wazi suala la hali ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizoporwa za Palestina na vilevile kuondolewa jeshi la Israel katika maeneo ya Quds tukufu na Ukingo wa Magharibi. Vilevile mzingiro wa eneo la Ukanda wa Ghaza unapaswa kukomeshwa na kuwekwa wazi njia ya mawasiliano kati ya eneo hilo la lile la Ukingo wa Magharibi.
Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na kuwekwa humo wahamiaji wa Kiyahudi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia vimezuia suala la kuundwa nchi huru ya Palestina kwa kipindi cha miaka 50 sasa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu imedumisha ujenzi wa vitongoji hivyo kwa kasi kubwa licha ya upinzani wa jamii ya kimataifa ili kwa upande mmoja kutatiza uwezekano wa kuvunjwa vitongoji hivyo katika siku za usoni, na katika upande mwingine iweze kuzuia kuundwa nchi huru ya Palestina.
Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana jamii ya kimataifa hata baadhi ya waitifaki wa Israel, imekuwa ikipinga vikali na kulaani sera hizo za Israel na kutoa wito wa kukomeshwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.