Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amempongeza Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa kuchaguliwa tena hivi karibuni kuiongoza nchi hiyo.
Katika ujumbe wake huo, Rais Rouhani
amemtumia salamu za kheri na fanaka Museveni kufuatia kuchagiliwa tena.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
amesema ana matumaini kuwa, uhusiano wa Iran na Uganda utazidi kuimarika katika
siku za usoni.
Tume ya Uchaguzi ya Uganda mwezi
uliopita ilimtangaza Yoweri Museveni kuwa Rais Mpya wa nchi hiyo baada ya
kushinda zaidi ya asilimia 60 ya kura na hivyo kumshinda mpinzani wake mkuu
Dakta Kiiza Besigye katika uchaguzi wa Februari 18.
Museveni ambaye tangu miaka 30
iliyopita hadi sasa anatawala Uganda, ni kati ya Marais wa Afrika ambao
wamezifanyia marekebisho katiba za nchi zao kwa kufuta kipengee kinachohusiana
na ukomo wa mihula miwili ya kuwepo madarakani rais wa nchi; na hivyo
kujiandalia njia ya kusalia madarakani.
Rais Museveni amesisitiza mara kwa
mara kuwa demokrasia ya Afrika isilinganishwe na ya nchi za Magharibi.
HIZBULLAH YALAANI 'HUJUMA' YA JUMUIYA YA NCHI ZA KIARABU.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, imelaani hatua ya
hivi karibuni ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuitaja harakati hiyo kuwa
"kundi la kigaidi" na kusema uamuzi huo ni sawa na "tangazo la
hujuma" kutoka Saudi Arabia.Katika taarifa, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Naim Qassim amesema utawala wa Saudia unatumia kila mbinu kuhakikisha kuwa Hizbullah inatajwa kuwa kundi la kigaidi. Akizungumza mjini Baalbek Lebanon, amesema Saudia imewashinikiza mawaziri wa nje wa nchi za Kiarabu kuchukua maamuzi dhidi ya Hizbullah.
Amesema Saudia inapinga Hizbullah kwa sababu harakati hiyo imeweza kutoa pigo kwa utawala haramu wa Israel sambamba na kutetea Umoja wa Kiislamu na kuwaunga mkono watu wa Yemen, Syria na Iraq ambao wanapata masaibu kutokana na udhalimu wa Saudia.
Ikumbukwe kuwa siku ya Ijumaa, nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiarabu zilitangaza katika kikao chao cha Cairo kuwa eti Hizbullah ni kundi la kigaidi. Uamuzi huo ulipingwa vikali na Algeria, Lebanon na Iraq. Uamuzi huo umekuja wiki moja baada ya Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kutangaza kuwa eti Hizbullah ni kundi la kigaidi.
Tayari nchi muhimu za Kiarabu kama vile Iraq, Algeria, Lebanon na Syria zimetoa taarifa na kupinga uamuzi huo dhidi ya Hizbullah. Chanzo cha habari (irib)