WAIRANI WAANDAMANA KULAANI JINAI ZA SAUDIA YEMEN.

Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran wameandamana kote nchini baada ya Sala ya Ijumaa kulaani jinai za utawala wa Saudia dhidi ya watu wa Yemen. Wananchi katika miji mikubwa kama vile Tehran, Qom, Mashhad na miji mingine 770 kote nchini wameandamana kupinga mauaji ya umati ya Waislamu wasio na ulinzi wala hatia wa Yemen ambao wamepoteza maisha katika hujuma zinazoongozwa na utawala dhalimu wa Saudi Arabia. Aidha waandamanaji hao wametaka jinai hizo za Saudia zisitishwe mara moja. Huku wakitoa nara kama vile 'Mauti kwa Marekani', 'Mauti kwa Aal Saud' na 'Mauti kwa Utawala wa Kizayuni' waandamanaji wametangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wasio na hatia Yemen. Baada ya maandamano hayo kumesomwa taarifa ya kulaani hujuma ya Saudia Yemen na njama za Marekani za kuhakikisha utawala wa Kizayuni unabakia katika eneo. Taarifa hiyo imesema Riyadh, mji mkuu wa Saudia sasa ni mji mkuu wa ugaidi. Halikadhalika wamelaani mpango wa pamoja wa Saudi Arabia na Wazayuni katika kuizingira Yemen na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingizwa nchini humo. Wakati huo huo Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Hilali Nyekundu ya Iran ameashiria hatua ya Saudia kuzuia misaada ya kibinaadmau kutoka Iran isiwafikie wanaohitajia nchini Yemen. Hujatul Islam wal Muslimin Muizz amesema kuwa, meli ya misaada ya kibinadamu kutoka Iran kesho itaelekea Yemen.

WAYEMEN WAANDAMANA KULAANI HUJUMA ZA SAUDIA.
Maelfu ya Wayemeni wamejitokeza kwa wingi katika mitaa ya mji mkuu Sana'a kulaani hujuma ya kinyama ya Saudia dhidi ya nchi hiyo.
Waandamanaji hao waliokuwa na hasira wametaka Saudi Arabia isitishe mara moja hujuma inayotekelezwa na ndege zake za kivita nchini humo. Huku wakitoa nara dhidi ya utawala wa kifalme wa Saudia, Wayemeni wamepinga vikali uingiliaji wa Saudia katika mambo ya ndani ya nchi hiyo. Halikadhalika washiriki wa maandamano hayo wametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuishinikiza Saudia ikomeshe jinai zake.
Ikumbukwe kuwa Saudia ilianzisha hujuma dhidi ya Yemen mnamo Machi 26 bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa. Lengo la hujuma hiyo ni kuiangusha harakati ya Ansarullah iliyoko madarakani na kumrejesha rais wa zamani wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansur Hadi ambaye ni kibaraka wa Saudia. Aghalabu ya waliopoteza maisha katika hujuma ya Saudia nchini Yemen ni raia wasio na ulinzi wakiwemo wanawake na watoto. Aidha Saudia imetumia silaha zilizopigwa marufuku kama vile mabomu ya vishada katika hujuma dhidi ya maeneo ya raia nchini Yemen.

AYATULLAH KHATAMI ALAANI JINAI ZA SAUDIA NCHINI YEMEN.
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa Tehran amelaani vikali jinai na unyama wa Saudi Arabia nchini Yemen.
Akihutubia halaiki kubwa ya waumini katika Chuo Kikuu cha Tehran, Ayatullah Seyyed Ahmad Khatami ameashiria hujuma inayoongozwa na Saudia huko Yemen na kusema wananchi wa Yemen wana haki ya kuamua mustakabali wao na kwamba wanapinga uingiliaji wa Marekani katika mambo ya ndani ya nchi yao. Ameongeza kuwa harakati ya Ansarullah nchini Yemen inapinga satwa ya mabeberu nchini humo na kwamba hatimaye Wayemeni wataibuka washindi katika mpambano yao dhidi ya njama za mabeberu. Aidha amelaani vikali mauaji ya raia wasiopungua 3,000 wa Yemen ambao wamepoteza maisha yao katika hujuma ya ndege za Kimarekani za Saudia na kusema jinai hizo ni sawa na za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina. Ayatullah Khatami amelikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kuhalalisha kwake jinai za madhalimu badala ya kuwaunga mkono Wayemen wanaodhulumiwa. Huku akiashiria uingiliaji wa Marekani katika maeneo mbali mbali duniani na uungaji mkono wa Washington kwa mauaji ya raia huko Yemen na Syria, Ayatullah Khatami amelaani sera za kivita za Marekani kote duniani na kuongeza kuwa Marekani inawadhulumu hata raia. Katika sehemu nyengine ya hotuba yake, Ayatullah Khatami ameashiria vitisho vya viongozi rasmi wa Marekani dhidi ya Iran na tamko lao kwamba chaguo la kijeshi lingalipo mezani. Akijibu vitisho hivyo, ameonya kuwa nchi yoyote itakayothubutu kuishambulia kijeshi Iran itajuta milele.