KUNA UWEZEKANO SAUDIA IKAMNYONGA SHEIKH NIMR AL BAQR.

Mkuu wa mtandao wa habari uliopewa jina la Sheikh Nimr Baqir an-Nimr, ambaye ni kiongozi wa kidini wa Waislamu wa Kishia nchini Saudia na ambaye anaendelea kushikiliwa katika korokoro za utawala wa nchi hiyo, ameonya juu ya kuwepo njama za kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya sheikh huyo. Sayyid Muhammad Musawi, ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la Mehr na kuuonya utawala wa Aal Saud juu ya kutekeleza hukumu hiyo ya kifo dhidi ya Sheikh huyo mwanaharakati, amesema kuwa kuuawa Sheikh Nimr kutautikisa utawala wa ukoo wa Aal Saud. Aidha amekosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa na nchi za Kiarabu kuhusiana na hukumu ya adhabu ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr Baqi an-Nimr, na kusema kuwa, mienendo hiyo inaonyesha wazi undumiakuwili wa Wamagharibi na asasi za haki za binaadamu duniani. Amesisitiza kuwa, bila shaka yoyote, kutekelezwa hukumu ya kifo dhidi ya sheikh huyo, kutaibua wimbi jipya la mapinduzi nchini Saudia na hata Bahrain. Juzi chanzo kimoja cha habari kilichoko karibu na Sheikh Nimr kilifichua kwamba, viongozi wa Aal Saud walikuwa wamepanga kutekeleza hukumu hiyo ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr tarehe 14 ya mwezi huu sawa na tarehe 25 Rajab. Askari wa utawala wa kidikteta wa Saudia, walimtia mbaroni Sheikh Nimr, mwezi Julai mwaka 2012 baada ya kumjeruhi kwa kumpiga risasi kadhaa akiwa ndani ya gari yake.