SISITIZO LA HAMAS LA KUFUATILIA MARIDHIANO YA KITAIFA PALESTINA.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, kutekelezwa makubaliano ya maridhiano ya kitaifa baina ya makundi ya Kipalestina ndio njia bora kabisa kwa ajili ya kufikiwa malengo matukufu ya wananchi madhulumu wa Palestina. Mussa Abu Marzook mjumbe mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameashiria kukiri viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani juu ya kugonga mwamba mazungumzo ya mapatano na kusema kuwa, katika mazingira kama haya, njia bora zaidi ya kujikwamua na hali iliyopo hivi sasa ni kutekelezwa makubaliano ya maridhiano ya kitaifa baina ya makundi ya Kipalestina na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kutoa ushirikiano unaohitajika katika uwanja huo. Duru ya mwisho ya mazungumzo eti ya mapatano yenye lengo la kutafuta njia za kuunda serikali mbili ambayo ilianza Julai mwaka 2013 kwa upatanishi wa Marekani, ilifikia tamati Aprili mwaka jana bila ya natija kutokana na ukwamishaji mambo wenye kuendelea wa utawala wa Kizayuni wa Israel hususan hatua yake ya kuendeleza ujenzi wa vitongojhi vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina. Mussa Abu Marzook amesema kuwa, kufuatilia makubaliano ya maridhiano ya kitaifa baina ya makundi ya Kipalestina na kutatuliwa hitilafu zinazohusiana na masuala kama kufanyika vikao vya Bunge sambamba na kufanyika uchaguzi wa Rais na Bunge, Wapalestina hawatahitajia himaya wala msaada wa Wazayuni au Wamarekani. Sisitizo la Hamas juu ya kutokuwa na matunda wala natija yoyote mazungumzo ya aina yoyote ile na adui Mzayuni na wakati huo huo kusisitiza Hamas juu ya kufuatiliwa makubaliano ya maridhiano ya kitaifa baina ya makundi ya Kipalestina kunafanyika katika hali ambayo, katika majuma ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni umezuia kipato cha kila mwezi cha dola milioni 130 za Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa kisingizio cha kujiunga mamlaka hiyo na asasi za kimataifa, jambo ambalo limeifanya hali ya Palestina kuwa mbaya zaidi. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika siku za hivi karibuni maafisa wa makundi ya mapambano ya Palestina ikiwemo Hamas na Jihadul Islami, mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza juu ya kufuatiliwa makubaliano ya maridhiano ya kitaifa na kuitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina kujiunga na mwenendo huo. Kabla ya hapo, Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Juni Pili mwaka jana alitangaza kuunda serikali ya maafikiano ya kitaifa kwa mujibu wa makubaliano ya maridhiano ya kitaifa yaliyokuwa yamefikiwa Aprili 23 hiyo mwaka jana baina ya harakati za mapambano za Fat'h na Hamas. Kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa Palestina kulifikiwa katika hali ambayo, harakati za Hamas na Fat'h katika miaka ya hivi karibuni zilitiliana saini makubaliano kadhaa ya maridhiano ya kitaifa, lakini kutokana na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel hakuna wakati ambao zilifanikiwa kuyatekeleza kivitendo makubaliano hayo. Hamas na makundi kama Jihadul Islami yanaamini kuwa, katika mazingira ya hivi sasa tadbiri na utendaji bora kabisa wa kukabiliana na mikakati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na njama za waungaji mkono wake yaani madola ya Magharibi hususan Marekani, ni kuweko mshikamano na mfungamano zaidi baina ya Wapalestina hususan kutekelezwa kivitendo makubaliano kamili ya makubaliano ya maridhiano ya kitaifa.

 WAPALESTINA WAANDAMANA KUIUNGA MKONO HAMAS.
Hukumu iliyotolewa na mahakama moja ya Misri ya kuitaja Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kuwa ni kundi la kigaidi imezua hasira na radiamali kali ndani na nje ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Maandamano makubwa yamefanyika katika Ukanda wa Gaza kulalamikia uamuzi huo wa mahakama ya Misri ambapo waandamanaji wamebeba mabango yenye jumbe za kulaani serikali ya Cairo.
Mustafa Barghouti, mwanasiasa mwandamizi wa Palestina amesema hatua hiyo ya Misri ni ya kisiasa na yenye lengo la kuvuruga umoja wa Wapalestina kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel. Naye msemaji wa Hamas, Sami Abu Zuhri ameitaja hukumu hiyo ya mahakama ya Misri kuwa hatari na yenye lengo la kudhoofisha mapambano ya Wapalestina dhidi ya Wazayuni maghasibu. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/…/47016-wapalestina-waandamana-kui…