HELIKOPTA ZA ISRAEL ZAUA WANACHAMA SITA (6) WA HIZBULLAH:

Wanachama wasiopungua sita wa Harakati ya Muqawama wa Hizbullah nchini Lebanon wameuawa, baada ya helikopta ya utawala wa Israel kushambulia kwa makombora maeneo ya milima ya Golan ndani ya ardhi ya Syria. Taarifa zinasema kuwa, shambulio hilo la makombora mawili lilifanyika katika eneo la mashamba ya Amal yaliyoko katika eneo la kiistratijia la Quneitra lililoko umbali wa kilomita 60 kusini mwa Damascus, mji mkuu wa Syria. Harakati ya Hizbullah imethibitisha kuuawa wanachama wake sita kwenye shambulio hilo, akiwemo Abu Issa mmoja wa makamanda na mtaalamu wa operesheni za vita wa Hizbullah na Jihad Mughniya mtoto wa shahidi Emad Mughniya Kamanda wa zamani wa Hizbullah. Taarifa ya Hizbullah imeeleza kuwa, shambulio hilo limefanyika wakati wanachama hao walipokwenda kukagua eneo la mashamba ya Amal. Duru za habari zinasema kuwa, gari iliyowabeba wanachama hao wa Hizbullah imeteketezwa kabisa, na nyingine kuharibiwa vibaya. Ndege za Israel zimekuwa zikishambulia mara kwa mara maeneo ya Syria tokea zilipoanza ghasia na machafuko nchini humo yapata miaka minne iliyopita. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, hadi sasa watu wasiopungua laki mbili wameshauawa kwenye vita vya ndani nchini Syria.

IRAN YAALANI MAUAJI YA WANACHAMA WA HIZBULLAH:
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali mauaji ya wanachama sita wa Harakati ya Mapambano ya Lebanon Hizbullah yaliyofanywa na utawala haramu wa Kizayuni. Akizungumza na televisheni ya Press mapema leo, Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Tehran inalaani vikali vitendo vyote vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni wa Israel vikiwemo vile vinavyotekelezwa na utawala huo dhidi ya watu wa Lebanon na Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya nchi hiyo. Zarif amesema sera ya ugaidi wa kiserikali ni sera inayofahamika ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Harakati ya Mapambano ya Lebanon Hizbullah imethibitisha kuuliwa wapiganaji wake sita katika shambulio jipya la anga lililofanywa na Israel katika mji wa kistratejia wa Quneira kusini magharibi mwa Syria. Hizbullah imewataja wanachama wake waliouliwa jana na Israel kuwa ni Jihad Mughniya mwana wa kiume wa Imad Mughniya kamanda wa ngazi ya juu wa harakati hiyo aliyeuliwa kigaidi na Israel na wapiganaji wengine watano waliotajwa kwa majina ya Mohammad Issa aliyekuwa na miaka 42, Abbas Ibrahim Hijazi miaka 35, Mohammad Ali Hasan Abu al Hassan miaka 29, Ghazi Ali Dawi miaka 26 na Ali Hasan Ibrahim miaka 21. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/…/46022-iran-yaalani-mauaji-ya-wan…