Ayatullahil Udhma Sheikh Nasser Makarim Shirazi Marja'a Taqlid wa Waislamu wa Madhehebu ya Kishia amesema kuwa, katika zama hizi umoja na mshikamano kati ya Waislamu una umuhimu mkubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu. Akizungumza na Sheikh Ahmad al Zein Mkuu wa Jumuiya ya Maulamaa wa Kiislamu wa Lebanon mjini Qum, kusini mwa Tehran Ayatullah Makarim Shirazi ameeleza kwamba, mambo yanayowakurubisha Waislamu ni mengi na kusisitiza kwamba leo hii ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuwa macho katika kukabiliana na njama za maadui. Kwenye mazungumzo hayo, Sheikh Ahmad al Zein ameelezea jinsi jumuiya hiyo ilivyoundwa yapata miongo mitatu iliyopita kutokana na taathira za harakati ya Imam Khomeini MA, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon na kusisitiza kwamba, kuamini mfumo wa utawala wa fakihi, kuzipa nguvu harakati za muqawama wa wanamapambano wa Palestina, kusambaza fikra na utamaduni wa umoja na mshikamano wa Waislamu kati ya Mashia na Masuni ni miongoni mwa malengo makuu ya kuundwa jumuiya hiyo. Jumuiya ya Maulamaa wa Kiislamu nchini Lebanon inayoundwa na wasomi na maulamaa 250 wa Kishia na Kisuni, iliundwa yapata miaka 35 iliyopita kutokana na ubunifu wa Imam Khomeini MA. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/habari/iran/item/45837-ayatullah-makarim-shirazi-umoja-unahitajika-baina-ya-waislamu