MAMILIONI WAELEKEA KARBALA KWA AJILI YA ARUBAINI.

Wakati siku ya maombelezo ya Arubaini ya Imam Hussein (A.S) ikiendelea kukaribia, mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaelekea katika mji mtukufu wa Karbala huko Iraq kwa ajili ya kushiriki kwenye shughuli hiyo. Wafanyaziara kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi za nje wanaelekea huko Karbala, huku baadhi yao wakitembea kwa miguu kutoka miji mbalimbali na mipakani mwa nchi hiyo. Polisi ya Iraq imechukua hatua muhimu za kuimarisha usalama unaowajumuisha maelfu ya askari kwa madhumuni ya kulinda usalama nchini humo na hasa katika mji mtakatifu wa Karbala.
Maafisa wa Iraq wanasema kuwa, licha ya kuwepo vitisho vya magaidi, idadi ya watu wanaoelekea Karbala kwa ajili ya kushiriki maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein (A.S) inaongezeka. Mji wa Karbala unatarajiwa kuwa mwenyeji wa wafanyaziara karibu milioni 17 wakati wa maombelezo ya Arubaini ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (A.S), yatakayofanyika siku ya Jumamosi.
Maombolezo ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala mnamo mwaka 61 Hijria. Mjukuu huyo wa Mtume na masahaba wake walipigana na jeshi la mtawala dhalimu Yazid bin Muawiya uliokuwa umepotosha dini na mafundisho yake na wakauwa shahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/…/45027-mamilioni-waelekea-karbala…