'NJAMA ZA WAMAGHARIBI DHIDI YA IRAN ZIMEFELI'
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil-Udhmaa Sayyid
Ali Khamenei, amesema kuwa njama za Marekani na nchi za kikoloni za
kujaribu kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na
kadhia ya nyuklia zimefeli. Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo alipokutana
na maulama, wanazuoni, wanafikra na wageni walioshiriki katika
kongamano la kimataifa kuhusu ‘Tishio la
Makundi ya Kitakfiri na yenye Misimamo ya Kufurutu Mipaka kwa Mtazamo
wa Maulama wa Kiislamu’ kongamano lililofanyika mjini Qom nchini hapa
ambapo sambamba na kuashiria mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi
la 5+1 amesema kuwa, licha ya Marekani na wakoloni wa Ulaya kuungana
katika njama za kulishinikiza taifa hili liwapigie magoti kuhusu kadhia
ya nyuklia, lakini wameshindwa na hawatofanikiwa. Akizungumzia ongezeko
la makundi ya kufurutu mipaka katika miaka ya hivi karibuni yaliyoundwa
na madola ya kibeberu kwa ajili ya kupambana na Uislamu, Kiongozi
Muadhamu amesema kuwa vitendo vya makundi hayo machafu ya kitakfiri,
vinafanyika kupitia mipango maalumu ya madola hayo ukiwemo utawala
haramu wa Kizayuni, lengo kuu likiwa ni kuwasahaulisha Waislamu na
walimwengu kwa ujumla kadhia ya Palestina na msikiti wa al-Aqsa.
Amefafanua kuwa, kuanzishwa mwamko wa kielimu, kimantiki na kueneza
elimu na umoja kwa ajili ya kung’oa mizizi ya harakati hizo za
kitakfiri, kuweka wazi njama za kisiasa za madola ya kibeberu katika
kuanzisha makundi hayo ya kitakfiri na kigaidi na kuzidisha uzingatiaji
wa umma wa Kiislamu katika masuala yao muhimu hasa kadhia ya Palestina,
ni miongoni mwa wadhifa muhimu wa maulama katika ulimwengu wa Kiislamu,
hii leo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil-Udhmaa
Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, kupotosha mwamko wa Kiislamu, kuharibu
miundombinu muhimu katika nchi za Kiislamu na kuchafua sura ya Uislamu
kupitia makundi ya kigaidi na kitakfiri, ni miongoni mwa malengo ya
Marekani na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba,
hatua ya madola hayo ya kutumia makundi ya kitakfiri nchini Iraq na
Syria ni kutaka kupotosha mapambano dhidi ya utawala ghasimu wa Israel
unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Akiashiria hatua za mara kwa
mara za ndege za Marekani kuwarushia silaha za kivita wapiganaji wa
kundi la kitakfiri la Daesh waliozingirwa kila upande amesisitiza kuwa,
Marekani inadai kuunda muungano wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na
kundi hilo la Daesh, katika hali ambayo ni huo uongo mtupu kwani lengo
la muungano huo ni kuhakikisha kuwa mapigano kati ya Waislamu wenyewe
kwa wenyewe havimaliziki. Hata hviyo amesema, maadui hao watashindwa tu
katika njama zao hizo. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/habari/kiongozi/item/44727-njama-za-wamagharibi-dhidi-ya-iran-zimefeli