Mamia ya Waislamu jana walifanya maandamano
makubwa mkabala wa Ubalozi wa Saudi Arabia mjini London, Uingereza
wakipinga adhabu ya kifo iliyotolewa na vyombo vya sheria vya nchi hiyo
dhidi ya Sheikh Nimr Baqer al Nimr mwanachuoni mashuhuri wa
nchini Saudi Arabia. Waandamanaji hao walipiga nara za 'Mauti kwa
utawala wa Aal Saud' na ' Sheikh Nimr aachiliwe huru' sanjari na kubeba
mabango na maberamu yaliyo dhidi ya utawala wa kifalme wa Saudi
Arabia, walisisitiza juu ya kuachiliwa huru mwanachuoni huyo.
Waandamanji hao sanjari na kuutaja utawala wa Saudi Arabia kuwa
mvunjaji mkuu wa haki za binadamu na unayaunga mkono makundi ya
kigaidi, wameitaka serikali ya Riyadh kumuachilia huru Sheikh Nimr Baqer
al Nimr. Kijana mmoja wa Kimarekani aliyeshiriki kwenye maandamano hayo
amelalamikia jinsi nchi zinazojinadi kuwa watetezi wa haki za
binadamu kama vile Marekani na Uingereza kwa kunyamazia kimya hukumu
hiyo ya kidhuluma na kusisitiza kwamba kimya hicho kinaonyesha wazi
kuwepo mashirikiano kati ya madola hayo ya Magharibi kwa utawala huo wa
kifalme katika kutenda jinai na kuwakandamiza wananchi wa Saudia. Kijana
huyo amesema na hapa tunamnukuu: ' Mimi siyo Muislamu na wala Mwarabu,
lakini naamini kwamba Sheikh Nimr ni kiongozi huru ambaye amedhulumiwa
na utawala katili na wa kifalme wa Saudi Arabia', mwisho wa kunukuu.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, nchi na mashirika mbalimbali ya kutetea haki
za binadamu yamelaani vikali hukumu hiyo ya kidhuluma iliyotolewa dhidi
ya mwanachuoni huyo. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/habari/habari/item/43858-waandamana-kupinga-hukumu-ya-kifo-dhidi-ya-sheikh-nimr