Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, njia pekee ya kuweza kusimama imara kukabiliana na kambi ya kibeberu iliyo dhidi ya ubinadamu ni kuendeleza fikra ya "kupambana" na kambi hiyo.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo wakati alipoona na Spika na Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na huku akiashiria namna mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulivyoundwa na jinsi ulivyoweza kudumu na fikra yake ya mapambano amesisitiza kuwa, haiwezekani kufikia kwenye malengo makuu na matukufu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu pasi na kuendelea na fikra ya kupambana na kambi ya kibeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyouawa shahidi Imam Musa al Kadhim AS na kuongeza kuwa, sababu inayoifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ishikilie msimamo wake wa kuendelea na mapambano si kwa kuwa inapenda vita, bali ni kwa sababu akili inahukumu kuwa, mtu ana wajibu wa kujiandaa vizuri wakati anapopita katika eneo lililojaa maharamia, na lazima awe na nguvu na uwezo wa kutosha wa kujilinda mbele ya maharamia hao.
Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kuwa, ulimwengu wa leo umejaa maharamia wanaopora heshima, utambulisho na maadili ya kibinadamu na kubainisha kuwa: Mabeberu wamejiimarisha kielimu, kiutajiri na nguvu za kijeshi na kipropaganda na wanatumia vitu hivyo kuficha jinai zao kubwa kwa kujifanya wema mbele ya walimwengu, kumbe ni wasaliti wa ubinadamu na wanaendesha vita vya kikatili katika maeneo mbalimbali duniani.
Jamhuri
ya Kiislamu ya Iran imesema iko tayari kutumia uwezo wake wa kupambana
na ugaidi katika kuisaidia Nigeria kuwanusuru wasichana zaidi ya 200
waliotekwa nyara na kundi la kitakfiri la Boko Haram. Katika mahojiano
maalumu na Press TV, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran
anayeshughulikia masuala ya Kiafrika na Kiarabu Hussein Amir-Abdollahian
amesema Iran imefanya mazungumzo na maafisa wa Nigeria
katika siku za hivi karibuni kuhusu kadhia hiyo. Amongeza kuwa Iran
imelaani vikali utekaji nyara wa washichana wa shule nchini Nigeria.
Afisa huyo wa Iran ameelezea matumaini yake kuwa vitendo vya kigaidi
vitafika ukingoni kote barani Afrika. Wakati huo huo habari za hivi
punde kutoka Nigeria zinasema magaidi wa Boko Haram wametekeleza hujuma
iliyopelekea watu wawili kupoteza maisha katika mji wa Jos kati mwa nchi
hiyo. Aidha imearifiwa kuwa siku ya Alkhamisi magaidi hao waliwaua watu
28 katika vijiji vilivyo katika jimbo la Borno kaskazini mwa Nigeria.
Jimbo hilo ni kituo cha uasi wa Boko Haram. Wanamgambo wa Boko Haram
wanawashikilia wasichana wa shule wapatao 223 waliotekwa nyara hivi
karibuni katika Jimbo la Borno kaskazini mwa Nigeria. Boko Haram ni
kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana
na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza
nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha
hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.
Utawala wa Kizayuni wa Israel katika siku za hivi karibuni
umebatilisha mamia ya vibali vya kuishi raia wa Palestina katika mji
mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Kuhusiana na
hatua hiyo ya kijuba ya Wazayuni, taasisi ya kutetea haki za Wapalestina
inayojulikana kama 'Mithaq' imetoa ripoti inayoonyesha kuwa, Wizara ya
Mambo ya Ndani ya utawala haramu wa Israel kati ya mwaka 2012 na 2013,
ilibatilisha vibali 241 vya ukaazi kwa Wapalestina kwa madai kwamba mji
huo ni makao ya Wazayuni. Taasisi ya Mithaq inasema hujuma hiyo dhidi ya
Wapalestina inaendelea na kwamba Walowezi wa Kizayuni wanapewa nafasi
za Wapalestina wanaofukuzwa Quds Tukufu. Taarifa ya taasisi hiyo inasema
hatua hiyo ya Tel Aviv haina lengo lingine ghairi ya kuuyahudisha mji
wa Quds unaobeba msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha
Waislamu.
Ripoti ya taasisi ya kutetea haki za Wapalestina inaelezea
unyama wanaotendewa raia wa Palestina wanaoishi katika mji wa Quds
ikisema kuwa, waliofutiwa vibali vya kuishi mjini hapo wanakatiwa huduma
zote muhimu yakiwemo maji, umeme na hata kuzuiwa matibabu katika vituo
vya afya vya mji huo. Hali hiyo inawafanya kukosa la kufanya na hivyo
kulazimika kuondoka kwa madhila makubwa. Mkuu wa taasisi ya Mithaq, Bw.
Fiyras Swabah amesema kuwa, hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuwapokonya
vibali vya kuishi na kuwafukuza Wapalestina kutoka mji wa Quds ni
kinyume cha sheria na mikataba yote ya kimataifa kama vile kipengee cha
43 cha Azimio la Hague (The Hague Convention) pamoja na kipengee cha nne
cha Azimio la Geneva (Geneva Convention).
Uzandiki na uafriti wa Israel dhidi ya Wapalestina
unafanyika katika hali ambayo utawala huo ghasibu umezidisha kasi ya
ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Wapalestina
unazozikalia kwa mabavu. Ujenzi wa vitongoji ni miongoni mwa sababu
zilizopelekea Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas,
kuondoka kwenye meza ya mazungumzo na Wazayuni mwanzoni mwa mwezi
uliopita. Abbas alisema mazungumzo yataendelea tu iwapo Israel
itawaachia huru wafungwa wa Palestina pamoja na kusimamisha ujenzi wa
vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina ilizopora
na kuzighusubu.
Hujuma na jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina
zinafanyika kwa baraka, ridhaa na himaya ya moja kwa moja ya Marekani na
waitifaki wake ambao hujidai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu.
Hii inadhihirishwa na kitendo cha wabunge wawili wa Marekani; Neil
Johnson na David McNally cha kuungana na Wazayuni katika kuuvunjia
heshima msikiti mtakatifu wa al-Aqsa hivi majuzi. Kitendo hicho
kumewakasirisha viongozi mbalimbali wa Kiislamu kuanzia wale wa kidini
hadi wale wa kisiasa. Nabih Berri, Spika wa bunge la Lebanon kwenye
radiamali yake amewataka viongozi wote wa Kiislamu duniani kuongeza
mashinikizo kwa utawala wa Kizayuni ili ukome kuuhujumu na kuuvunjia
heshima msikiti wa al-Aqsa pamoja na matukufu mengine ya Kiislamu na
yale ya Kikristo.