MATUKIO YANAYOENDELEA KUJIRI NCHINI SYRIA.


Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naeem Qasim amesema njama za Magharibi dhidi ya Syria zimegonga mwamba. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kwamba Magharibi inapaswa iukubali ukweli kwamba imeshindwa nchini Syria na si kutaka kung'ang'ania kufikia malengo yake ya kikoloni katika nchi hiyo. Sheikh Naeem Qasim ameongeza kwamba Marekani na waitifaki wake wa Magharibi wametumbukia kwenye kinamasi cha mchafukoge na wala hawawezi kufikia malengo yao katika hali ambayo Syria imegeuka kuwa mahala pa mkusanyiko wa makundi yanayobeba silaha yenye misimamo ya kufurutu mpaka kutoka pembe tofauti za dunia.
Katika jinai yao ya karibuni kabisa, magaidi waliopiga kambi nchini Syria juzi Jumatano waliwaua raia 16 wakiwemo wanawake na watoto katika eneo la Karam Zaitun lililoko kwenye mji wa Homs katikati mwa nchi hiyo. Jinai hiyo ilifanywa masaa mawili tu baada ya miripuko miwili ya mabomu iliyotokea katika eneo la Karam Louz, katika mji huohuo wa Homs na kusababisha vifo vya raia 25 na kuwajeruhi wengine 107. Sambamba na matukio hayo, kanali ya televisheni ya al Manar ya Lebanon imetangaza kuwa kijiji cha Rankus kimekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wabeba silaha. Kijiji hicho kilikuwa moja ya vituo vikuu vya magaidi ambao sasa wamesambaratishwa na kukimbilia maeneo ya milimani. Katika operesheni iliyotekelezwa na jeshi la Syria la kukikomboa kijiji cha Rankus, magaidi kadhaa waliangamizwa akiwemo Abu Talha al Baghdadi, mmoja wa viongozi wakuu wa kundi la kigaidi la Jabhatun Nusra katika eneo la al Qalamun. Wakati huohuo duru za Lebanon zimeripoti kuwa wakimbizi wa Syria walioko nchini humo wameanza kurejea makwao. Kwa mujibu wa ripoti za duru hizo, katika siku za hivi karibuni kundi la pili la raia wa Syria waliokuwa wameomba hifadhi nchini humo waliondoka na kurejea nchini mwao. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa idadi ya wakimbizi wa Syria walioorodheshwa nchini Lebanon imepindukia watu milioni moja. Lebanon pamoja na nchi nyengine jirani na Syria zimetoa hifadhi kwa wakimbizi zaidi ya milioni mbili kutoka nchini humo ambao wamelazimika kuyahama makaazi yao na kukimbilia nchi jirani kuomba hifadhi kwa kuhofia mashambulio ya magaidi. Tangu mwaka 2011 Syria imekumbwa na jinamizi la vita vya ndani vilivyoanzishwa na kuongozwa na nchi Magharibi zikishirikiana na baadhi ya nchi, zikiwemo za Kiarabu katika eneo…/ 

 'SHUGHULI ZA NYUKLIA ZA IRAN HAZIWEZI KUSIMAMISHWA'
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema shughuli za ustawi na utafiti wa nyuklia Iran kamwe hazitasimamishwa.
Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo leo Jumatano mjini Tehran alipokutana na wakuu na wataalamu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, ‘wote wanapaswa kufahamu kuwa hata kama mazungumzo (ya Iran na madola makubwa ya dunia) yanaendelea, shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu zitaendelea na kwamba hakuna mafanikio yoyote ya nyuklia Iran yatakayosimamishwa.’ Aidha amesema uhusiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA, unapaswa kuwa wa kawaida. Kiongozi Muadhamu amesema imethibitika kuwa Iran haitaki silaha za nyuklia lakini kila wakati maafisa wa Marekani wanapozungumza kuhusu kadhia ya nyuklia, daima huibua suala la silaha za nyuklia kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Ameendelea kusema kuwa, mazungumzo hayamaanishi kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasalimu amri kuhusu malengo yake ya sayansi ya nyuklia. Ayatullah Khamenei amesema wawakilishi wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia wanapaswa kusisitiza kuhusu kuendelea utafiti na ustawi wa nyuklia. Ameongeza kuwa hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kulegeza msimamo kuhusu kusimamishwa shughuli za nyuklia za Iran. Ayatullah Khamenei amesema wawakilishi wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia hawapaswi kukubali udhalilishaji kutoka upande wa pili wa mazungumzo. Aidha amesema wakuu wa serikali ya Iran wanapaswa kuwa na msimamo imara kuhusu mafanikio ya nyuklia nchini.

AYATULLAH KASHANI: IRAN HAITAACHIA HAKI YAKE YA NYUKLIA.
 
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa mjini Tehran amesema leo kwamba taifa la Iran kamwe alitafumbia jicho haki yake ya kisheria ya kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. Ayatullah Mohammad Emami Kashani amesema miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani inapaswa kupanuliwa katika kila kona ya taifa hili ili vijana wenye ujuzi katika uga huo waweze kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la nchi yao. Khatibu huyo wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran amesema Iran ni mwanachama mwaminifu kwenye mkataba wa kuzuia uzalishaji na uenezaji wa silaha za atomiki (NPT) na kwa mujibu wa mkataba huo, kila nchi mwanachama ina idhini ya kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Ayatullah Kashani pia amezungumzia azimio lililopitishwa majuzi na Bunge la Ulaya dhidi ya Iran ambapo amesema azimio hilo halina itibari yoyote mbele ya taifa adhimu la Iran. Amesisitiza kwamba hatua ya wabunge wa Umoja wa Ulaya imeonyesha uadui wa wazi dhidi ya Iran na thamani za Kiislamu hapa nchini. Azimio hilo linadai eti ukiukwaji wa haki za binadamu hapa nchini umekithiri.