Kwa kutofautiana mwanadamu na viumbe vingine, na kwa ubora wake kwao,
Mwenyezi Mungu amempa akili ambayo kwayo anamiliki uwezo wa kufikiri na kutoa
rai, na kwa akili hiyo amepewa utashi wa kuweza kuchukua maamuzi na uhuru wa
kuchagua. Na kwa hiyo amekuwa anastahiki taklifu na kusemeshwa na Mwenyezi
Mungu, na amestahiki kupata malipo anapotii, na anastahili adhabu kwa maasi, na
kwa akili yake na utashi wake mwanadamu anaweza kufanya kazi ya kuistawisha
ardhi na kufanya maisha yawezekane na kunufaika na kheri za ulimwengu.
Hivi ndivyo ilivyotaka hekima ya Mwenyezi Mungu, mwanadamu awe ni mwenye
kufikiria, mwenye matakwa, mwenye uhuru wa maamuzi na hiyari ya kuchagua,
lakini baadhi ya miongozo miovu katika ulimwengu wa mwandamu mwenyewe, na ni
kutoka ndani ya watu wa jinsi yake, inajaribu kumnyima sifa hii tukufu ambayo
Mwenyezi Mungu amempa. Ambapo baadhi ya watu wanakwenda mbio kuwadhibiti walio
kando yao miongoni mwa wanadamu na wanapora uhuru wao wa kufikiria na haki yao
ya kuchagua. Mwanadamu amekabiliwa na bado angali anakabiliwa na aina mbili za
majaribio ya ukandamizaji na udhibiti:
Ukandamizaji wa Kimwili: Kudhibiti harakati zake na shughuli zake, na Ukandamizaji wa
Kifikra: Kupora uhuru wa rai yake, na haki yake ya kujieleza. Na ikiwa
mwonekano wa ukandamizaji wa kimada umeshamalizika, hakika vitendo vya
ukandamizaji wa kifikra bado vingalipo sana, hususan katika jamii zetu za Kiafrika
na za Kiislamu. Na ukandamizaji wa kifikra unamaanisha: Kwamba upande fulani
unaipa nafsi yake haki ya kuwapangia wengine maeneo ya kufikiri, na unakwenda
mbio kuwalazimisha wakubali rai zake na fikira zake kwa njia ya ubabe na
udhibiti.
Na miongoni mwa mwonekano wa ukandamizaji wa kifikra ni haya yafuatayo:
1.Kulazimisha rai kwa wengine kwa nguvu na kupora uhuru
wao katika kuchagua.
2.Kupora haki za kimada na kimaanawi kwa wengine kwa
sababu ya kuwachagulia wao fikra.
3.Dharau na muamala mbaya kwa wenye rai tofauti.
Kwa nini kuwe na ukandamizaji wa kifikra?
Ikiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amempa mwanadamu akili ili afikiri kwa
akili hiyo, na utashi ili aamue na kuchagua, na kubeba jukumu la uamuzi wake na
uchaguzi wake, kwa nini baadhi wanajaribu kuwanyima wengine haki ya kutumia
kipaji hiki cha kiungu na kunufaika nacho, hivyo wanatumia ukandamizaji dhidi
ya akili za wengine na utashi wao, wao wanafikiria kwa niaba ya watu, na
kuwalazimisha watu kukubali rai zao. Na mwenye kujaribu kukhalifu na kutumia
uhuru wake wa kufikiri na haki ya kuchagua rai aliyokinaika nayo, basi atapata
adhabu na adha kutoka kwao! Ambapo wanatumia kila njia ya kibano na adhabu ya
kimada na kimanawi dhidi ya wanaoasi mamlaka yao ya kifikra.
Hakika sababu halisi ya watu hawa kutumia ukandamizaji wa kifikra
aghlabu ni msukumo wa kimaslahi, kwa lengo la kupata mamlaka dhidi ya wengine
na kwa kufuata kwao ubinafsi. Lakini wao wanazungumza sababu nyingine
wanayoiegemezea vitendo vyao vya ukandamizaji wa kifikra, nayo ni msukumo wa
ikhilasi kwa ajili ya haki ambayo wanaiamini katika rai yao, na raghaba ya
kutaka kueneza haki na kuwaongoa wengine.
Na tunapotafakari madai haya na kujadili kisingizio hiki katika mwanga
wa akili na sharia, tunakuta ni madai ya uongo na kisingizo cha kimakosa. Hiyo
ni kwa sababu madai yao ya kwamba rai yao ina haki yanakabiliwa na madai
yanayofanana na hayo kutoka kwa wengine, kwani kila mwenye dini au madhehebu au
rai na anaona kuwa njia yake ni ya haki, je wanakubali jaribio la wengine la
kulazimisha rai zao juu yao?
Hakika mwanadamu kuitakidi usahihi wa rai yake, na ikhilasi yake katika
rai hiyo, na raghaba yake ya kufuatwa na wengine, yote hayo ni mambo ya
kisharia, lakini sio kwa kulazimisha na ukandamizaji, bali ni kwa njia ya
kuwakinaisha wengine rai hiyo, na mwenye kukataa kukinaika basi yuko huru
katika uchaguzi wake, sawasawa awe katika haki au katika batili, na si akili
wala mantiki kumlazimisha.
Na kwa kuwa kwa kawaida nyanja ya kidini huwa inapata mtihani wa kuwepo
makundi na pande zinazotumia ukandamizaji wa kifikra na zinakwenda mbio
kulazimisha rai zake, kwa kuzingatia kwamba huo ni wajibu wa kidini, na ni
taklifu ya kisharia, basi ilikuwa ni lazima kujadili vitendo hivi katika mwanga
wa mafunzo ya kidini na dhana yake. Je, dini inaruhusu kutumia ukandamizaji wa
kifikra kwa maana ya kulazimisha rai kwa nguvu na kupora haki za wanaokhalifu,
na kuwa na muamala mbaya pamoja nao?
Hakika ukisoma kwa uelewa Aya za Qur'ani Tukufu, maandiko ya Sunnah,
sira tukufu ya Nabii, na kauli na sira ya Maimam wa Ahlulbait (as), utakuta
mkusanyiko wa dhana na mafunzo ya kidini unatia mkazo juu ya uhuru wa mwanadamu
na haki yake katika kuchagua, na kwamba anabeba jukumu la maamuzi yake na
uchaguzi wake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yanapinga ukandamizaji na
kulazimisha fikra juu ya watu.