Itikadi zangu na Waislamu wote ni yale masuala yaliyoelezwa kwenye Qur’an Tukufu na kubainishwa na Mtume Muhammad (S.A.W.W) na viongozi wa kweli baada yake. Msingi na asili ya itikadi hizo zote ambao pia ndio muhimu zaidi na wenye thamani kuliko zote ni msingi wa Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa msingi huo tunaamini kwamba, muumba wa Ulimwengu na mwanadamu ni dhati takatifu ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka ambaye ni mjuzi wa yote, muweza wa kila kitu na mwenye kumiliki kila kitu. Msingi huo unatufunza kwamba, mwanadamu anapaswa kusalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu peke yake, na hapaswi kumtii Mwanadamu yeyote isipokuwa yule ambaye kumtii kwake ni kumtii Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo aidha, mwanadamu yeyote hana haki ya kuwalazimisha wanadamu wengine kunyenyekea mbele yake. Msingi huo vilvile unatufunza msingi wa uhuru wa mwanadamu na kwamba, mtu yeyote hana haki ya kumnyima uhuru mtu mingine, jamii au taifa lolote. Hana haki ya kumuwekea sheria na kumpangia kanuni za mwenendo na mahusiano yake kwa kutegemea ufahamu wake ambao ni nakisi mno, au kwa msingi wa matamshi na matamanio yake. Kwa mujibu wa msingi huo pia tunaamini kwamba, uwekaji wa sheria kwa ajili ya maendeleo umo mikononi mwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka, kama ambavyo kanuni za ulimwengu na maumbile zimewekwa nay eye Mwenyezi, na saada na ukamilifu wa mwanadamu na jamii umo katika kutii sheria za Mwenyezi Mungu ambazo zimebainishwa kwa mwanadamu kupitia Mitume wake; na kwamba, kuporomoka kwa mwanadamu kumetokana na kunyimwa uhuru na kusalimu amri mbele ya wanadamu wengine. Kwa msingi huo, mwanadamu anapaswa kupambana dhidi ya vizuizi na minyororo ya utumwa na kukabiliana na wale wanaomuita kwenye utumwa, na pia kujikomboa yeye na jamii ili watu wote wasalimu amri na kuwa waja wa Mwenyezi Mungu. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana sheria zetu za kijamii zikaanza kwa kupambana na madola ya kidikteika na kikoloni. Msingi huo wa Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu vilevile unatufunza kwamba wanadamu wote ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye muumba wetu sisi sote, na wote ni viumbe na waja wake. Kimsingi, wanadamu wote ni sawa, na suala pekee linalomfadhilisha na kumfanya mtu kuwa bora kuliko mwingine ni takwa (uchamungu) na kujiepushana upotofu na maasi. Kwa msingi huo, jambo lolote linalovuruga msingi wa usawa katika jamii na kueneza upendeleo usiokuwa na msingi wowote linapaswa kupigwa vita.”
Imam Khomein alikuwa akisema: “Mizani na kipimo katika dini ya Kiislamu ni radhi za Mwenyezi Mungu na wala si Shakhsia za watu. Tunazipima Shakhsia za watu kwa kutumia haki, na wala si kupima haki kwa kutumia mizani na uzito wa watu. Mizani siku zote ni haki na uhakika.”