UTAWALA




"Ewe Mwenyezi Mungu, hakika wewe unafahamu kuwa yale yaliyotoka kwetu hayakuwa kwa ajili ya kugombania utawala wala kupata chochote kati ya mabaki ya kinachosagika. Lakini yalitoka kwa ajili ya kuhami mafunzo ya dini Yako na kudhihirisha wema katika nchi yako, ili wasalimike wale waliyodhulumiwa miongoni mwa waja Wako na zifanyiwe kazi hukumu Zako zilizoachwa."
KUIFUATA HAKI NA KUIDHIHIRISHA VITENDONI: Atakayeifanya haki kuwa ndio dira basi watu watamfanya mtawala. Atakayeitawala nafsi yake atapata utawala. Utawala wako ukipenya hadi ndani ya nafsi yako basi nafsi za watu zitajikusanya kuelekea kwenye uadilifu wako. Kiongozi bora ni yule ambaye matamanio yake hayamwongozi. Kiongozi mwenye akili sana ni yule anayeitawala nafsi yake kwa ajili ya raia kupitia yale yanayoangusha hoja za raia dhidi yake, na akawatawala raia kupitia yale yanayothibitisha hoja yake dhidi yao.
USHUJAA KATIKA KUTEKELEZA HAKI NA KUSIMAMISHA UADILIFU: Imam anahitaji moyo wenye akili na ulimi wenye kauli na moyo mpana ili asimamishe haki nzito.
NIA NJEMA: Mtawala bora ni yule mwenye vitendo na nia njema, mwadilifu kwa askari wake na raia wake.
UFASAHA WA MANENO: Imam anahitaji….ulimi wenye kauli.
IHSANI KWA RAIA: Atakayewafanyia ihsani raia wake Mwenyezi Mungu humtandazia mbawa za rehema zake na humwingiza katika msamaha wake. Atakayewafanyia ihsani watu wake anastahiki utawala.
KUENEZA UADILIFU KWA WATU WOTE: Nguzo ya utawala ni uadilifu. Atakayefanya uadilifu utawala wake hupenya. Aliye mwadilifu katika utawala wake hatohitajia wasaidizi wake. Atakayetenda kwa uadilifu Mwenyezi Mungu atalinda utawala wake. Mwenye kuzidi uadilifu wake siku zake husifika. Mtawala mwenye maadili bora ni yule anayewajumuisha watu kwa uadilifu wake.
UTAWA WA NAFSI: Mtawala bora ni yule mwenye kuizuia sana nafsi yake. Mbora ni yule asiyebabaishwa wala kudanganywa huku tamaa hazimlaghai.
UCHUMI NA KURATIBU MAISHA: Hatoangamia yule mwenye kufanya iktiswadi. Siasa nzuri hudumisha utawala. Uratibu mzuri na kujiepusha na ubadhirifu ni utawala bora.
UADILIFU WA NAFSI: Uadilifu dhidi ya nafsi ni pambo la utawala. Zaka ya nguvu ni uadilifu dhidi ya nafsi.
UPOLE: Msingi wa utawala ni kutumia upole. Siasa nzuri ni upole.
UVUMILIVU: Uvumilivu ni msingi wa utawala. Nguzo ya utawala ni kifua kipana (uvumilivu). Msamaha ni Zaka ya uwezo. Muadhibu mtumwa wako amwasipo Mwenyezi Mungu lakini msamehe akuasipo wewe. Utawala wa uadilifu hupatikana katika mambo matatu: Kulainika katika jambo ulilo na uhakika nalo, kulipiza kisasi katika jambo la uadilifu na kumpendelea mwenzio katika jambo ulilokusudia.
KUTETEA DINI: Ifanye dini kinga ya dola yako, na shukurani kinga ya neema yako, hivyo kila dola inayozungukwa na dini haishindwi, na kila neema inayokingwa na shukurani hainyang’anywi.
KUJIZUIA KWA BIDII: Omba msaada wa uadilifu kwa kuwa na nia njema kwa raia, kupunguza tamaa na kuzidi kujizuia dhidi ya maasi.
KUHISI KUWA MAMLAKA NI AMANA YA MWENYEZI MUNGU ILIYO JUU YAKO: Hakika mtawala ni muhazini wa Mwenyezi Mungu hapa ardhini. Hakika mamlaka yako si wito wa chakula kwa ajili yako.
KUWA MACHO: Ambaye hayajamdhihirikia akiwa macho hawatomnufaisha chochote walinzi wake. Miongoni mwa alama za dola ni kuwa macho (kuwa chonjo) ili kulinda mambo.
KUTOJIVUNIA NGUVU: Mwenye hadhi hajivunii cheo alichopata hata kama ni kikubwa namna gani, na dhalili hujivunia cheo chake.
KUAMRISHA YANAYOWEZEKANA: Ukitaka utiiwe omba yanayowezekana. Mgao sahihi wa kazi na kuainisha majukumu ya kila mmoja: Kila mwanadamu kati ya watumishi wako mpe kazi yake ambayo utamwajibisha kwayo, kufanya hivyo ni bora ili wasitegeane.
KUGAWA WEMA: Atakayetoa wema wake atastahiki uraisi. Ukarimu ni utawala. Anayetoa cheo chake husifika. Pambo la utawala ni kuwapendelea watu (kabla ya nafsi yako). Rejea: Ghurarul-Hikam Wa Durarul-Kalim cha Al-Amidiy, sehemu ya nne, Uk. 327 – 348.
MUHTASARI: Uislamu ulikuja kuanzisha dola ya Mwenyezi Mungu yenye mpangilio wa Mwenyezi Mungu na utawala wa kuigwa ambao utamhakikishia mwanadamu wema wa sasa na wa baadaye. Mtume (s.a.w.w.) kiongozi aliasisi dola na kusimamisha nguzo zake. Ama wasii wake mlinzi wa ujumbe wake alibainisha mafunzo ya dola ya kuigwa baada ya kufukuza uovu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.). Akabainisha sababu za kudumu dola, kukamilika na kuendelea. Akabainisha sababu za kuporomoka dola, ustaarabu wake na utamaduni wake. Ujumbe wake wa kuigwa aliyoutuma kwa gavana wake wa Misri Malik Al-Ashtar unatoa taswira halisi timilifu ya utaratibu wa utawala wa kiislamu.