1- Mola mwingi wa Rehema, twakushukuru jaliya
Mtume mpe salama, na watoto wake piya
Ni hao waliozama, kitabu kukichambuwa
Kafariki Bi Fatma leo tunamliliya.
2- Kajitokeza Fatma, mengi ametufanyiya
Apendeza kilazama, kama alivyo Nabiya
Ibilisi amezama, hawezi kumuingiya
Kafariki Bi Fatma leo tunamliliya.
3- Muhammad amesema, kwa kurudia rudiya
Kipande changu cha nyama, ni Fatma Zahriya
Na mimi yananiuma, mabaya akifanyiwa
Kafariki Bi Fatma leo tunamliliya.
4- Huyu mwanangu Fatma, hana wa kumfikiya
Wanawake wote wema, hadi iumbwe duniya
Hadi siku ya Kiyama, Fatma ni Malkiya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
5- Nyumbani kwa huyu Mama, ndipo pa kukimbiliya
Masikini na Yatima, wote walimtambuwa
Yeyote aliyekwama, kwake alikimbiliya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
6- Aliletewa Fatma, Kikongwe kimezidiwa
Kilichokuja kwa wema, Madina kutembeleya
Na njaa inamuuma, akamwambia Nabiya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
7- Apelekwe kwa Fatma, hadi alipoingiya
Akaambiwa Fatma, babu kaharibikiwa
Muhammad kamtuma, uje kumsaidiya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
8- Akiba yake Fatma, alikwisha kuitowa
Mkufu wake Fatma, Mzee kaupokeya
Hutoki kwa huyu Mama, bila kukuzawadiya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
9- Akarudi kwa heshima, mkufu kashikiliya
Sahaba mwenye heshima, mkufu kaununuwa
Babu kataja gharama, palepale akapewa
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
10- Mkufu wake Fatma, hajabu karejeshewa
Mkufu wa huyu Mama, Mzee kasitiriwa
Kakombolewa mtumwa, hajabu ukarejeya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
11- Hivi alivyo Fatma, hivi ndivyo sawa sawa
Wazazi wake Fatma, ni Khadija na Nabiya
Bahari mbili za wema, ndio alimotokeya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
12- Alipokufa Hashima, vurugu ilitokeya
Kwenye nyumba ya Fatma, watu wamekimbiliya
Akaumizwa Fatma, dini akiiteteya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
13- Afya ya bibi Fatma, ikaanza kupoteya
Hapana tena uzima, tangu kufa kwa Nabiya
Akiuwawa kinyama, usije kumkimbiya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
14- Akausia Fatma, Zainabu kumwambiya
Hussein kumtizama, mwanangu nakuusiya
Akiuwawa kinyama, usije kumkimbiya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
15- Ali akamtazama, nae kamchaguliya
Akamuowe Fatma, wajina ametimiya
Upate mtoto mwema, mlinzi wa Husseiniya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
16- Maagizo ya Fatma, kamwe hayakurejeya
Abbasi mtoto mwema, Mola akawaleteya
Shujaa asiyekoma, hadi kaaga duniya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
17- Kwa leo bibi Fatma, aiaga duniya
Kaacha mipango vyema, kwa mila yake Nabiya
Tangulia ee Fatma, katuombee shifaa
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
18- Beti hii nasimama, siwezi kuendeleya
Roho yangu yaniuma, Fatma akiumiya
Hiyo siku ya Kiyama, tutakuja jioneya
Kafariki bi Fatma leo tunamliliya.
Mtunzi: Juma N. Magambilwa (Juma Shia)
Kwa maoni Simu namba: (+255) 0712 147 889 - (+255) 0222664158, email afroshiatz@yahoo.com