Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Saba Rabiul Thani mwaka 1435 Hijria, inayosadifiana na Machi Mosi mwaka 2014 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita sawa na tarehe 10 Esfand 1357 Hijria Shamsia, Imam Khomeini MA aliwasili katika mji wa kidini wa Qum ulioko kusini mwa Tehran. Mnamo mwaka 1343 Hjria Shamsia, Imam Khomeini alibaidishiwa nje ya Iran na utawala wa Kifalme wa Shah. Hata hivyo mfalme Shah alipinduliwa katika mapambano ya mfululizo ya wananchi Waislamu wa Iran yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA. Baada ya kupinduliwa mfalme Shah, Imam Khomeini MA alielekea katika mji wa Qum katika siku kama ya leo na miezi kadhaa baadaye alilazimika kuhamia mjini Tehran kutokana na wajibu na udharura wa kuweko Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji mkuu.