Kitabu ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza kwa jina la, Shiism in Sunnism. Sisi tumekiita, Ushia Ndani ya Usunni.
Kitabu hiki, Ushia Ndani ya Usunni ni matokeo ya utafiti wa kielimu uliofanywa na fakihi mwanachuoni Sayyid Muhammad RidhaMudarrasi Yazdi juu ya kile kinachoonekana kuwa ni hitilafu za matendo ya kiibada kati ya Shia na Sunni. Na hili likawafanya Masunni ambao ndio wengi waone kila kinachofanywa na Mashia, ambacho hakifanani na kile ambacho wao wanakifanya kuwa ni makosa. Kwa mfano, katika udhu (wudhuu), Mashia wao hupaka miguu badala ya kuosha kama wafanyavyo Masunni na kukiona kitendo hicho kuwa ni makosa. Katika swala, Mashia wao wanaona kuswali kwa kukusanya swala ni sahihi ambapo Masunni wao wanakiona kitendo hicho kuwa sio sahihi, na mengine mengi ambayo yamejadiliwa ndani ya kitabu hiki. Lakini kwa utafiti huu alioufanywa mwanachuoni huyu, amethibitisha kwamba yale matendo yote ya kiibada yanayofanywa na Mashia ni sahihi na akayatolea ushahidi kutoka kwenye vitabu vya Kisunni vilivyoandikwa na wanazuoni wakubwa wa madhehebu hiyo, kama ambavyo utaona katika kitabu hiki.
Sisi tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena katika akili za watu.
Kutokana na ukweli huo, Taasisi yetu ya Al-Itrah imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.
Tunawashukuru ndugu zetu, Dk. M. S. Kanju na Aziz Hamza Njozi kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.
Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni mwanga kwa wasomaji wetu na kuzidisha upeo wao wa elimu ya dini.
Kitabu asili yake ni cha lugha ya Kiarabu kwa jina la, Idi ‘l-Ghadir kilichoandikwa na Muhammad Ibrahim al-Muwahhid al-Qazwini. Sisi tumekiita, Idi al-Ghadir.
Idi maana yake sikukuu. Katika Uislamu kuna Idi kubwa mbili: Idi al-Fitri na Idi al-Haji. Idi al-Fitri (Sikukuu Ndogo) ni ya kwanza ambayo Waislamu husherehekea baada ya kumaliza saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na Idi al-Haji (Sikukuu Kubwa) ni ya pili ambayo Waislamu husherehekea tarehe kumi ya mwezi wa Dhulhija wakati mahujaji wanapokuwa wanahiji huko Makka.
Idi hizi zimetajwa katika Qur’ani Tukufu. Lakini pia kuna Idi nyingine ambazo husherehekewa na Waislamu wote na nyingine husherehekewa na baadhi ya Waislamu. Siku ya Ijumaa ni siku ya Idi kwa Waislamu wote. Ugomvi uko kwenye Idi mbili zinazosherehekewa na Mashia: Idi al-Ghadir na Idi al-Mubahila. Katika kitabu hiki mwandishi anaelezea kuhusu Idi al-Ghadir, chanzo chake, wapi ilitokea na madhumuni yake.
Kwa ufupi Idi hii chanzo chake ilikuwa ni tukio kubwa sana la kihistoria katika Uislamu lililotokea sehemu ijulikanayo kama Ghadir khumm wakati Mtukufu Mtume alipokuwa anarejea kutoka Makka kutekeleza Hija yake mashuhuri iitwayo, Hija ya Kuaga (Hijjatul Widaa).
Madhehebu zote za Kiislamu zinakubaliana kutokea kwa tukio hili, lakini wanachotofautiana ni tafsiri ya khutba ambayo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliitoa sehemu hiyo akiwa juu ya mimbari iliyotengenezwa kwa matandiko ya ngamia. Haya ndio ambayo msomaji atayasoma na kupata maelezo yake ndani ya kitabu hiki. Tafadhali fuatana na mwandishi.
Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni vitu ambavyo havina nafasi tena katika akili za watu.
Kwa hiyo, Taasisi yetu ya Al-Itrah imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu hususan wazungumzaji wa Kiswahili.
Tunamshukuru ndugu yetu Abdul-Karim Juma Nkusui kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kukitarjumi kitabu hiki kwa Kiswahili kutoka lugha ya asili ya Kiarabu. Aidha tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake. Allah awalipe wote malipo mema hapa duniani na kesho Akhera – Amin.
Mchapishaji
Al-Itrah Foundation.
S.L.P - 19701,
Dar es Salaam,Tanzania.
Simu: +255 22 2110640
Barua Pepe: alitrah@raha.com.