KWA NINI IMAM HUSSEIN (a.s) ALISIMAMA DHIDI YA MALUUNI YAZID IBN MUAWIYYAH NA KUKATAA KULA KIAPO CHA UTII?



Imam Hussein (a.s) alielewa kwamba kula kiapo cha utii kwa Yazid kusingeleta faida yeyote kwa Ummah wa Kiislamu bali kungehatarisha uhai wa Uislamu. Imam alikuwa hana uchaguzi bali kuulinda na kuuchunga Uislamu na kukabiliana na Yazid na madai yake ya kuwatawala Waislamu hata ikibidi kujitolea Muhanga maisha yake na ya wafuasi wake wapendwa.
Kumkubali Yazid kama Khalifa wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w), kiongozi na mwakilishi wa Waislamu itakuwa na maana ya kuharibu kazi ngumu aliyoifanya Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s) ya kuusimamisha Uislamu. Itakuwa ni kubomoa dini tukufu ya Mwenyezi Mungu na kuondosha ubinadamu juu ya ardhi. Hivyo ilibidi Imam Hussein (a.s) akatae kutoa kiapo cha utii kwa Yazid. Uislamu ulikuwa ulikuwa hauwezi kudumu mpaka Imam Hussein (a.s) ajitolee Muhanga, yeye ambaye ndiye Imam wa zama hizo, mlinzi wa dini, amani na utu ambaye alikuwa badala ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) na mwakilishi wa Mwenyezi Mungu ulimwenguni.

Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa tayali amemfahamisha Imam tukio hili alipokuwa yungali mdogo ambalo litatokea baada ya kifo chake na Imam alijua upinzani mkubwa unaomsubiri siku za baadaye. Imam Hussein (a.s) alipambanua kwamba njia pekee ya kuamsha Ummah wa Kiislamu kutoka katika usingizi ni yeye kujitoa Muhanga na kila kilicho kitakatifu, na kuufahamisha Ummah kwamba bora mtu kufa kuliko kupigia magoti batili. Shirki siyo tu kuabudu Masanamu, lakini mbaya zaidi kuliko hiyo ni kumkubali kiongozi mpotofu, muovu, twaghuti kama kiongozi. Ni kukana uongozi wa Mwenyezi Mungu na kupigia magoti uongozi wa Shetani.

Hali ya kutisha maisha yake ilimlazimisha Imam Hussein (a.s) kuacha mji wa Babu yake na kuelekea Makkah. Lakini hata Makkah hakuwa na usalama kwa sababu maluuni Yazid alikuwa amepeleka watu wa kumuua Imam mjukuu wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) hata kama atakuwa anatufu Nyumba ya Mwenyezi Mungu! Hali hii ilimlazimisha Imam Hussein (a.s) kuondoka Makkah bila ya kufanya Ibada ya Hijjah-ilhali Hijjah imewadia na kuelekea nji wa kufa ambako Waislamu walikuwa wanamuita aje awaongoze na kwamba wako tayali kula kiapo cha utii kwake kama Khalifa wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Amir wa Waumini.

Tabia za usaliti na udunia na kupenda madaraka na dunia ziliwafanya watu wa kufa kumsaliti Imam Hussein (a.s) na kusalimu amri kwa maluuni Ubaydullah bin Ziyad, gavana wa Yazid katika nji wa kufa. Hali hii ndiyo iliyopelekea Imam Hussein (a.s) mjukuu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kuuliwa kikatili katika ardhi ya Karbala, mnamo tarehe 10 Muharram, 61 H.

"Hakika mauaji ya Hussein (a.s) yana yana joto ndani ya nyoyo za Waumini kamwe halitapoa" Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w)

"Wale wanaolia kwa kusikia msiba wa familia yangu, machozi yao ni kinga kwao dhidi ya Moto na Allah atawaweka Peponi." Rejea: (Bihar al-Anwar, Juz. 44, uk. 279)