1- Mola wetu msifika, Kila kitu akijua
Salamu twazipeleka, Kwa Mtume wa Jalia
Na walio takasika, Watoto wake Nabiya
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
2- Hussein akiwa Makka, watu watu walimpokea
Waumini wakumbuka, enzi za tumwa Nabia
Kamwe huwezi kuchoka, Hussein akiongea
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
3- Yazid kakasirika, tangu aliposikia
Katika mji wa Makka, Hussein aheshimiwa
Majasusi kapeleka, wakapate kumuuwa
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
4- Wauwaji wamefika, Hussein kajiandaa
Japo Hijja imefika, Hussein kajiandaa
Alikwisha vaa shuka, kwa mujibu wa Sheria
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
5- Yabidi avue shuka, kaziepuka ghasiya
Hussein anaondoka, Iraq kuelekea
Isije ndani ya Makka, damu ikamwagika
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
6- Wiki tatu zinafika, Imam anatembea
Kufa bado hajafika, watu wakamzuia
Aliyoyaacha Makka, huko kayakuta pia
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
7- Kaambiwa bila shaka, Muslimu kauliwa
Mwisho kakatwa na shoka, kichwa wamekipanguwa
Wanawe wamewashika, vichwa wakavipanguwa
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
8- Hussein kabadilika, moyoni anaumia
Nini anachokitaka, Yazid wa Muawiya
Siwezi kubadilika, yeye kumpa baiya
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
9- Huru nae ametoka, Imam kumzuia
Na jeshi limefurika, litayari kwa kuuwa
Usalama ukitaka, Yazid mpe baiya
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
10- Imam akatamka, kamwe simpi baiya
Wacheni nirudi Makka, wasijekufa raia
Au nisiende Makka, niende ninapojua
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
11- Imam akageuka, mbali akaangalia
Maadui wamechoka, waumwa kiu na njaa
Huruma ikamshika, huduma kawapatia
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
12- Na wote wakatosheka, hakubaki mwenye njaa
Na maji wametosheka, Hussein kawagawia
Karbala akashika, njia ya kuelekea
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
13- Imam njia kashika, safari yaendelea
Jangwa moja walifika, Farasi kawagomea
Ndipo wakapumzika, Imam akaelewa
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
14- Watu wamekusanyika, wageni kuwangalia
Imam akainuka, wenyeji kuulizia
Wengine wakatamka, panaitwa Nainawa
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
15- Wengine wakatamka, panaitwa Mariya
Kikongwe kikainuka, jina ninalolijuwa
Ni babu akatamka, panaitwa Karbala
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
16- Imam akatamka, babu umesema sawa
Damu itapomwagika, ni hapa tunapoingia
Ndugu zangu tumefika, pa kuiaga dunia
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
17- Ombi letu tunataka, wakisha tushambulia
Msiache kutuzika, enyi mlohudhuria
Kama mtababaika, jueni mnakosea
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
18- Kina mama tunataka, waume wakikataa
Njoni nyie kutuzika, kutuacha ni vibaya
Watoto mje tuzika, wakubwa wakikataa
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
19- Kiasi gani mwataka, aridhi tutanunua
Bei waliotamka, Imam kawapatia
Kamwe msije ondoka, ingawa tumenunua
Kwa heri mji wa Makka, Yazid kanikamia.
Na: Juma S. Magambilwa