KIONGOZI MUADHAMU AFAFANUA KUHUSU UCHUMI WA KUSIMAMA KIDETE.


Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, sera za 'Uchumi wa Kusimama Kidete' ni tadbiri ya muda mrefu katika ustawi wa kiuchumi na kufikia malengo ya juu ya kiuchumi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran alipozungumza na maafisa wa ngazi za juu serikalini pamoja na wakurugenzi wa sekta za uchumi, vyombo vya habari na taasisi za kielimu. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa 'Sera za Uchumi za Kusimama Kidete' ambazo zimetangazwa hivi karibuni zinaweza kutumika katika hali mbalimbali. Ameendelea kusema kuwa sera hizi hazitumiki Iran tu bali nchi nyingi zinatumia mbinu za uchumi wa kusimama kidete kutokana na mgogoro wa kiuchumi duniani. Ayatullah Khamenei amesema kwa upande mmoja Iran inataka kuendelea kuwa na uhusiano wa kiuchumi na dunia na kwa upande wa pili pia inataka kuwa nchi yenye kujitegemea kiuchumi ili isiathirike na sera za madola makubwa duniani ambayo huwa na nia mbaya na haribifu. Amesema, kwa kutekelezwa sera za 'Uchumi wa Kusimama Kidete' Iran itashuhudia kustawi uchumi, uzalishaji mkubwa wa kitaifa, uadilifu wa kijamii, ongezeko la ajira, na maisha bora zaidi kwa wananchi. Kiongozi Muadhamu amesema, lengo jingine la 'Uchumi wa Kusimama Kidete' ni kutumia uwezo mkubwa wa kimaada na kimaanawi wa wananchi, kukabiliana na vikwazo, kutatua matatizo ya kiuchumi na kuzuia uchumi wa nchi kuathiriwa vibaya na mgogoro wa kiuchumi duniani. Aidha amesema lengo jingine la sera hizo ni kukabiliana na vita vya kiuchumi vya adui na kuongeza kwamba: "Vikwazo dhidi ya Iran vilikuwepo hata kabla ya kuanza kadhia ya nyuklia na hata kama mazungumzo ya nyuklia yatafikia natija, vikwazo vitaendelea kwani kadhia hii na kadhia ya haki za binaadamu na masuala mengine ni visingizio tu."


M/MWEKUNDU WATAKA KULINDWA HAKI ZA KINADAMU CAR:

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetoa wito wa kuheshimiwa haki za binadamu hususan Waislamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ripoti zinasema kuwa, Waislamu katika maeneo ya magharibi mwa mji mkuu Bangui wameendelea kuyakimbia makazi yao na kukimbilia katika nchi za Cameroon na Chad kutokana na kuandamwa na wanamgambo wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka. Georgios Georgantas, Mkuu wa Ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ameashiria kuendelea machafuko, mauaji na kuuawa Waislamu na kusisitiza kwamba, kuna haja ya kuheshimiwa haki za binadamu katika nchi hiyo. Wakati huo huo, wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wameelekea Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa shabaha ya kuanza uchunguzi wa kina juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa nchini humo. Taarifa zinasema kuwa, timu ya watu watatu ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa itabaki nchini humo kwa muda wa wiki mbili na kuzungumza na wahanga pamoja na mashuhuda wa matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu.


NJAMA ZA MAGHARIBI KUVURUGA UCHUMI WA WAISLAMU.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema, madola ya Magharibi yanafanya njama za kuzuia ustawi wa kiuchumi na ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi za Waislamu duniani ili kuzuia nchi hizo kujitegemgea. Larijani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran katika, 'Kongamano la Kimataifa Kuhusu Nafasi ya Nchi za Kiislamu katika Mlingano wa Nguvu Duniani'. Spika wa Bunge la Iran ameelezea masikitiko yake kuwa kuna mifarakano baina ya nchi za Waislamu duniani jambo ambalo limepelekea kuwepo maingiliano machache ya kibiashara na hivyo madola makubwa ya Kimagharibi ndio yanayonufaika na hali hiyo. Larijani pia ameashiria njama za nchi magharibi kuzuia nchi za Waislamu kuwa na nguvu duniani ambapo ametoa mfano wa jambo hilo kwa kutaja njama za Wamagharibi za kujaribu kuizuia Jamhuri ya Kiislamu kupata teknolojia ya nyuklia licha ya kuwa wanajua Iran inataka teknolojia hiyo kwa malengo ya amani hasa kutokana na Fatwa ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye amesema matumizi ya silaha za nyuklia ni haramu. Larijani amesema, kusimama kidete ndio njia pekee ya kuziwezesha nchi za Kiislamu kupata teknolojia za kisasa. Ametoa mfano mwingine akisema, nchi za Magharibi zina wasiwasi na makombora ya Iran kutokana na kuwa Iran yenyewe ndio iliyojitegenezea makombora hayo. Larijani amesema nchi za Magharibi zimefeli katika njama zao za kudhibiti kikamilifu utajiri wa anneo la Mashariki ya Kati. Aidha amesema stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa na uhusiano mzuri wa kisiasa na kiuchumi na nchi zote za Waislamu.