Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema hatokuwa tayari katika hali yoyote ile kuitambua rasmi Israel kama nchi ya Kiyahudi. Mahmoud Abbas ametangaza msimamo huo leo alipohutubia hadhara ya vijana wa Kipalestina na kufafanua kuwa wawakilishi wa Mamlaka ya Ndani katika mazungumzo na utawala wa Kizayuni wako thabiti katika msimamo wao na kwamba hawatokubali abadani kuitambua Israel kuwa ni dola la Kiyahudi. Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameshatangaza kwamba ataitambua nchi huru ya Palestina kwa sharti kuwa Mamlaka ya Ndani iutambue utawala huo haramu kuwa ni dola la Kiyahudi.
Katika upande mwengine kituo cha utafiti kuhusu hali za Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni kimetanabahisha juu ya ukiukaji wa haki za wanawake wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza hayo. Akizungumza leo kwa mnasaba wa Siku ya Wanawake Duniani, Mkuu wa kituo hicho Ra’fat Hamdunah ametoa wito kwa waandishi wa habari na jumuiya za kutetea haki za wanawake kuwafikishia walimwengu taarifa za masaibu waliyonayo wanawake 22 wa Kipalestina wanaoishi katika hali mbaya kabisa ya kibinadamu katika jela za utawala haramu wa Israel…/.
ZARIF APUUZA MADAI YA UTAWALA HARAMU WA KIZAYUNI.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif amekosoa vikali tuhuma za utawala haramu wa Kizayuni juu ya kukamatwa meli ya Iran iliyokuwa imesheheni silaha na makombora kuelekea Ukanda wa Ghaza. Akiashiria tuhuma hizo katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri mwenzake wa Indonesia Raden Mohammad Marty Muliana Natalegawa, Zarif amesema kuwa, madai hayo hayana msingi na ni ya kipuuzi na kuhoji kuwa, suala hilo linazidi kutia shaka hasa kwa vile tuhuma hizo zinatolewa sambamba na ziara ya Waziri Mkuu wa utawala huo pandikizi Benjamin Netanyahu nchini Marekani? Amesema kuwa, madai ya Netanyahu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni uongo ambao umezoeleka kwa katika kujaribu kuichafua sura ya Iran, kimataifa. Hii ni katika hali ambayo hadi sasa na licha ya kutoa madai hayo yasiyo na mashiko, utawala katili wa Kizayuni umeshindwa kuthibitisha madai hayo. Juzi makundi ya muqawama ya Palestina ya HAMAS na Jihadul Islami yalikanusha madai ya utawala huo haramu kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imepanga kuyapelekea makundi hayo makombora ya kisasa na kusisitiza kuwa, madai hayo hayana ukweli wowote.
SAUDIA: IKHWANUL MUSLIMIN YA MISRI NI KUNDI LA KIGAIDI.
Saudi Arabia imeitangaza rasmi harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin ya Misri kuwa ni kundi la kigaidi. Utawala wa kifalme wa Saudia umeiweka Ikhwanul Muslimin, inayoendesha harakati zake bila kutumia nguvu na silaha kwenye orodha moja na makundi ya kigaidi ya Al Qaeda, Dola la Kiislamu la Iraq na Sham na An Nusra yanayofanya ugaidi wa mauaji na umwagaji damu nchini Syria kwa lengo la kuiangusha serikali ya nchi hiyo. Uamuzi huo uliotangazwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia kufuatia msimamo wa huko nyuma wa nchi hiyo wa kuuunga mkono uamuzi wa jeshi la Misri wa kumwondoa madarakani rais halali wa nchi hiyo Muhammad Morsi ambaye ni mwanachama wa Ikhwanul Muslimin, umetafsiriwa kama kielelezo cha uungaji mkono kamili wa Saudia kwa hatua za serikali ya Cairo iliyowekwa madarakani na jeshi za kuikandamiza harakati hiyo ya Kiislamu. Itakumbukwa kuwa mara baada ya kuondolewa madarakani Morsi mwezi Julai mwaka jana, Saudia ikishirikiana na baadhi ya nchi nyengine za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ziliipatia serikali ya Misri iliyowekwa madarakani na jeshi msaada wa dola zaidi ya bilioni 12. Serikali ya Misri iliipiga marufuku Ikhwanul Muslimin mwezi Disemba mwaka jana na kuitangaza kuwa ni kundi la kigaidi. Katika radiamali iliyotoa kwa uamuzi huo, Ikhwanul Muslimin imeeleza kushangazwa na uamuzi huo wa utawala wa Kifalme wa Saudia ikisisitiza kwamba harakati hiyo haina sera za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyengine. Akitilia mkazo nukta hiyo, Jamal Khashoggi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa ya Saudia amehoji ni vipi serikali ya Riyadh imechukua uamuzi wa kuiweka Ikhwanul Muslimin kwenye orodha ya makundi ya kigaidi ilhali harakati hiyo haiendeshi harakati zozote ndani ya Saudia wala dhidi ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo?.../.