Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran wameanza kikao chao mjini Tehran. Kikao hicho cha 15 kitadumu kwa muda wa siku mbili na kimeanza kwa hotuba ya mwenyekiti wa baraza hilo Ayatullah Mohammad-Reza Mahdavi Kani. Kati ya wanachama waandamizi wa baraza hilo waliohudhuria kikao cha leo ni pamoja na Rais Hassan Rouhani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu, Ayatullah Hashemi Rafsanjani na Mkuu wa Vyombo vya Mahakama Ayatullah Amoli Larijani. Akihutubia wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Ayatullah Mahdavi Kani ameashiria mazungumzo ya Iran na kundi la 5+1 yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani na kuelezea matumaini yake kuwa wajumbe wa Iran katika mazungumzo hayo watalinda haki za watu wa Iran. Kikao hicho pia kimehutubiwa na mgeni mwalikwa ambaye leo alikuwa ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araqchi ambaye ni mjumbe mwandamizi katika mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1. Araqchi amelifahamisha baraza hilo kuwa haki ya Iran ya kurutubisha madini ya urani imelindwa katika mazungumzo ya nyuklia. Ameongeza kuwa Iran itarutubisha urani kwa kiwango cha 3.5 kwa ajili ya miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani. Baraza la Wanazuoni Wataalamu huchaguliwa kwa kura za wananchi na hufanya vikao mara mbili kwa mwaka kuchunguza masuala muhimu ya kitaifa. Baraza hilo lina jukumu la kusimamia utendaji kazi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na taasisi zinazofanya kazi chini yake. Aidha baraza hilo lina jukumu la kumchagua Kiongozi Muadhamu iwapo hilo litahitajika.
Rais Hassan Rouhani ametoa hakikisho kuwa serikali yake haitakiuka 'mistari myekundu' ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na kundi la 5+1. Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu leo mjini Tehran, Rais Rouhani ameongeza kuwa, katika mazungumzo ya nyuklia, Iran italinda kikamilifu haki zake za kumiliki mradi wa nyuklia wenye malengo ya amani. Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa, vikwazo dhidi ya Iran si vya kiadilifu na walioviweka wamefanya makosa. Ameongeza kuwa vikwazo hivyo vinavyoongozwa na Marekani vinapaswa kuondolewa katika mapatano ya mwisho ya nyuklia kati ya Iran na madola sita yenye nguvu duniani. Amesema iwapo upande wa pili utaonyesha nia njema na iradi ya kisiasa ya kutatua kadhia ya nyuklia, basi mapatano yanaweza kufikiwa katika kipindi cha miezi sita ijayo. Iran imekuwa ikifanya mazungumzo ya nyuklia na kundi la 5+1 linalojumuisha nchi za Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani. Mapatano ya awali ya nyuklia na kundi hilo yalifikiwa Novemba 24, 2013 huko Geneva Uswizi na kuanza kutekelezwa Januari 20. (irib)