ALIYEIVUNJIA HESHIMA QUR'ANI MAURITANI AADHIBIWE:


Chama tawala nchini Mauritania, kimelaani vikali vitendo vya kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu kilichofanyika nchini humo. Ripoti iliyotolewa na chama hicho tawala kinachoongozwa na Rais Mohamed Ould Abdel Aziz, imeeleza kuwa, kukivunjia heshima Kitabu kitakatifu cha Qur’an, ni dhambi isiyosamaheka ambayo wahusika wake wanatakiwa kusakwa na kuadhibiwa. Aidha ripoti hiyo imeongeza kuwa, wahusika wa vitendo hivyo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu, hata kama watakuwa ni kutoka kundi na mrengo wowote ule, lazima wawajibishwe kutokana na vitendo vyao hivyo viovu. Siku ya Jumapili iliyopita watu wanne wasiojulikana, waliingia katika msikiti wa eneo la Tayarat huko kaskazini mwa Nouakchott, mji mkuu wa Mauritania na kuchana nakala kadhaa za Qur’ani Tukufu, suala lililoibua hasira na maandamano ya wananchi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, Januari 3 mwaka huu polisi katika mji wa Nouadhibou, ilimtia mbaroni mtu aliyejulikana kwa jina la Muhammad Ould Sheikh kwa kosa la kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu (SAW), huku Wizara inayoshughulikia masuala ya Kiislamu nchini humo ikiwataka maimamu wa Ijumaa kulaani kitendo hicho katika hotuba zao.Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/habari/mchanganyiko/item/38595-aliyeivunjia-heshima-qur-ani-mauritani-aadhibiwe