WATU WA TANO WAUAWA KATIKA MIRIPUKO YA MABOMU BEIRUT:


Watu watano wameuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia hujuma ya kigaidi iliyofanyika leo kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

Ripoti zinasema mabomu mawili yaliripuka katika mtaa wa Bir Hassan karibu na Ubalozi wa Kuwait na Ofisi ya Idara ya Utamaduni katika Ubalozi wa Iran mjini Beirut. Tayari kundi la kigaidi la Brigedi ya Abdullah Azzam lenye mfungamano na al-Qaeda limeshatangaza kuhusika na hujuma hiyo. Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imesema litaendeleza mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na harakati ya Hizbullah.

Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi mjini Beirut. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bi. Marzieh Afkham amesema waliotekeleza hujuma hiyo ni maadui daima wa usalama na umoja wa taifa la Lebanon na ni vibaraka wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ikumbukwe kuwa mwezi Novemba mwaka jana watu zaidi ya 20 waliuawa shahidi akiwemo mwambata wa utamaduni wa Iran wakati magaidi walipolipua bomu karibu na Ubalozi wa Iran kusini mwa Beirut. Kundi la kigaidil la Brigedi ya Abdullah Azam lilitangaza kuhusika na hujuma hiyo. Kiongozi wa kundi hilo, Majid al Majid raia wa Saudi Arabia alikamatwa mwezi Januari na kufariki dunia siku chache baadaye akiwa gerezani huko Lebanon. (irib)