Kitabu Tawhid na Shirk kinatarajia kutoka hivi karibuni ni tarjuma ya kitabu cha Kiarabu
kiitwacho, at-Tawhid wa ‘sh-Shirk fi ‘l-Qur’ani ‘l- Karim kilichoandikwa
na Sheikh Ja’far Subhani. Sisi tumekiita, Tawhid na Shirk.
Kitabu hiki kinajadili kwa mapana na marefu suala la umoja wa Waislamu
na kuwakosoa wale wanaojaribu kuleta mfarakano na fitna katika dini kwa
kutumia madhehebu, hususan wale wanaowashambulia Mashia katika
vitabu vyao kwamba wao (Mashia) ni makafiri.
Mwandishi katika kitabu hiki anaelezea imani ya Shia katika Tawhid na
jinsi wanavyojiepusha na shirk nukta ambazo wapinzani wa Shia wanazitumia
kuupotosha ukweli juu ya Ushia. Wapinzani hawa hawajishughulishi
kusoma vitabu vya Shia wala kusoma majibu yanayotolewa juu ya vitabu
vyao, bali kazi yao ni kurudiarudia tu yale yaliyotapikwa na watangulizi
wao na kupotosha Ummah kwa kalamu zao zenye sumu.
Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususani wakati huu wa
maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo uwongo, ngano
za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena
katika akili za watu.
Kutokana na ukweli huo, Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua
kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yaleyale
ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.
Tunamshukuru ndugu yetu, Amiri Mussa Kea kwa kukubali jukumu hili la
kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki
Tawhid na shirk
kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.
Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa na changamoto kubwa
kwa wasomaji wetu.
Mchapishaji
Al-Itrah Foundation.
S.L.P - 19701,
Dar es Salaam,Tanzania.
Simu: +255 22 2110640
Barua Pepe: alitrah@raha.com
Kitabu hiki kinachapishwa hivi karibuni, ni cha mafunzo juu ya swala, hususani swala tano za faradhi za kila siku. Ni mfululizo wa masomo yanayotolewa na Taasisi ya Zahra Foundation ya Marekani kwa ajili ya vijana wa Kiislamu walioko shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu.
Swala ni nguzo muhimu sana ya dini. Imepokewa hadithi ikisema kwamba Siku ya Hesabu kitu cha kwanza kuangaliwa ni swala; kama swala ikionekana kuwa safi basi huchukuliwa kwamba matendo yote ni safi, hivyo, mtu huyo hupitishwa moja kwa moja katika Sirati na kupelekwa Peponi. Na imekuja katika hadithi kwamba Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Swala ni nguzo ya dini, mwenye kusimamisha swala amesimamisha dini, na mwenye kuiacha swala hakika ameiangusha dini.” Mtume (s.a.w.w.) akaendelea kusema: “Tofauti baina yetu na ukafiri ni kuacha kuswali (taariku ‘s-swalaa).” Yaani kinachotutofautisha sisi Waislamu na ukafiri ni kuacha swala. Swala ndiyo inayotutofautisha na ukafiri kwa sababu kafiri yeye huwa haswali. Hadithi nyingine kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) inasema kwamba: “Kila kitu kina uso na uso wa dini (ya Uislamu) ni swala.” Kitu cha kwanza kuonekana katika kila kitu ni uso wake, kama uso ni safi huchukuliwa kwamba kitu chote ni safi, kama uso ni mchafu huchukuliwa kwamba kitu chote hicho ni kichafu. Kwa hivyo, hadithi inatuhimiza kuswali ili kuuweka uso wa dini katika hali ya usafi ili dini yetu kwa ujumla iwe safi.
Tumekiona kitabu hiki ni kizuri sana kwa ajili ya vijana wetu walioko katika mashule ya kisekula ambao muda wao wa kuhudhuria madrasa za kidini ni mdogo. Kitabu hiki asili yake ni cha lugha ya Kiingereza, Taasisi yetu ya Al-Itrah imeamua kukichapisha kwa lugha ya Kiswahili ili vijana wa Kiswahili au wanaoongea lugha hii wapate kufaidika na yaliyomo kwenye kitabu hiki.
Mwisho wa kitabu hiki kuna maswali mwanafunzi anatakiwa ayajibu na atume majibu hayo kwa Jameel Kermalli, barua pepe: jameelyk@aol.com
Tunamshukuru ndugu yetu Dkt. Mohamed Kanju kwa kukitarjumi kitabu hiki kutoka lugha ya Kiingereza, pia shukrani zetu ziwaendee wale wote waliosaidia kwa njia moja au nyingine mpaka kuwezesha kitabu hiki kuchapishwa. Allah awalipe wote malipo mema hapa duniani na huko Akhera pia.
Mchapishaji
Al-Itrah Foundation.
S.L.P - 19701,
Dar es Salaam,Tanzania.
Simu: +255 22 2110640
Barua Pepe: alitrah@raha.com