Imam Khomeini ambaye alikuwa akifuatilia kwa makini matukio ya wakati huo ya Iran na ya Kimataifa, alitumia vema fursa iliyojitokeza.
Mwezi Agosti 1977, alitoa ilani akitangaza: Hali ya sasa ya ndani na nje na kuakisiwa kwa jinai za utawala wa Shah katika duru na vyombo vya habari vya kigeni, imetayarisha fursa ambayo inapaswa kutumiwa vilivyo na duru za kielimu na kiutamaduni, rijali wazalendo na Wanafunzi wa vyuo vikuu wa nje na ndani ya nchi na pia jumuiya za Kiislamu katika maeneo yote, na kuanza harakati mara moja bila ya hofu yoyote.
Sehemu nyingine ya ujumbe huo alisema:
Kupuuza haki za mamia ya mamilioni ya Waislamu na kuwatwisha watawala waovu na kuupa fursa utawala usiokuwa halali wa Iran na Serikali ya Israel ya kughusubu haki za Waislamu, kuwanyima uhuru na kuamiliana nao kwa mbinu za karne za kati, ni jinai ambazo zinasajiliwa katika faili la Marais wa Marekani.
Kitendo cha kuuwa Shahidi Ayatollah Alihaj Mustafa Khomeini hapo Octoba 1977 na shughuli kubwa ya maombolezo iliyofanyika nchini Iran kufuatia tukio hilo, ilianzisha tena harakati mpya katika vyuo vya kidini na katika jamii ya Iran.
Katika zama hizo, Imam Khomeini na kwa njia ya kustaajabisha, alilitaja tukio hilo la kuuawa mwanawe kuwa ni katika neema za siri za Mwenyezi Mungu. Utawala wa Shah ulilipiza kisasi kwa Imam kwa kuchapisha makala na kumvunjia heshima katika gazeti la Ittilaat.
Makala hiyo ilifuatiwa na malalamiko makubwa yaliyopelekea kutokea harakati ya tarehe 9 Januari 1978. Katika harakati hiyo ya malalamiko, Wanafunzi kadhaa wanamapinduzi waliuawa. Harakati ya mapambano ilianza tena katika mji wa Qum na katika kipindi kifupi na mazingira yanayotofautiana kikamilifu na yale ya tarehe 5 Juni 1963, harakati hiyo ilienea nchini kote. Shughuli za maombolezo ya siku ya 3,7 na 40 za kuwakumbuka Mashahidi waliokuwa wameuawa katika mapambano ya wakati huo katika miji ya Tabriz, Yazd, Jahrom, Shiraz, Isfahan na Tehran zilichochea tena harakati za mapambano. Katika kipindi hicho chote, jumbe mbalimbali na za mara kwa mara za Imam na kanda za redio za hotuba zake ambazo ziliwahamasisha wananchi kusimama kidete na kuendeleza mapambano hadi kuanguka kwa misingi ya utawala wa kifalme na kuasisi Serikali ya Kiislamu.