HIZBULLAH KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA ISRAEL:


Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, kwa kuwa Israel bado ingalipo, harakati ya Hizbullah itaendelea kuwepo na kusisitiza kuwa, muqawama siyo nishani na medali, bali muqawama ni imani, subira na kujitolea kwa ajili ya malengo matakatifu. Sheikh Naeem Qassim ameongeza kuwa, chokochoko zinazoshuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati zinasababishwa na madola ya Magharibi kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Qassim amebainisha kuwa, Hizbullah iliingia nchini Syria kulisaidia jeshi la nchi hiyo baada ya kupita mwaka mmoja na miezi minane tokea kuanza machafuko nchini humo na wakati huo zilishuhudiwa kwa wazi kabisa njama za kuisambaratisha Syria kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Qassim ameongeza kuwa, lengo la kuingia wanamgambo wa Hizbullah nchini Syria ni kuilinda serikali ya Damascus isiangukie mikononi I mwa makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayoungwa mkono na baadhi ya nchi za Kiarabu na madola ya magharibi. Akizungumzia milipuko ya mabomu iliyotokea wiki chache zilizopita nchini Lebanon, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa, magaidi na makundi ya Kisalafi na yale ya kitakfiri  yamepanga kutekeleza  malengo mawili nchini Lebanon ambayo ni kukabiliana na muqawama na jeshi la serikali ya Lebanon.