MUFTI WA LEBANON ATAHADHARISHA NJAMA ZA WAZAYUNI:


MUFTI WA LEBANON ATAHADHARISHA NJAMA ZA WAZAYUNI:

Sheikh Muhammad Rashid Qabbani Mufti wa Lebanon amesema kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinazusha fitina katika nchi za Kiarabu ikiwemo Lebanon na kuongeza kwamba fitina hizo ni sehemu ya Mpango wa Mashariki ya Kati Mpya lakini mpango huo hautafaulu.

Sheikh Qabbani ameeleza kuwa, Israel inatumia hali hiyo kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayun, kuwahamisha Wayahudi kutoka maeneo tofauti duniani na kuwapeleka ardhi za Palestina zinazokalia kwa mabavu huku ikiwafukuza Wapalestina ambao ndio wamiliki asili wa ardhi hizo. Mufti wa Lebanon pia amekosoa operesheni za kigaidi za kujilipua kwa mabomu nchini Lebanon na Mashariki ya Kati, na kusisitiza kwamba kila mtu anayewaua watu bila hatia kwa kujilipua, basi atakuwa amefanya dhulma na dhambi kubwa.


MAREKANI YAONGEZA MISAADA YAKE KWA UTAWALA WA KIZAYUNI WA ISRAEL:

Habari kuhusu kuongezeka misaada ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel zimeenea hivi sasa katika hali ambayo viongozi wa Marekani wanadai kuwa hawapendelei upande wowote katika mazungumzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni. Likiakisi habari hiyo, gazeti la Kizayuni la Globes limefichua kuwa, kiwango cha misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Israel kimeongezeka mwaka huu wa 2014 na kufikia karibu dola bilioni tatu na milioni 600. Kwa mujibu wa gazeti hilo, misaada hiyo tayari imeshapitishwa na Baraza la Congress la Marekani wakati wa kupasisha bajeti ya serikali ya shirikisho ya nchi hiyo. Kwa upande wake gazeti la Kimarekani la Christian Science Monitor hivi karibuni lilifichua kwamba tangu mwaka 1973 hadi hivi sasa, walipa kodi nchini Marekani wamebeba gharama ya dola bilioni 1,600 kulipia matumizi ya Israel jambo ambalo kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya kiuchumi wa Marekani, fedha zilizotumiwa na Marekani kuilinda na kuikingia kifua Israel ni zaidi ya matumizi ya nchi hiyo katika vita vyake vya Vietnam. La kukumbuka kuwa, duru za kisiasa na vyombo vya habari vya Marekani navyo vinakiri kwamba misaada rasmi ya kila mwaka inayotolewa na Marekani kwa utawala wa Kizayuni bila ya masharti yoyote ni mingi mno ikilinganishwa na kile kinachotangazwa na viongozi wa nchi hiyo. Kwa mfano hivi karibuni, gazeti la kila wiki la American Free Press lilifichua kuwa, tume ya operesheni za nje na mipango inayohusiana na operesheni hizo ya kamati maalumu ya bajeti ya Baraza la Congress la Marekani siku zote inafanya vikao vyake kwa siri kubwa katika chumba kimoja ndani ya jengo la Congress kutokana na kuogopa wanaharakati wa amani wasigundue kiwango cha misaada ya kijeshi inayotolewa na Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Viongozi hao wa Marekani wanaogopa sana kusikia kuwa wananchi wa Marekani wanajua nchi yao inagharamika kiasi gani kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel. Hivi karibuni pia Mark Dankof mwanasiasa wa Marekani ambaye aligombea kiti cha senate katika uchaguzi uliopita nchini humo alisema kuwa, serikali ya Marekani inatumia dola bilioni 10 kila mwaka kuisaidia Israel kwa njia tofauti. Misaada ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni licha ya kwamba nchi hiyo hivi sasa imekumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na nakisi kubwa ya bajeti kutokana na siasa zake za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyinginezo duniani. Misaada mingi ya kigeni ya Marekani inakwenda kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na sehemu kubwa ya misaada hiyo ni ya kijeshi, jambo ambalo linazidi kuipandisha kiburi Israel cha kufanya jinai za kivita na kuzidi kukaidi sheria za kimataifa. Misaada hiyo ya Marekani kwa Israel imeongezeka katika hali ambayo kwa mujibu wa sheria za Marekani kwenyewe, nchi hiyo imepigwa marufuku kuusaidia utawala wowote ule ambao unatumia silaha na fedha za Marekani kwa ajili ya kushambulia au kufanya ukandamizaji. Katika upande mwingine malalamiko ya walimwengu dhidi ya Marekani yameongezeka na kufika hadi ndani ya Marekani kwenyewe ambako wananchi, wanaharakati wa masuala ya amani na wasomi wa Vyuo Vikuu wanalalamikia mara kwa mara misaada hiyo ya Marekani kwa Israel. Cha kushangaza ni kuwa, licha ya kwamba wananchi wa Marekani wamekumbwa na matatizo mengine ya kiuchumi hivi sasa, lakini viongozi wa nchi hiyo wanaendelea kuwakamua walipa kodi wa nchi hiyo na hawafikirii hata angalau kupunguza tu misaada yao kwa Israel. Kwa upande wao wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, serikali ya Barack Obama imeongeza misaada yake kwa Israel kwa nia ya kuziridhisha lobi za Kizayuni nchini Marekani kama njia ya kuandaa mazingira ya kushinda katika uchaguzi ujao, mrengo wenye misimamo sawa na ya serikali ya hivi sasa huko Marekani. 


UN: WAISLAMU WANAKABILIWA NA HATARI CAR:

Afisa mwandamizi wa masuala ya haki za binaadamu katika Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu kuongezeka mashambulizi dhidi ya Waislamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema, magenge ya wanamgambo wanaharibu na kupora misikiti, maduka na nyumba za Waislamu katika maeneo kadhaa ya Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Imearifiwa kuwa, katika siku za hivi karibuni wanajeshi wa Ufaransa walioko Bangui wamewatimua wanamgambo Waislamu wa kundi la Seleka na hivyo kuwaacha raia Waislamu bila ulinzi. Kutokana na hali hiyo magaidi wa Kikristo wanaojulikana kwa jina la anti-balaka wanawashambulia kikatili raia Waislamu wakiwemo wanawake na watoto wadogo na kuwaua kiholela. Kuna askari 1,600 wa Ufaransa na maelfu ya askari wengine wa kulinda amani kutoka nchi za Kiafrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini wameshindwa kuzuia mauaji ya Waislamu yanayofanywa na magenge ya Wakristo. Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yameonya kuwa kuna uwezo wa kutokea mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika. Waziri mkuu mpya wa nchi hiyo Andre Nzapayeke ameunda baraza la mawaziri 20 wakiwemo waungaji mkono wa Seleka na anti-balaka ili kujaribu kurejesha utulivu nchini humo. Mapigano ya ndani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yalianza mwezi Machi mwaka jana baada ya kung'olewa madarakani serikali ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo François Bozizé. (irib)