MAZUNGUMZO YA NYUKLIA, HAKI ZA BINADAMU KATIKA HOTUBA YA KIONGOZI MUADHAMU:
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei jana
alihutubia mjumuiko mkubwa wa maulamaa, wanazuoni na watu wa matabaka
mbalimbali wa mkoa wa Qum sambamba na hauli ya 36 ya harakati ya
kihistoria ya watu wa mji huo dhidi ya utawala wa Shah. Katika hotuba
yake Kiongozi Muadhamu alisema kuwa moja ya mambo muhimu ya harakati
hiyo ya watu wa Qum ni kutegemea imani yao kubwa kwa Mwenyezi Mungu
sambamba na kuwa na maarifa na uoni wa mbali katika mazingira magumu ya
kupambana na adui.
Uzoefu wa kihistoria wa taifa la Iran kabla
na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umeonesha kuwa, taifa hilo
daima limekuwa likiwashinda maadui kwa kutegemea imani yake kubwa kwa
Mwenyezi Mungu na kuwa na maarifa na kuona mbali. Ushindi wa Iran katika
vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam, kuvuka
vipindi na misukusuko mingi na migumu ya vikwazo na kuwa macho mbele ya
njama mbalimbali za kisiasa katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita na
kuweza kuzima njama hizo ni vielelezo vya wazi vya imani kubwa ya taifa
la Iran na kuwa kwake makini katika vipindi mbalimbali vya uhai wa
Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Miongoni mwa mambo
yaliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika
hotuba yake ya jana ni mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea kati ya Iran
na kundi la 5+1. Amesisitiza kuwa mazungumzo hayo hayatokani na
mashinikizo ya vikwazo bali Iran inafanya mazungumzo kwa mujibu wa
maslahi yake.
Baada ya kuja madarakani serikali mpya hapa
nchini, suala la kuamiliana na mfumo wa kimataifa kwa mujibu wa
kuheshimiana lilipewa kipaumbele katika siasa za nje za Jamhuri ya
Kiislamu. Muamala mzuri wa Iran mkabala wa nchi za Magharibi ambao
ulikaribishwa sana na watu wa Ulaya ulizilazimisha serikali za nchi za
Magharibi kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya nyuklia na Iran. Duru
kadhaa za mazungumzo hayo ya Iran na kundi la 5+1 huko Geneva zimeonesha
kwamba, Tehran haikuingia katika mazungumzo kwa sababu ya mashinikizo
ya vikwazo.
Kabla ya kuanza mazungumzo hayo nchi za Magharibi
hususan Marekani zilitishia kuwa zingeshambulia taasisi za kuzalisha
nishati ya nyuklia hapa nchini. Hata hivyo matokeo ya mazungumzo ya
tarehe 24 Novemba 2013 yameonesha kuwa Wamagharibi hawana njia nyingine
ghairi ya kuamiliana na Iran.
Suala la haki za binadamu ni
miongoni mwa mambo yaliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu katika hotuba ya
jana. Amesema Wamarekani hawana haki ya kuzungumzia maudhui ya haki za
binadamu kwa sababu serikali ya Marekani ndiyo mvunjaji mkubwa wa haki
hizo duniani.
Wamagharibi hususan Marekani wamekuwa wakitumia
suala la haki za binadamu kwa ajili ya kufikia malengo yao nchini Iran.
Hata hivyo ushahidi na nyaraka za kuaminika zinaonesha kuwa, wanaodai
kuwa vinara wa haki za binadamu duniani ndio hao hao wavunjaji wakubwa
wa haki hizo. Mauaji ya watoto wadogo na wanawake wa Afghanistan,
Pakistan na Yemen kutokana na mashambulio yanayofanywa na ndege zisizo
na rubani za Marekani (drone), mateso yaliyofanywa na Wamarekani dhidi
ya wafungwa katika jela za Abu Ghuraib huko Iraq, Guantanamo Bay Cuba na
Bagram huko Afghanistan na uungaji mkono wa Washington kwa jinai
zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa
la Palestina ni sehemu ndogo tu ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu
wa Marekani na waitifaki wake.
Na Amir Ibrahim Rutajengwa. (irib)