Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran amesema kuwa, matatizo yanayoukumba ulimwengu wa Kiislamu kwa sasa yanatokana na makundi ya kisalafi na yale yanayowakufurisha Waislamu wengine. Akiwahutubia waumini walioshiriki kwenye ibada ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran, Ayatullah Muhammad Emami Kashani ameongeza kuwa, maadui wa dini ya Kiislamu wanayaunga mkono makundi ya kisalafi yanayowakufurisha Waislamu wengine nchini Syria na Iraq kwa lengo la kushadidisha hitilafu na mpasuko katika safu za Waislamu.
Ayatullah Kashani amesema makundi hayo yamechafua sura na taswira safi ya dini tukufu ya Uislamu na kuongeza kuwa, kuna ulazima wa kuepukana na masuala yanayosababisha mpasuko na hitilafu katika Umma wa Kiislamu. Ayatullah Kashani amesikitishwa na hatua ya Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kufuta mwaliko alioutoa awali kwa serikali ya Iran wa kushiriki mkutano wa kimataifa wa Geneva II wa kujadili mgogoro wa Syria na kusisitiza kuwa, katika kudhamini siasa na malengo ya madola ya kibeberu duniani, Umoja wa Mataifa umethibitisha wazi kuwa damu zilizomwagika za Waislamu wasio na hatia wa Syria na Iraq hazina thamani yoyote. (irib)
AYATULLAH AKHTARI: WAISLAMU WAWE MACHO NA MAADUI.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt (as) ameutaka ulimwengu wa Kiislamu kuwa macho katika kukabiliana na fitina za kimadhehebu zinazopandikizwa na maadui wa Uislamu kwa lengo la kuzusha mfarakano katika Umma wa Kiislamu.
Akihutubia waumini kabla ya Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran, Ayatullah Muhammad Hassan Akhtari amesema kuwa, Uwahabi hauna chimbiko katika Uislamu na kusisitiza kwamba, kila mahala zinapomwagika damu za Waislamu, wafuasi wa kundi hilo wanahusika na jinai hizo. Ayatullah Akhtari ameongeza kuwa, tapo la Kiwahabi, kwa kutumia mwavuli wa makundi yanayowakufurisha Waislamu wengine, limekuwa mstari wa mbele kutekeleza njama na malengo machafu ya madola ya kibeberu duniani ya kutaka kuasisiwa serikali vibaraka zitakazotii amri za madola hayo na kuzusha mifarakano kati ya Waislamu.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahbul Bayt (as) ameongeza kuwa, tokea zama za uhai wa Mtume Muhammad (saw) hadi leo hii, maadui wa dini tukufu ya Uislamu wanafanya njama mbalimbali za kuzusha hitilafu na mpasuko kati ya wafuasi wa dini hii tukufu. Ameongeza kuwa, hata baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yalijitokeza makundi mbalimbali yaliyofanya njama za kuwataka wananchi wayape mgongo mapinduzi haya, lakini uoni wa mbali wa wananchi na tadbiri ya Imam Khomeini (ma) viliweza kuzima njama hizo