Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Quds huko Palestina amekikosoa vikali kimya cha nchi na taasisi za Kiarabu na Kiislamu kuhusiana na uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.
Yassin Hammoud ameonya kuhusiana na mipango mipya ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kugawa nyakati na sehemu baina ya Waislamu na Mayahudi katika msikiti wa al-Aqswa na kusisitiza kwamba, mji wa Quds unapitia kipindi nyeti na cha kihistoria na kwamba, watu wote wana jukumu kuhusiana na kadhia hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Quds huko Palestina amesisitiza kwamba, kimya cha umma wa Kiislamu na Kiarabu mbele ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Quds inayokaliwa kwa mabavu kinahesabiwa kwamba ni kuwa pamoja na utawala huo ghasibu katika njama na mipango yake.
Yassin Hammoud ameitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kuchukua hatua za haraka na za maana ili kusimamisha mara moja mipango ya kijinai ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Masjid al-Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu.