Khatibu wa muda wa sala ya Ijumaa ya hapa Tehran amesema kuwa serikali ya Marekani imeendelea kuwatendea jinai wananchi wa Iran katika miaka baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ayatollah Muhammad Ali Muvahidi Kermani Khatibu wa sala ya Ijumaa ya hapa Tehran ameashiria kufanyika kwa hamasa nchini Iran maandamano ya Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari tarehe 13 mwezi Aban sawa na tarehe Nne Novemba na kupigwa shaari za "mauti kwa Marekani" na kuwabainishia wananchi wa Iran kwamba, hawapasi kughafilika mbele ya maadui wakubwa wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa sababu kughafilika na kutokuwa makini mkabala na maadui hao kuna madhara makubwa. Ayatollah Muvahidi Kermani ameashiria jinai za mfululizo za Marekani katika miaka ya hivi karibuni na pia mapambano ya Imam Khomeini Mwenyezi (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya Marekani na mfumo wa ubeberu na kueleza kuwa, Imam Khomeini alikuwa macho mbele ya njama zote zilizotekelezwa na Marekani na mfumo wa ukistikbari dhidi ya wananchi wa Iran na kwamba alikuwa akichukua misimamo thabiti katika uwanja huo. Khatibu wa sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema kuwa Jack Straw Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje wa Uingereza amekiri katika mahojiano na kanali ya televisheni ya BBC juu ya uadui wa Marekani na Uingereza kwa taifa la Iran na kuongeza kuwa wachukuaji wakuu wa maamuzi wa mtawala dhalimu Shah wa Iran zilikuwa ni Marekani na Uingereza na kwamba utawala wa Kitaghuti wa Shah haukuwa na uthubutu wa kukabiliana na nchi hizo bali ulikuwa mtii wa amri zilizokuwa zikitolewa na nchi hizo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatollah Muhammad Ali Muvahidi Kermani ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kuomboleza tukio la kihistoria la kuawa shahidi Imam Hussein (a.s), Imam wa tatu wa Washia duniani kote na wafuasi wake watiifu na kueleza kuwa, mapambano yaliyoendeshwa na Imam Hussein (a.s) yameacha darsa na ibra kubwa kwa Waislamu ambapo moja ya ibra hizo ni kutowaogopa maadui. Khatibu wa sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo katika mji wa Tehran amesisitiza kuwa waumini wanapaswa kuwa na utulivu katika kukabiliana na adui na pia wawe na matarajio haya kwamba hatimaye watashinda.