AGHA JAWAD NAQVI

Kama ungeuonesha mzoga wa ng’ombe kwa mtu na kisha akasema kwamba mnyama huyu hakufa kwa sababu anaona mamilioni ya viumbe (minyoo) wakiwa katika harakati ndani ya mzoga wa ng’ombe huyu ambao wanakula, wanakunywa na kuzaliana, mara moja utabishana na kusema kwamba harakati hii ya minyoo ndani ya mzoga huu yenyewe ni ushahidi kwamba ng’ombe huyu amekufa. Kama minyoo hii isingekuwepo basi kungekuwa na uwezekano wa hoja, iwapo mnyama huyu yu hai au mfu. Hivyo sasa tunaweza kuhitimisha kwamba kama mamilioni ya minyoo inaonekana ikiwa katika harakati ndani ya mzoga wa kiumbe, basi kiumbe huyo hachukuliwi kuwa yu hai, ni mfu.

Tunaweza kuchukua mfano huu huu kuulekeza kwenye jamii. Wakati jamii ikifa kifo cha Umma basi watu wanaoishi ndani ya jamii hii iliyokufa hawawezi kuchukuliwa kama wako hai; kwa kweli mfano wao ni kama ule wa minyoo ndani ya mzoga. Kama mtu atasema katika mji wetu watu wana maduka makubwa, majumba, wanakula vyakula vya anasa, wana watoto, na wanawajibika kila mahali na wana familia kubwa, lakini jamii hii haina maisha ya “Umma”, basi harakati zote hizi na kula, kunywa kutaonesha kifo cha jamii hii. Kuishi maisha kama hayo ya minyoo ndani ya mwili uliokufa hakuchukuliwi kama maisha. Maisha yanayoendeshwa katika jamii iliyokufa ni maisha ya uvundo, wakati ambapo kama mtu atapita kwenye maisha haya atashika pua yake kujizuia na harufu mbaya ya jamii hii iliyokufa.

Minyoo hii inazaliwa wakati jamii inapokufa. Jukumu na kazi ya minyoo hii ni kunyonya tu damu ya jamii iliyokufa, kukwangua minofu kutoka kwenye jamii na kuitafuna. Hufikiria kazi yao ni kula tu rushwa, kuishi kwa riba, kutengeneza dunia yao na kufikiria tu masilahi yao binafsi. Hawajali kuhusu afya na ustawi wa jamii, wanafurahia kunyonya damu ya jamii na kubeba marundo ya minofu ya jamii na kupeleka majumbani kwao. Tunajisikia vibaya hata kuzungumzia kuhusu viumbe hawa, hii ni kwa sababu siku zote kiumbe aliye hai anajisikia vibaya kuhusu mwili uliokufa.