UMOJA WA WAISLAMU NA KUMTAMBUA ADUI NDIO DAWA YA MATATIZO YA ULIMWENGU WA KIISLAMU (2013/10/14 - 12:59)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Hamdu zote ni zake Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu na sala na salamu zimshukie Bwana wa Manabii na Mitume wa Mwenyezi Mungu na Aali zake watukufu na masahaba zake wema.

Kuwadia kwa msimu wa Hija kunapaswa kutambuliwa kuwa ni sikukuu kubwa ya Umma wa Kiislamu. Fursa kubwa inayoletwa na siku hizi zenye thamani katika miaka yote kwa Waislamu duniani ni kemia inayofanya muujiza ambayo iwapo itathaminiwa ipasavyo na kutumiwa vizuri inaweza kutibu magonjwa mengi ya ulimwengu wa Kiislamu.

Hija ni chemchemi ya baraka tele za Mwenyezi Mungu. Ninyi Mahujaji mliopata saada, mumepata fursa ya kuosha nyoyo zenu katika amali na ibada hii iliyojaa usafi na umaanawi na kutumia hazina hii ya rehma, izza na qudra kwa ajili ya kujiwekea akiba ya umri wenu wote. Msimu huu wa ibada ya Hija ni shule ya kujifunza na kujistawisha ambayo ina masomo ya kuwa wanyenyekevu na kujisalimisha kwa Mola Mlezi, kubeba majukumu waliyopewa Waislamu na Mwenyezi Mungu, kufanya jitihada, nishati na harakati katika kazi za dini na dunia, kurehemeana na kusameheana katika kuamiliana na ndugu, masomo ya ushujaa na kujiamini katika kukabiliana na matukio mazito na kuwa na matumaini na msaada wa Mola Karima katika kila mahala na katika kila kitu. Kwa ufupi tunasema kuwa, msimu wa ibada ya Hija ni uwanja wa kujenga shakhsia ya mwanadamu kwa mujibu wa vigezo vya Kiislamu. Kwa msingi huo mnaweza kujipamba humo kwa vito hivyo vya kiroho na kufaidika na hazina hiyo tukufu na kuchukua matunda yake kwa ajili ya nafsi zenu na zawadi kwa nchi, mataifa yenu na Umma mzima wa Kiislamu.

Hii leo Umma wa Kiislamu unahitajia zaidi wanadamu wanaoambatanisha pamoja amali, imani, usafi wa roho, ikhlasi, muqawama mbele ya maadui wenye vinyongo pamoja na kuijenga nafsi kiroho na kimaanawi. Hii ndiyo njia pekee ya wokovu wa jamii kubwa ya Waislamu kwa kipindi kirefu kutoka kwenye matatizo iliyotumbukia ndani yake ama kwa mikono ya adui au kutokana na udhaifu wa azma, imani na busuri.

Hapana shaka kuwa kipindi cha sasa ni kipindi cha mwamko na kupata utambulisho wa Waislamu; uhakika huu unaweza kuonekana waziwazi kupitia changamoto zinazozikabili nchi za Waislamu. Ni katika mazingira haya ndipo azma na irada inayoegamia kwenye imani, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, kuona mbali na tadbiri vinapoweza kuyapatia ushindi na fahari mataifa ya Waislamu katika changamoto hizi na kuyafikisha kwenye mustakbali wenye izza na utukufu. Kambi nyingine ambayo haiwezi kustahamili mwamko na izza ya Waislamu, imejitosa katika medani kwa nguvu zake zote na inatumia nyenzo zake zote za kiusalama, kinafsi, kijeshi, kiuchumi na kipropaganda kwa ajili ya kuwatibua na kuwakandamiza Waislamu na kuwashughulisha wao kwa wao. Hali ya nchi za magharibi mwa Asia kuanzia Pakistan hadi Syria, Iraq na Palestina, nchi za Ghuba ya Uajemi, na vilevile nchi za kaskazini mwa Afrika kuanzia Libya, Misri na Tunisia hadi Sudan na baadhi ya nchi nyingine, inaweka wazi mambo mengi. Vita vya ndani, taasubiri kipofu za kidini na kimadhehebu, machafuko ya kisiasa, kuenea ugaidi uliojaa ukatili, kujitokeza makundi na mirengo yenye misimamo ya kufurutu mipaka ambayo yanatumia mbinu za kaumu zilizokuwa zikiishi maisha ya kishenzi katika historia kama kupasua vifua vya wanadamu na kutafuna nyoyo zao, watu wanaobeba silaha wanaoua watoto na wanawake, watu wanaochinja vichwa vya wanaume na kuwabaka wanawake na wakati mwingine kufanya jinai hizo za kukirihisha na kuchafua moyo kwa kutumia jina na bendera ya dini, yote hayo ni matokeo ya mpango wa kishetani na kibeberu wa mashirika ya kijasusi ya wageni na tawala vibaraka wao katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ambayo yanatayarisha mazingira ya ndani kwa ajili ya matukio hayo na kuyaonjesha shubiri mataifa mbalimbali. Ni wazi kuwa katika hali kama hii hatuwezi kutarajia kuwa nchi za Waislamu zitajaza mapengo yao ya masuala ya kimaanawi na kiroho na kupata amani, hali bora ya maisha na maendeleo ya kisayansi na nguvu ya kimataifa ambavyo ndiyo baraka za mwamko na kupata utambulisho wa Kiislamu. Hali hii ya maafa inaweza kuutia ugumba mwamko wa Kiislamu na kuharibu utayarifu wa kiroho uliojitokeza katika dunia ya Kiislamu, na kwa mara nyingine kuyatumbukiza kwa muda mrefu mataifa ya Waislamu katika mkwamo, hali ya kutengwa na mporomoko na hatimaye kusahaulisha kabisa masuala muhimu ya Waislamu kama kadhia ya kuikomboa Palestina na mataifa mengine ya Waislamu kutoka kwenye makucha ya Marekani na Wazayuni. Tiba mujarabu na ya kimsingi inaweza kufupishwa katika sentensi mbili muhimu ambazo zote ni katika masomo muhimu ya ibada ya Hija:


Kwanza: Umoja na udugu wa Waislamu chini ya bendera ya Tauhidi.


Pili: Kumjua adui na kukabiliana na njama na mbinu zake. 

Somo kubwa la ibada ya Hija ni kuimarisha udugu na mshikamano. Hapa, katika ibada ya Hija, inazuiwa pia kufanya ubishani na malumbano. Vazi la aina moja, amali za aina moja, harakati za aina moja na mwenendo wa upole hapa katika Hija vina maana ya usawa na udugu wa watu wote wanaoamini tauhidi. Hili ni jibu la wazi la Uislamu kwa kila fikra, itikadi na wito unaowaondoa katika Uislamu baadhi ya Waislamu na watu wanaoamini al Kaaba na Tauhidi. Watu wenye fikra za kuwakufurisha Waislamu ambao wamekuwa wanasesere wa siasa za Wazayuni mahaini na waungaji mkono wao wa Kimagharibi ambao wanafanya jinai za kutisha na kumwaga damu za Waislamu wasio na hatia, na wale wanaojidai kushikamana na dini na kuvaa mavazi ya wanazuoni wa dini wanaochochea moto wa hitilafu kati ya Shia na Suni na wengineo mfano wao, wanapaswa kuelewa kwamba ibada ya Hija inabatilisha madai yao. Inashangaza kuona watu wanaotambua marasimu ya kujibari na kujitenga na washirikina ambayo ina asili katika amali ya Mtume Mtukufu (saw) kuwa ni mabishano yanayozuiwa katika Hija; watu hawa wenyewe ndio wanaochangia zaidi katika kuzusha machafuko ya umwagaji damu kati ya Waislamu.

Mimi, kama walivyo maulamaa wengi wa Kiislamu na wale wanaoumizwa na masuala ya Umma wa Kiislamu, ninatangaza tena kwamba, kila neno au amali inayochochea moto wa hitilafu kati ya Waislamu, kuvunjiwa heshima matukufu ya mojawapo ya makundi ya Waislamu au kukufurisha moja kati ya madhehebu za Kiislamu ni kuhudumia kambi ya ukafiri na shirki na kusaliti Uislamu; na amali hiyo ni haramu.

Kumtambua adui na mbinu anazotumia ndiyo nguzo ya pili. Kwanza kabisa hatupasi kughafilika na kumsahau adui mwenye kinyongo, na marasimu ya kumpiga mawe mara kadhaa shetani katika ibada ya Hija ni nembo ya kukumbuka suala hilo daima katika fikra na akili zetu. Pili ni kwamba hatupasi kufanya makosa katika kumtambua adui yetu asili ambaye hii leo ni kambi ya ubeberu wa kimataifa na kanali ya watenda jinai ya Kizayuni. 

Tatu ni kuwa, tunalazimika kuainisha vyema mbinu za adui huyo mkaidi ambazo ni kuzusha hitilafu kati ya Waislamu, kueneza ufisadi wa kisiasa na kimaadili, kutoa vitisho na vivutio kwa shakhsia na watu mashuhuri, kuweka mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya mataifa mbalimbali na kuzusha shaka katika imani na itikadi za Kiislamu na vilevile kuwatambua vibaraka na vikaragosi wao wanaowafanyia kazi kwa kujua au bila ya kujua.

Madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani yanaficha sura zao halisi kwa kutumia msaada wa zana za kisasa za vyombo vya habari na kutumia hila na ujanja mbele ya fikra za mataifa mbalimbali kwa madai ya kutetea haki za binadamu na demokrasia. Madola haya yanadai kutetea haki za mataifa ilhali mataifa ya Waislamu kila siku yanaona kwa macho na kuhisi kwa nyoyo moto wa fitina zao. Tunapotazama taifa linalodhulumiwa la Palestina ambalo kwa miongo kadhaa sasa linaendelea kujeruhiwa kwa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake, au katika nchi za Afghanistan, Pakistan na Iraq ambako ugaidi uliotengenezwa na siasa za ubeberu na vibaraka wao umeyafanya machungu kama shubiri maisha ya mataifa hayo, au nchini Syria ambayo inashambuliwa na chuki za mabeberu wa kimataifa na vikaragosi wao wa kieneo na imetumbukizwa katika vita vya umwagaji damu vya ndani kwa dhambi ya kuunga mkono harakati ya mapambano dhidi ya Wazayuni, au Bahrain au Myanmar ambako katika kila mojawapo ya nchi hizo Waislamu wanaosumbuliwa na mashaka mbalimbali wamesahaulika na maadui zao wanaungwa mkono, au mataifa mengine ambayo yanatishiwa mara kwa mara na Marekani na waitifaki wake kushambuliwa kijeshi au kuwekewa vikwazo vya kiuchumi au kukabiliwa na uharibu wa kiusalama, yote hayo yanaweza kuonesha vyema sura halisi ya vinara hawa wa mfumo wa ubeberu kwa walimwengu wote.

Shakhsia wa kisiasa, kiutamaduni na kidini katika maeneo yote ya ulimwengu wa Kiislamu wanalazimika kufichua uhakika huu. Huu ni wajibu wetu sote wa kidini na kiakhlaki. Nchi za kaskazini mwa Afrika ambazo kwa masikitiko makubwa zimekumbwa na hitilafu kubwa za ndani, zinalazimika kuliko nchi nyingine, kutilia maanani wajibu huu adhimu, yaani kumtambua adui, mbinu na njama zake. Kuendelea hitilafu kati ya mirengo mbalimbali ya kitaifa na kughafilika na hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hizo ni hatari kubwa ambayo hasara zake kwa Umma wa Kiislamu haziwezi kufidika haraka.

Hatuna shaka kwamba mataifa yaliyosimama kidete katika eneo hilo linaloonesha kielelezo cha Mwamko wa Kiislamu, kwa idhini yake Mwenyezi Mungu, hayataruhusu mshale wa saa urejee nyuma na kurejesha kipindi cha watawala waovu, vibaraka na madikteta; hata hivyo ni wazi kuwa kughafilika na nafasi ya madola ya kibeberu katika kuzusha fitina na kuingilia mambo yao ya ndani vitatatiza kazi zao na kuchelewesha kwa miaka mingi kipindi cha izza, usalama na hali bora ya kimaisha. Tuna imani kubwa na uwezo wa mataifa na nguvu iliyowekwa na Mwenyezi Mungu Mwenye hikima katika azma, imani na busuri ya watu na tumeiona na kuijaribu nguvu hiyo kwa macho yetu katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hima yetu ni kuyalingania mataifa ya Waislamu tajiriba hii ya ndugu zao katika nchi hii yenye fahari na isiyochoka.

Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu arekebishe hali za Waislamu na kuwaepusha na vitimbi vya adui. Vilevile namuomba Mwenyezi Mungu atakabali Hija na kuwapa uzima wa mwili na roho na tunu kubwa ya kimaanawi ninyi nyote Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu.

Wassalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh

Sayyid Ali Khamenei

5 Dhulhija 1434 Hijria

19 / Mehr/ 1392 Hijria Shamsia    (11 Oktoba 2013)