Ibrahim anachukua nafasi ya pande zote, akiwa anatukuzwa na Mayahudi, Wakristo na Waislam sawasawa. Qur’ani inaonyesha kabisa kwamba Mtume wa Uislamu alidai kuifuata dini (imani) ya Ibrahim ambaye aliwaita wafuasi wake Waislam1. Ahadith nyingi zenye kuhusu maisha yake ni sehemu ya urithi wa Kiislam na kwa kiwango kikubwa sana zimeathiri mwendo wa Kiislam na maadili.
Ibrahim alikuwa na watoto wawili wa kiume, Is’haak na Isma’il ambao walikuwa kimpangilio ni mababu wa Waisrael na wa Mtume wa Uislamu.
Ibrahim na Isma’il waliinua Ka’aba iliyoko Makka ambayo dini iliifanya mahali pa kukutania watu wote wa ulimwengu mzima. Na miaka ilivyokuwa inapita hii iliota nafasi ya maana sana kwa kizazi cha Ibrahim.
Uislamu unatilia umuhimu mkubwa maelezo ya kimungu yasemayo kwamba Ibrahim alikuwa ameamriwa na Mungu kumtoa kafara mwanawe Isma’il, na akawa tayari kwa kutekeleza mtihani huo mkubwa kwa utulivu mkubwa. Isma’il, pia aliridhia utekelezwaji wa maatakwa ya ki-Mungu, lakini kitendo hasa cha kuchinja kiligeuzwa katika wakati wa mwisho kabisa, uingiliaji kati wa mbinguni ukambadilisha Isma’il kwa mnyama ambaye alitolewa karara badala yake. Hata hivyo ilitangazwa kwamba kafara hilo ambalo limeakhirishwa lingekuwa lije kufanywa kwa chinjo kubwa katika njia ya Mwenyezi Mungu.2 Uislamu unaadhimisha tukio hili kila mwaka kama Idd al-Adh’ha au Id al-Qurbani, sherehe ya kuchinja (kutoa kafara).
Vizazi vya watoto wawili wa Ismail, Nabit na Qaydhan vilifanya makazi katika Hijaz na vikazaana na kuongezeka kwa idadi kubwa sana. Mmoja wa watoto wa mwanzoni wa Nabit, aliyeitwa Adnaan alikua na kupata umaarufu mkubwa. Vizazi ishirini na moja na karibuni miaka 600 inasimama kati yake na Mtume wa Uislamu ambaye nasaba yake kwa Adnaan haipingiki, na imetolewa katika kiambatisho “A”. Hata hivyo, bado kuna wasiwasi kwamba ni yupi katika watangulizi wake alijipatia jina la Quraish.
Wakati mmojawapo wa mababu (wahenga) wa Mtume, Qussay, vizazi vitano tu vilipita kutoka yeye, alipopanda madarakani, akaunganisha wato- to wa Nadhr na wakaling’oa kabila la Khuzaa likiwa ndiyo walezi wa Ka’aba, wakaichukua Makka mikononi mwao, wakajenga makazi hapo, wakajenga ukumbi wa halmashauri, wakapanga kanuni za sheria za mwenendo wa kijamii na wakaandaa utaratibu wa kuwapatia chakula na maji mahujaji waendao Hijja3
Abd Manaf, mwana wa Qusay, alijipatia jina (umaarufu) mwenyewe katika wakati wa uhai wa baba yake.4 Mwanae Amri, aliyefahamika zaidi kama Hashim aliwazidi ndugu zake na akapendelewa peke yake kupanga mpango wa kuwapatia maji na chakula mahujaji waendao Hijja.
Alianzisha safari (misafara) za kibiashara kwenda Sham (Syria) na Yemen, na katika wakati wa uhaba aliwahudumia watu wa Makka kwa kuwapatia vipande vya mikate iliyokatwakatwa na kuchovya kwenye supu, akajipatia jina la Hashim, ‘Hashm’ likiwa na maana ya “kuvunja vunja’, meng’enya n.k. kwa lugha ya kiarabu.5
Hashim alirithiwa na ndugu yake aliyeitwa Muttalib ambaye alifuatwa na mtoto wa Hashim, Shayba, ajulikanaye kama Abd al-Muttalib, ambaye aliwapita kwa utukufu na madaraka wale wote waliomtangulia kabla yake6 na akapewa cheo cha Sayyidul-Batha’ (kiongozi wa Makka)7. Wawili kati ya watoto wake wa kiume walikuwa Abdallah na Abu Talib.
Abdul-Muttalib alikuwa ameapa kumtoa mhanga mwanawe Abdallah, lakini aliweza kuepuka kufanya hivyo kwa kutoa mhanga mbadala wa ngamia mia moja.8
Abdallah alimtangulia baba yake kufa, na Abu Talib akarithi shughuli na utukufu wote wa baba yake. Jukumu lake kubwa kabisa, hata hivyo, lilikuwa la uangalizi wa malezi ya mtoto yatima wa Abdullah, Muhammad.
Mapema katika maisha yake mtume huyu wa baadaye alijipatia jina la Amin (mwaminifu) kutokana na uaminifu wake na kutegemewa kwake. Waarabu walikabidhi vitu vyao vya thamani kwake kwa ajili ya hifadhi salama na walikuwa wakikubali maamuzi yake katika masuala muhimu.
Uvunjikaji wa sheria wa jumla na uonevu ulifuatia kifo cha Abdal-Muttalib na dhuluma dhidi ya wanyonge na wageni walikaa bila ya kuadhibiwa. Wakati Muhammad bin Abdullah alikuwa amekaribia miaka ishirini aliungana na ndugu zake na baadhi ya makabila mengine ya Ki-Quraishi kuanzisha mapatano (mkataba) muhimu sana (hilf-alfudul), ambao kwawo wale wote waliohusika walikula kiapo ambacho kiliwalazimisha kuunga mkono njia ya wenye kuonewa, kupata haki za waliodhulumiwa waliotenzwa nguvu na hasara zao kufidiwa.
Kiapo hiki kilikwenda kinyume na msimamo wa desturi wa Ki-Arabu ambao ulihusisha kutetea fungamano (muungano) la kikabila tu, ambalo wakati mwingine lilikuza migogoro midogo midogo na kufikia kuwepo visasi vya kurithi vya kikabila. Kizazi cha Hashim kiliongoza katika kujaribu kuondosha hali hii ya mwenendo wa kitaifa na kuifanya haki, uadilifu na mwenendo mwema viheshimike mahali pote.
Ali alizaliwa na Abu Talib ndani ya Ka’aba mjini Makka, upendeleo ambao hakuupewa mtu mwingine yeyote yule. Muhammad wakati huo alikuwa na umri wa takriban miaka 30 (thelathini). Wakati Ali alipokuwa bado ni mchanga, njaa iliipiga Makka, na ikamwacha Abu Talib katika mazingira magumu sana, hivyo Muhammad alimchukua Ali kwenda kuishi pamoja naye ili kumwondolea ami yake sehemu ya mzigo wake.
Karne ya saba ya zama za Ukristo ilikuwa kipindi kisichokuwa na ufumo cha ujahilia wakati Uislamu ulipotokea huko Uarabuni. Kwa miaka kadhaa ujumbe wa dini (imani) mpya ulihubiriwa kwa siri sana. Kisha Mtume akaamriwa na Mungu aufikishe kwa ndugu zake wa karibu.9
Mtume kwa hiyo aliwaita watoto wote wa kizazi cha Abdul Muttalib, na akijitangaza mwenyewe kama Mtume wa Mwenyezi Mungu, alilingania upweke wa Mungu (Tawhid), na akawauliza wageni waliokusanyika hapo kama ni nani miongoni mwao angemuunga mkono katika kueneza ujumbe wa Uislamu kwa kuelewa wazi kwamba huyo angekuwa ni ndugu, wasii na mrithi wa Mtume. Suala hili aliliuliza kwa kulirudia rudia, lakini kila wakati alikuwa ni Ali tu, ingawa alikuwa bado ni mdogo sana, ndiye aliyejibu, akimuahidi usaidizi kamili. Mtume alimtangaza Ali kama ni ndugu, wasii na mrithi wake.
Kwa ueneaji wa Uislamu, uabudu masanamu ulifikia kukataliwa waziwazi, na kwa sababu hiyo Maquraishi wakawa maadui wa Mtume wasio na huruma na wakaazimia kumdhuru. Madhali Abu Talib alikuwa hai haiba yake yenye nguvu ilimzuia Mtume wa Uislamu kupatwa na huzuni.
Baada ya vifo vya Abu Talib na mke wa Mtume, Khadija, mateso ambayo alikuwa akabiliana nayo yaliongezeka ukali na marudio ya mara kwa mara, na Mtume akaamua kuondoka kwenda Madina. Walipozipata habari hizi, maquraishi waliizunguka nyumba yake usiku mmoja ili wamuue, lakini Mtume aliwatoka akimwacha Ali amelala katika kitanda chake.10
Kutoka kwa Mtume kwenda Madina, kuitwako Hijra, hakukuzuia uchokozi dhidi ya Waislam, na vita kama vile vya Badr, Uhud na Khandaq (mtaro) ilibidi vipiganwe, na ulikuwa wakati wote ni upanga wa Ali ndio ulileta ushindi wa kung’ara kwa Uislamu.
Mtume alimwozesha binti yake Fatima kwa Ali kwa mujibu wa amri ya ki-Mungu, na aliyakataa maombi ya wengine wengi kwa ajili ya posa ya kipande hiki cha nyama na damu yake mwenyewe,11 kiongozi wa wanawake wa peponi, ambaye kwamba Mtume alitumia kusimama wakati wowote Fatima alipokuwa akimtembelea. Kutokana na wazazi wa heshima kama hao, Ali na Fatima, walizaliwa watoto wawili wa kiume, Hasan na Husein.
Vipi Husein angeweza kusahau desturi za hali ya juu na sifa zisizo na kifani ambazo familia yake walikuwanazo siku zote tangu zama za kale? Aliwakilisha kawaida ambayo ilikuwa na rekodi isiyovunjika ya utoaji mhanga. Ni lazima awe amesikia jinsi gani babu yake mkubwa (mhenga) Ibrahim alivyoandaa kumtoa kafara mwanawe kwa kutii amri ya mbinguni, jinsi gani babu yake Abdul-Muttalib, alivyomtoa kafara mwanawe Abdullah, jinsi gani mhenga wake Hashim alivyoitumia mali kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanadamu, na jinsi gani familia yake ilivyochukua wajibu mkubwa katika kuifanya hilf al-fudul kuwasaidia waliokuwa wanateswa na kusimamia haki kwa ajili ya wanaokandamizwa. Kwa hakika Husein alishikilia kwamba kiapo hicho kiliendelea kuwa halali kutumika.
Husein alijua kwamba babu yake mzaa mama yake, Mtume Muhammad (s.a.w.w.), alipatwa na taabu nyingi na mateso yasio na mwisho katika kuu- tangaza na kuueneza Uislamu, kwamba babu yake mzaa baba yake, Abu Talib, alimlinda Mtume na Uislamu kwa nguvu zake zote na uwezo wa haiba yake, kwamba wakati wowote hatari ilipotishia Uislamu, wa kwan- za kukabiliana nayo na kuipiga vita hiyo, bila ya kujali matokeo yote yatakayomtokea, alikuwa ni baba yake, Ali bin Abi Talib.
Ni kawaida tu kwamba simulizi za matendo haya bora na mwenendo wa wahenga wake ni lazima viwe vimewasha moto wa fikira na mawazo ya kijana Husein na kuzaa ndani mwake tamaa ya kutenda matendo makubwa kama hayo ya ucha-Mungu, ya utii kwa utashi wa Mungu, kutumikia haki na kuiletea heshima familia yake tukufu.
1. Qur'an 2:128
2. Qur’an; 37:107
3. Ibn Is’haaq, al-Sira, uk. 52-56
4. Ibn Is’haaq, uk. 55
5. Ibn Is’haaq, uk. 58
6. Ibn Is’haaq, uk. 61
7. Ibn Is’haaq, uk. 25
8. Ibn Is’haaq, uk. 66 - 68
9. Qur’ani; 26:214
10. Ibn Is’haaq, uk. 223
11. Sahih Bukhari, Juz. 2, uk. 74, 185, 189 na Sahih Muslim, Juz. 2, uk. 290