Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa changamoto kuu zinazoyakabili Mapinduzi ya Kiislamu hivi sasa, ni kukabiliana na tawala zenye kupenda kujitanua duniani katika jitihada za mapinduzi hayo za kueneza ujumbe wake wa Kiislamu duniani ambao ni kujiepusha na dhuluma. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo alipokutana na makamanda na maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kuashiria kuwa, mantiki ya dhuluma na ukandamizaji daima imekuwa ikikabiliana na linganio la kujiepusha na dhuluma, suala lililopelekea mwangwi wa mapinduzi hayo utoke nje ya mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupokelewa kwa mikono miwili na watu wa mataifa mbalimbali duniani. Amesema kuwa, ujumbe wa mapinduzi ya taifa la Iran, umekuwa ukipambana vikali na mataifa ya kibeberu, tawala zenye kufungamana nao na mitandao vamizi ya kimataifa, katika hali ambayo utawala wa kimabavu na waitifaki wake, unajitahidi kueneza satwa yake kupitia mambo makuu matatu ambayo ni kueneza vita, umasikini na ufisadi. Amesisitiza kuwa dini Tukufu ya Kiislamu inapambana na mambo hayo na kwamba hiyo ndio changamoto kuu ambayo imekuwa ikiikabili Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema kuwa, kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita utawala wa Kiislamu hapa nchini Iran, umekuwa ukikabiliana na matatizo na hujuma mbalimbali za madola ya kibeberu.
SHEIKH PONDA ANYIMWA DHAMANA, AREJESHWA RUMANDE.
Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Nchini Tanzania, Sheikh Ponda lssa Ponda, amerudishwa mahabusu baada ya kunyimwa dhamana leo katika kesi yake iliyoendelea kusikilizwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawdhi mkoa wa Morogoro.
Kama kawaida umati mkubwa wa waumini wa dini ya Kiislamu ulifurika mahakamani hapo hii leo kusikiliza kesi hiyo namba 128 ya mwaka 2013 ambayo imeahirishwa hadi Oktoba 1 mwaka huu. Sheikh Ponda alipigwa risasi tarehe 10 Agosti baada ya kutoa mhadhara katika msikiti mmoja mjini hapo. Hata hivyo polisi walikanusha kumpiga risasi kiongozi huyo wa kidini nchini Tanzania. Aidha kiongozi huyo amekuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi katika gereza la Segerea anakozuiliwa hadi sasa sanjari na kuwekwa masharti makali ya kumuona, suala ambalo liliwapelekea Waislamu kutishia kukinyima kura chama tawala CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015. Mwenyekiti wa kongamano alikotoa hotuba kwa mara ya mwisho Sheikh Ponda kabla ya kupigwa risasi, Sheikh Idd Mussa Msema, alisema kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu begani na maafisa wa polisi waliokuwa wakijaribu kumkamata.
Jeshi la Syria limefanikiwa kuyadhibiti maeneo ya Rif Dimashq karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Damascus na kuwaangamiza wapiganaji 50 wa magaidi wanaoendesha machafuko katika nchi hiyo. Kanali ya televisheni ya al-Mayadin imetangaza kuwa, vikosi vya Syria vimefanya operesheni kubwa ya kijeshi katika kitongoji cha Shab'a huko al-Ghouta Mashariki palipokuwa maficho ya magaidi wa Jabhat al-Nusra na kufanikiwa kudhibiti maeneo hayo. Aidha jeshi la Syria limedhibiti barabara zinazoelekea katika maeneo hayo. Eneo la al-Ghouta Mashariki huko Rif Dimashq ni miongoni mwa ngome na maficho ya magaidi wa Jabhatun Nusra.
IRAN INATAKA AMANI KATIKA LANGO BAHARI LA HORMOZ.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran imedhamiria kwa dhati kushuhudia amani ikidumishwa katika lango la kistratejia la Hormoz.
Rais Hassan Rouhani amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitaka lango bahari la Hormoz kuwa lango la amani, urafiki na udugu.
Rais wa Iran ameyasema hayo leo katika mazungumzo na Sayyid Badr bin Saud al Busaidi, Waziri wa Oman anayehusika na Masuala ya Ulinzi aliyepo ziarani hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Iran ameshiria pia uhusiano wa kirafiki wa muda mrefu kati ya Iran na Oman na kutaka kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili hizo katika nyanja mbalimbali khususan katika sekta ya ulinzi.
Naye Waziri wa Oman anayehusika na Masuala ya Ulinzi ya nchi hiyo amesifu mchakato wa ushirikiano wa kiulinzi kati ya Oman na Iran kuwa mzuri na kueleza kwamba anataraji uhusiano kati ya Tehran na Muscat utaimarika zaidi katika nyanja zote.
Waziri wa Oman anayehusika na masuala ya Ulinzi Sayyid Badr bin Saud al Busaidi aliwasili jana hapa nchini Iran akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi yake.Chanzo cha habari
http://kiswahili.irib.ir/habari