SHEIKH TWAYYIB: WAMAGHARIBI WAHESHIMU UISLAMU.

Sheikh wa Chuo Kikuu cha al-Azhar nchini Misri Ahmad Muhammad at-Twayyib amesisitizia udharura wa nchi za Magharibi kuheshimu dini tukufu ya Kiislamu.

Sheikh Ahmad at-Twayyib ameyasema hayo alipokutana na balozi wa Vatican nchini Misri Van Paul Goupil. Amevitaja kavunjiwa heshima matukufu ya dini ya Kiislamu kuwa ni mstari mwekundu na kuongeza kuwa, Uislamu ni dini iliyojumuisha matukufu yote ya mwanadamu na kwamba, Waislamu wamejiandaa kushirikiana na pande zote kwa lengo la kueneza uadilifu na maendeleo duniani. Amekosoa vikali mienendo ya Wamagharibi katika kuchafua sura ya Uislamu na kusema kuwa, dini ya Kiislamu si ile inayoarifishwa na Wamagharibi.

Kwa upande wake balozi wa Vatican nchini Misri Van Paul Goupil amesema kuwa, Vatican inaiheshimu dini ya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla na kwamba, inafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuinua kiwango cha ushirikiano na uelewano baina ya Wakristo na Waislamu lengo kuu likiwa ni kuimarisha uadilifu na amani duniani.


GENERALI GOLAN: HAKUNA WA KUMPINDUA RAIS ASSAD.

Meja Jenerali Yair Golan mmoja wa makamanda wa  ngazi za juu wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel amenukuliwa na gazeti la Jerusalem Post akisema kuwa, Rais Bashar Assad wa Syria anaweza kuendelea kubaki madarakani kwa miaka mingine kadhaa, licha ya kushadidi  mapigano ya ndani nchini humo.

Meja Jenerali Golan kamanda wa majeshi ya Israel yaliyoko kwenye mpaka wa utawala huo na Syria ameongeza kuwa, hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuuangusha utawala wa Rais Assad katika miaka ya hivi karibuni. Golan amedai kuwa, Syria, harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni maadui wakubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Matamshi ya kamanda wa jeshi la Israel yanatolewa katika hali ambayo, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani pamoja na watawala wa baadhi ya nchi za Kiarabu zinaisakama Syria kutokana na misimamo yake imara ya kuunga mkono kikamilifu mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wakati huo huo,Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia, imetangaza kuwa, wafungwa 1,239 waliohukumiwa adhabu ya kifo nchini humo wameachiliwa huru kwa masharti wapelekwe Syria kwa lengo la kupambana na majeshi ya nchi hiyo.


RUSSIA, MAREKANI ZATOFAUTIANA RIPOTI YA UN KUHUSU SYRIA.

Marekani na Russia zimetofautiana kuhusu ripoti iliyotolewa na wachunguzi wa Umoja wa Taifa kuhusu matumizi ya silaha za kemikali huko Syria. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power amesema ripoti hiyo inaonyesha wazi kuwa, serikali ya Syria ndiyo iliyotumia silaha za kemikali Agosti 21 viungani mwa mji wa Damascus. Bi. Samantha amesema makombora yaliyotumiwa ni ya kitaalamu ambayo waasi hawawezi kuyapata. Naye balozi wa Russia katika umoja huo, Vitaly Churkin amesema kuwa, Ripoti hiyo ya wataalamu wa UN haijataja ni nani aliyetumia silaha hizo na hivyo madai ya Marekani hayana msingi wowote. Churkin amesema baadhi ya wapinzani wa Rais Asad ni makamanda wa zamani wa jeshi ambao waliondoka serikalini na rundo kubwa la silaha yakiwemo makombora na inawezekana walitumia makombora hayo ili ionekane kwamba serikali ndiyo iliyohusika. Russia imesisitiza kuwa ina ushahidi wa wazi unaoonyesha wapinzani ndio waliotumia silaha za kemikali Agosti 21 dhidi ya raia ambapo zaidi ya watu 1000 waliuawa. Marekani, Uingereza na Ufaransa zinaanda rasimu ya azimio litakalopigiwa kura kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Maraifa ingawa Russia imesema baadhi ya vipengee vya azimio hilo sharti vifutwe la sivyo italipigia kura ya veto. Chanzo cha habari

http://kiswahili.irib.ir/habari