Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema mgogoro wa sasa nchini Syria umesababishwa na fikra ya demokrasia ya kiliberali ya nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani. Ayatullah Ahmad Khatami aidha amelaani vikali vitisho vya vita dhidi ya Syria hasa kutoka Marekani. Halikadhalika amelaani kuendelea mauaji ya watu wa Syria na kuongeza kuwa, 'ni takribani miezi 30 sasa ambapo watu wa Syria wanakabiliwa na hujuma ya magaidi wanaopata himaya ya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudi Arabia, Uturuki na Qatar. Maelfu ya watu wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto wameuawa kwa umati katika hujuma hizo.' Ayatullah Khatami amesema ushahidi unaonyesha kuwa Marekani imekuwa ikiwaunga mkono kifedha na kwa silaha magaidi wa Al Qaeda nchini Syria. Amesema kuwa Al Qaeda ni mtekelezaji wa sera za Marekani nchini Syria na kuongeza kuwa miaka michache iliyopita Marekani iliivamia Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi wa Al Qaeda lakini sasa inashirikiana na magaidi hao. Ayatullah Khatami amesema Wamarekani wanadai eti rais Bashar al Assad wa Syria amekiuka haki za binaadamu katika hali ambayo Marekani imetenda jinai za kuogofya huko Afghanistan na Iraq. Amesema Marekani ni mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binaadamu duniani. Ayatullah Khatami amesema serikali ya Syria haijatumia silaha za kemikali kwani jeshi lake lililikuwa limepata mafanikio makubwa sana dhidi ya magaidi katika miezi ya hivi karibuni.
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema nchi yake itaisiadia Syria iwapo nchi hiyo itavamiwa kijeshi.
Akizungumza leo baada ya kumalizika kikao cha viongozi wa nchi za G20 katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia, Putin amesema nchi yake imekuwa ikiisaidia Syria kwa silaha, kiuchumi na kibinaadamu na itaendelea kufanya hivyo.
Putin amesema madai kuwa serikali ya Syria imetumia silaha za kemikali ni uzushi. Ameongeza kuwa magaidi ndio waliotumia silaha hizo za kemikali ili kuchochea hujuma ya kijeshi dhidi ya Syria. Matamshi hayo ya Putin yamekuja baada ya Marekani na waitifaki wake wachache kuzidisha ngoma za vita dhidi ya Syria kwa madai kuwa eti jeshi la Syria limetumia silaha za kemikali katika mapambano dhidi ya magaidi. Serikali ya Syria imekanusha vikali madai hayo na kusema magaidi wanaopata himaya ya Marekani, Qatar, Saudi Arabia, Israel na Uturuki ndio ambao wametekeelza hujuma kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia.
Rais Vladimir Putin wa Russia Jumanne
wiki hii alionya kuwa nchi yake ina mipango yake ya siri ya kukabiliana
na shambulio tarajiwa la kijeshi la Marekani dhidi ya Syria.
Akizungumza katika mahojiano na Kanali
ya Kwanza ya Televisheni ya Russia, Putin alisema bado ni mapema
kubainisha wazi mipango ya Russia ya kukabiliana na uvamizi tarajiwa wa
kijeshi nchini Syria.
Mapema wiki hii pia Putin alisema kuwa,
tuhuma za utumiwaji silaha za kemikali zinazoelekezwa kwa serikali ya
Syria, ni upuuzi mtupu. Aidha rais huyo wa Russia alimhutubu rais wa
Marekani kwa kusema kuwa, Obama ambaye ametunukiwa tuzo ya amani ya
Nobeli, anatakiwa kufikiria mara mbili juu ya vita vitakayowalenga raia
wasio na hatia huko Syria, ikiwa uvamizi huo utatimia.
Rais Barack Obama wa Marekani amekaidi wito wa viongozi wa dunia ambao wamemtaka asitishe mpango wake wa kuivamia Syria kijeshi. Aghalabu ya viongozi wa nchi muhimu duniani kiuchumi G20 ambao wamemaliza mkutano wao leo huko Saint Petersburg Russia wamemtaka Obama afutilie mbali mpango wake wa kuishambulia Syria. Duru za kidiplomasia zinasema Obama alionekana kutengwa katika kikao hicho kwani ni nchi tatu tu ambazo zimeunga mkono wazi wazi mpango wake wa kivita dhidi ya Syria. Nchi hizo ni Ufaransa, Saudi Arabia na Uturuki. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon akizungumza pembizoni mwa kikao cha G20 amekiri kuwa ameshindwa kuzishawishi nchi zingine duniani zijiunge naye pamoja na Marekani katika kuivamia Syria kijeshi.
Rais Vladimir Putin wa Russia na mwenzake wa China Xi Jinping wamejitokeza wazi kupinga hujuma yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria. Aidha India, Indonesia, Argentina, Brazil, Afrika Kusini na Italy pia zimepinga wazi uvamizi wa kijeshi Syria. Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye amehudhuria kikao hicho pia amepinga vikali hujuma yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria. Kwa upande wake Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria Lakhdar Brahimi amesema hakuna nchi yoyote yenye haki ya 'kuchukua sheria mikononi mwake' na kuanzisha vita dhidi ya Syria pasina kuwepo idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Chanzo cha habari
http://kiswahili.irib.ir/habari