MAREKANI ITAPATA PIGO LITAKALOWADHURU


Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesisitiza kuwa, Wamarekani wanatenda kosa kubwa nchini Syria na kwa msingi huo, watapata pigo litakalowadhuru. Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo alipokutana na Ayatullah Mohammad-Reza Mahdavi Kani, Mkuu wa Baraza la Maulamaa Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na wajumbe wa baraza hilo hapa mjini Tehran. Kiongozi Muadhamu ameashiria njama za Uistikbari zenye lengo la kutatua matatizo ya eneo la Mashariki ya Kati kwa mujibu wa maslahi yao na kusema, kwa muda mrefu madola hayo ya kibeberu yamekuepo katika eneo hili, huku yakitumia mabavu na ukatili na kutaka kufanya kila njama za kutaka kumaliza harakati za muqawama, lakini hata hivyo huko nyuma hayakuweza na baada ya hapa pia hayatoweza. Amesema lengo kuu la mabeberu katika eneo hili ni kutaka kulidhibiti eneo kwa maslahi ya utawala haramu wa Kizayuni. Ameongeza kwa kusema kuwa, kadhia ya hivi karibuni kuhusiana na silaha za kemikali, ina lengo lililoko nyuma ya pazia na wala si kwa lengo la kutaka kutetea haki za binaadamu. Akiashiria harakati za kundi kibaraka linalowakufurisha Waislamu wengine linalotumia jina la Suni na kundi lingine kibaraka linalotumia jina la Shia amesema, wasomi wote wa Kishia na Kisuni lazima wawe macho ili hitilafu zilizoko baina ya madhehebu za Kiislamu zisije zikaanzisha kambi mpya za kukabiliana na kuwafanya wakaghafilika na adui yao hasa. Kwa upande mwingine ameashiria juu ya Mwamko wa Kiislamu na kusema kuwa, yeyote yule anayedhania kuwa, Mwamko wa Kiislamu umemalizika, basi anakosea, kwani mwamko huo umeenea katika jamii mbalimbali za Kiislamu, na kile kinachoshuhudiwa hii leo katika eneo ni njama za Uistikbari ukiongozwa na Marekani, kutaka kuuzima mwamko wa Kiislamu duniani.