IMAM KHOMEIN ALIIBUA MWAMKO WA KIISLAMU.


Mwenyekiti wa Baraza la Maulamaa Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran amesema kuwa Hayati Imam Khomeini MA alipelekea kuibuka mwamko wa Kiislamu duniani. Ayatullah Mohammad-Reza Mahdavi Kani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran wakati akifungua Kikao cha 14 cha baraza hilo. Ameongeza kuwa utendaji kazi wa Imam Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo ambalo lilipelekea kuibuka mwamko wa Kiislamu duniani. Ayatullah Kani pia ameashiria kushiriki kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi wa rais wa Juni 14 na kusema rais aliyechaguliwa anapaswa kutenda kazi yake kwa mujibu wa matakwa ya wananchi.

Kikao hicho cha siku mbili pia kimehudhuriwa na rais wa Iran Dkt. Hassan Rohani, Mkuu wa Baraza la Kulinda Katiba Ayatullah Ahmad Jannati na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo Ayatullah Hashemi Rafsanjani pamoja na mkuu wa Vyombo vya Mahakama Ayatullah Sadeq Amoli ambao wote ni wanachama. Baraza la Maulamaa Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu ni chombo cha wanazuoni wa Kiislamu waliofika katika ngazi za juu ambao huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi katika uchaguzi wa kitaifa. Baraza hilo lenye wanachama 86 huwa na kikao mara mbili kwa mwaka ambapo hujadili na kuchunguza masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa.