Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Barack Obama wa Marekani
katika siku hizi ameamua kuvaa gwanda la vita na kupiga ngoma za vita.
Rais huyo wa Marekani ambaye alipewa zawadi na amani ya Nobel mwaka 2009
anafanya kila awezalo kuanzisha mashambuzi ya kijeshi dhidi ya Syria.
Juhudi kubwa za kutaka kuanzisha vita za Obama zimefikia kiasi kwamba
ameamua kuungana na mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi wa rais mwaka
2008 John MacCain kupigia debe mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria.
Hata hivyo kuungana kwa wapinzani hao wawili wa jana katika kupiga ngoma
za vita dhidi ya Syria hakuna maana kwamba wanachama wote 535 wa
Congresi ya Marekani pia wanaafikiana juu ya suala hilo.
Japokuwa aghlabu ya wanachama wa Congresi ya Marekani
wanapinga utawala wa sasa wa Syria na wanatarajia kuona Rais Bashar
Assad akipinduliwa, lakini wakati huo huo wana wasiwasi mkubwa kuhusu
suala la kunzisha vita vingine Mashariki ya Kati. Kwa sasa Marekani imo
katika vita vilivyogharimu fedha na maisha ya watu wengi huko
Afghanistan na operesheni nyingi za kijeshi katika pembe mbalimbali za
dunia ikiwa ni pamoja na huko Yemen, Pakistan na Somalia. Vita hivyo
vinaunguza mabilioni ya walipa kodi wa Marekani. Kwa mfano tu katika
vita vya Iraq na Afghanistan pekee, Marekani imetumia dola zaidi ya
trilioni moja na hivyo kuvifanya vita vilivyogharimu fedha nyingi zaidi
katika historia baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Katika hali ya sasa ambapo ustawi wa uchumi wa Marekani ni
wa karibu asilimia mbili tu na asilimia 7 ya nguvu kazi ya nchi hiyo
haina ajira, wabunge wa Marekani wana wasiwasi mkubwa kuhusu suala la
kuanzisha vita vyenye gharama kubwa huko Syria. Vilevile tajiriba ya
mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iraq imeonesha kuwa, tathmini ya awali
kuhusu gharama za vita kabla ya vita vyovyote haiwezi kutegemewa hata
kidogo. Hii ni pamoja na kuwa uwezekano wa kuuliwa kwa askari wengi wa
Marekani katika vita vinavyotaka kuanzishwa na nchi hiyo huko Syria
unaitia kiwewe jamii ya Marekani ambayo hadi sasa bado inazika maiti za
askari wa nchi hiyo wanaouawa huko Afghanistan.
Wakati huo huo wabunge wa Marekani wana wasiwasi kwamba
mashambulizi hayo ya Obama yanayodaiwa kuwa yatalenga vituo na maeneo
maalumu nchini Syria, yatatoka katika mkondo wake na kuzusha moto katika
eneo zina la Mashariki ya Kati. Hii ni pamoja na kuwa hakuna mbunge
hata mmoja wa Marekani anayeweza kudhamini kwamba, mashambulizi ya
makombora ya Syria hayataikumba Israel. Suala hilo lina umuhimu mkubwa
kwa lobi ya Israel ndani ya Congresi ya Marekani kuliko hata suala la
kutumiwa silaha za kemikali nchini Syria.
Wakati huo huo kwa mtazamo wa badhi ya wabunge wa Congresi
ya Marekani, hakuna haja ya kutangaza vita wakati Marekani
haijashambuliwa na nchi yoyote. Hata hivyo Rais Barack Obama anatumia
kisingizio cha kutumiwa silaha za kemikali huko Syria kwa ajili ya
kuhalalisha hujuma ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo. Kwa msingi huo iwapo
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitapasisha azimio lolote la
kuidhinisha vita huko Syria, basi itakuwa vigumu mno kwa Rais wa
Marekani kuikinaisha Congresi juu ya udharura wa kujipa nafasi ya polisi
ya dunia.
Hayo yote mpenzi msikilizaji yanamfanya rais Barack Obama
wa Marekani aliyewahi kutunukiwa tuzo ya amani ya Nobel aonekane katika
joho la wapiga ngoma za vita. Hata hivyo iwapo Obama hatafanikiwa
kuishawishi Congresi juu ya udharura wa kuanzishwa mashamnbulizi dhidi
ya Syria basi hilo litakuwa pigo kubwa kwa shakshia yake. Ni kwa msingi
huo ndiyo maana baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vikaiita hatua
ya Obama ya kulirejesha suala la kuanzisha vita dhidi ya Syria kwenye
Congresi ya nchi hiyo kuwa ni mchezo wa kamari ya kisiasa ambayo katika
hali zote mbili, yaani kuingia vitani au la, Obama mwenyewe ndiye
atakayeshindwa na kulamba mweleka.RAIS ASSAD AIONYA UFARANSA KUHUSU UCHOKOZI WAKE.
Rais Bashar al-Assad wa Syria ameionya Ufaransa na kuitahadharisha kuhusiana na chokochoko yoyote ile dhidi ya nchi yake. Akizungumza katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Ufaransa la Le Figaro amesema kuwa, madai kwamba, vikosi vya Syria vilifanya mashambulio ya silaha za kemikali Agosti 21 mwezi uliopita huko kusini mwa nchi hiyo ni upuuzi mtupu. Rais Assad ameionya Ufaransa na kuitaka isianzishe chokochoko yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria. Rais wa Syria ametahadharisha kwamba, shambulio dhidi ya Syria litakuwa na matokeo mabaya mno. Amesema, watu wanaoituhumu Syria kwamba, imefanya mashambulio ya silaha za kemikali wanapaswa kutoa ushahidi badala ya kupiga domo kaya tu. Rais Assad amezipa changamoto Marekani na Ufaransa kwa kuziambia kwamba, kama zina ushadidi basi ziutoe badala ya kuendelea kupiga ngoma ya vita dhidi ya Syria. Chanzo cha habari http://kiswahili.irib.ir/habari